KONA YA MSTAAFU: Mstaafu anapoishia kujiuliza deni la taifa linamhusuje…

Mstaafu wetu wa Kima Cha Chini ameshtuka sana wiki iliyopita pale Dodoma Siri- Kali ilipomwambia kuwa yeye ni mmoja wa Watanzania milioni 64 wanaodaiwa Shilingi milioni moja na laki sita kila mmoja, kama sehemu yake kati ya Shilingi 107 trilioni ambazo nchi yake hii aliyoijenga mwenyewe inadaiwa. Amechoka kabisa!

Si amechoka kabisa tu, bali pia ameshtuka mno kiasi cha kupata shikizo la damu au BP na kuharakisha safari yake ya kuwa ‘mkazi’ wa kudumu wa Kinondoni (makaburini) kuwa ya kasi zaidi kwa mwendokasi wa G6, kama upo!

Siku zote yeye anajua kuwa pamoja na shida zake zote za kuwa yeye anapumua tu, nchi hii wengine wanaishi kiasi cha kutaka mishahara yao kulipwa kwa dola na namba za magari yao ziwe tofauti na za Watanzania wengine, ili pengine waweze kuruhusiwa kupita barabara maalumu  za mwendokasi za ili V8 zao ziweze kukwepa mikweche mingine, huku trafiki wakipiga saluti!

Sijasikia lolote linalomhusu mstaafu wa kima cha chini anayepokea na kutegemewa kuishi, kwa shilingi laki moja na elfu kumi tu kwa mwezi, rudia hapo, kwa mwezi!  Huyu huyu  anayetegemewa kuamka asubuhi moja ya mwezi Oktoba kumpigia kura mheshimiwa anayetaka kulipwa mshahara wake kwa dola badala ya kumpambania mpigakura wake Mzee Mstaafu apate matibabu ya bure!

Ndio, siku zote mstaafu wetu alikuwa akijua deni linalomhusu binafsi kama yeye lililkuwa lile la benki ya dotcom anayopitishia kipensheni chake uchwara, inayodai kuwa inawajali sana wastaatu na ikatoa mkopo wa kuwasaidia, huku ikiwabamiza kwa tozo zisizotofautisha wakopaji, awe mstaafu, awe mfanyabiashara, woote ni kubamizwa!

Ndiyo, Mstaafu wetu alikuwa akijua deni lake la shilingi milioni mbili na laki kadhaa, alilokopa kwenye benki hiyo ya dotcom alipoendekeza shida zake, ikiwemo maradhi yake ya kizee. Akajiingiza kichwa kichwa kukopa na sasa akitegemea kuwa linaisha mwaka 2026 mwezi fulani wa mwisho mwisho.  

Sasa anashituka sana kuambiwa kuna deni lingine linamhusu, tena sio tu yeye peke yake, bali na vitegemezi wake wa ‘nchi hii ya ‘Jamhuri ya Watu wa Familia yake’ – mwenza wake, watoto wake ambao pamoja na kumaliza mavyuo, wengine bado wanaisaka ajira kwa tochi, huku wakishauriwa kurudi Veta kwanza, ili kieleweke, na wajukuu zake. Eti wote sasa wanadaiwa shilingi milioni moja na laki sita kila mmoja, wakati watoto wangu hawa, sio wajukuu, hawajawahi kuona milioni moja zikoje!

Siri-kali imemtoa hofu Mstaafu na Watanzania wengine milioni 64, hofu isiyotoka kwamba mstaafu asiwe hofu kwa kuwa hakuna mtu atakuja kumgongea hodi na kuwataka kulipa  deni wanalodaiwa.  Hofu ya mstaafu haitoki Kwa vile anajua kwamba hakuna mtu atakayekuja kuwagongea hodi kudai chake ‘wamlipe asepe’, la hasha, hofu yake inatokana na tozo zitakazoundwa ili kulipa deni la Taifa la Shilingi trilioni…mama wee!…107 !

Mstaafu anajua kuwa akinunua unga, sukari, maharage, dagaa, sabuni na vinginevyo, kuna tozo inayotozwa ili kulipa deni la Taifa.

Hofu ya mstaafu ni kuwa isije ikatokea Mheshimiwa mmoja ‘akavumbua’ tozo hata kwenye kupumua hewa hii tuliyopewa bure na Mungu bila tozo yoyote!

Mstaafu wetu anajikuta akiliangalia deni hili Taifa na kuliona hamlimhusu kwa chochote kile. Litamhusuje huku akiona Siri-kali yake ikikopa ili kuwa na uwezo wa kuwanunulia ma VX waheshimiwa wake, huku waheshimiwa wa nchi zinazotukopesha wakienda ofisini na baisikeli au magari ya bei rahisi kama ‘Vakswageni’?

Deni linamhusu vipi wakati nchi inatoa Shilingi milioni tano au kumi kwa kila oli linalofungwa na timu zetui kubwa badala ya tmu ya taifa tu, huku yeye aliyeijenga nchi kwa jasho na damu yake akipokea pensheni ya shilingi Laki Moja na Elfu kumi Kwa miaka 21?

Ndio, linamhusuje yeye , wakati Siri-kali inafanya kile CAG alichosema miezi kadhaa nyuma kuwa kuna matumizi yasiyo na tija’ ya shilingi 347 bilioni ambayo mstaafu wetu anadhani kuwa ni pamoja na kununua magoli ya timu zetu kubwa kwa shilingi milioni tano, kupeleka wasanii wetu ndege nzima kwenda huko ‘duniani’ kusuuza macho na kuwasafirisha bure kuzindua treni la umeme.

Deni linamhusuje yeye wakati hakuna mkopo hata mmoja uliotumika kumwongezea pensheni yake ya shilingi Laki sio Pesa kwa mwezi inayokatwa kodi, huku mbunge wake anayemwakilishana, anayetakiwa kumpigia kura, analipwa Shilingi milioni…mama wee!… 14 kwa mwezi zisizokatwa, rudia, zisizokatwa kodi!

Mstaafu anajikuta akifarijika kwa namna fulani Siri-kali kutangaza kuwa wastani wa umri wa kuishi wa Watanzania ni miaka 67. Hajui afarijike au aogope kuhusu hili, maana kwa yeye kuwa na miaka 66 Siri- Kali inamfahamisha kuwa amebakisha mwaka mmoja tu kuwa ‘mkazi’ wa kudumu wa Kinondoni, hali itakayomuondolea maswahibu yote haya ya kulipa deni lisilomhusu. Lipeni wenyewe!

0754 340606 / 0784 340606

Related Posts