Mbadala wa madiwani hawa hapa mabaraza yakivunjwa

Dar es Salaam. Wakati mabaraza ya madiwani kote nchini yakivunjwa rasmi leo Juni 20, 2025, majukumu yao sasa yatatekelezwa na wakurugenzi wa halmashauri pamoja na wakuu wa idara katika halmashauri hadi pale watakapopatikana madiwani wengine.

Hata hivyo, watendaji hao hawataruhusiwa kuanzisha miradi mipya ya maendeleo, bali wataendelea kusimamia utekelezaji wa miradi iliyoachwa na madiwani katika halmashauri husika.

Tangazo la kuvunjwa kwa mabaraza hayo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais—Tamisemi, Mohamed Mchengerwa ambaye amesema tayari amekwisha saini notisi za kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani katika mamlaka za wilaya na miji.


Mchengerwa ameeleza kwamba masuala yote ya kiutendaji katika halmashauri kusimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiana na wakuu wa idara watakaokuwa kama wajumbe wa kamati.

Ameelekeza kuwa mkurugenzi wa halmashauri hataruhusiwa kuanzisha miradi au uwekezaji mpya ikiwa ni pamoja na kubadilisha au kurekebisha mradi, uwekezaji au uamuzi wowote uliopitishwa na halmashauri kabla ya kuvunjwa.

Amesisitiza kwamba matumizi mabaya ya mamlaka au kutotekeleza kwa ufanisi majukumu ya kiutawala kwa mujibu wa notisi hizi, kutamfanya mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa sheria.

Wakati mabaraza hayo yakivunjwa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajiwa kuvunjwa Juni 27, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan wakati Baraza la Wawakilishi likitarajiwa kuvunjwa Jumatatu Juni 22, 2025.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jomary Satura ili kufahamu uzoefu wake na namna watakavyofanya kazi katika kipindi cha miezi minne ambayo mabaraza ya madiwani hayatakuwepo.

Satura amesema katika kipindi ambacho madiwani hawapo, nafasi hizo zinakaimiwa na menejimenti ya halmashauri.

Katika kukaimu huko, Satura amesema katika halmashauri za miji, mkurugenzi ndiye anakuwa meya huku zile halmashauri za wilaya, mkurugenzi anakuwa mwenyekiti wa halmashauri.

“Hata wakati Waziri wa Tamisemi anatangaza kuvunjwa kwa mabaraza hayo alilisema hili, huku akionya wakurugenzi kutotumia nafasi hizo za ukaimu vibaya katika kutekeleza majukumu yao,” amesema.

Hata hivyo, kwa upande wa madiwani, amesema wakuu wa vitengo ndio wanakuwa kama madiwani, nafasi ambazo watazikaimu mpaka pale baraza jipya litakapopatikana baada ya uchaguzi.


Aidha, amesema baada ya baraza hilo kupatikana, mkurugezi atapaswa kutoa taarifa za mambo yote aliyotekeleza wakati baraza lilipokuwa halipo ikiwemo miradi ya maendeleo.

Pamoja na hayo, Satura amesema mkurugenzi hataruhusiwa kuanzisha miradi mipya katika kipindi chote hicho na kama angetaka hivyo alipaswa kuwasilisha katika vikao vya mwisho vya baraza ili kuridhiwa.

“Kama kuna mradi mkurugenzi ulikuwa unaona ni muhimu kufanyika ndani ya kipindi hiki, ulipaswa uwasilishe hoja hiyo mapema kwenye baraza kabla ya kuvunjwa ili baraza lijadili na kuridhia, lakini kama hukufanya hivyo, ukijiamulia mwenyewe, huo ni uvunjifu wa sheria,” amesema.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo amewashukuru madiwani wa halmashauri ya Temeke kwa namna walivyompa ushirikiano katika kipindi chake cha uongozi.

Satura ambaye ametimiza mwaka mmoja na miezi minane tangu ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo, akitokea halmashauri ya Ilala, amesema madiwani hao wamekuwa wakiwapa nafasi watumishi kutekeleza majukumu yao kulingana na utaalamu waliokuwa nao, jambo ambalo ni gumu kulipata katika maeneo mengine.

“Naweza kusema Halmashauri ya Temeke ni ‘Stress Free’ (hakuna msongo wa mawazo), madiwani wanakuacha unafanya kazi kulingana na utaalamu wako, deni linabaki kwako kuwapa matokeo yanayoonekana.


“Hii ikiwa ni tofauti na kwenye halmashauri nyingine ambapo hadi watumishi wanaogopa kufanya kazi zao kiweledi kutokana na madiwani kuwafuatafuata nyuma, kwa kweli Temeke nawapongeza sana madiwani,” amesema Satura.

Katika hilo, amesema hata alipowapelekea baraza hilo mapendekezo ya kuigawa Temeke katika kanda, walipokea wazo hilo kwa mikono miwili na matokeo ya uamuzi huo umeifanya Temeke hadi kufika Aprili mwaka huu, kukamilisha malengo ya ukusanyaji mapato wa Sh53 bilioni waliokuwa wamejiwekea katika mwaka 2025 ambapo miezi iliyobaki watakuwa wanakusanya fedha za ziada.

Kwa kufanya hivyo, amesema itawafanya kuwa na uhakika na utekelezaji wa miradi waliyojiwekea, jambo ambalo pia madiwani lazima wawapende kwa kuwa wana uhakika wananchi wao wanaenda kuondolewa kero zilizokuwa zinawasibu.

Akizungumzia uzoefu wake katika kazi, diwani wa Kivule, Nyansika Getama amesema alishawahi kuwa diwani huko nyuma, lakini ilivyofika mwaka 2015 hakuchaguliwa, lakini uchaguzi uliofuata mwaka 2020 alifanikiwa kurejea tena.

“Katika kipindi ambacho nilikuwa nje, miradi mingi niliyoiacha ilisimama, vilevile na nilipochaguliwa nikaiendeleza niliposhia,” amesema Getama.

Kati ya miradi hiyo, amesema ipo inayohusu afya, elimu na barabara, yote ikigharimu jumla ya Sh10.4 bilioni.

Kwa upande wa elimu, amesema anaweza kujenga Shule ya Mshikamano ambayo imewasaidia kuwapunguzia kutembea kilometa tisa wanafunzi waliokuwa wakisoma shule ya Kivule.

“Baada ya kukamilika kwa shule hiyo, niliwahamisha wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza hadi la tano kutoka Shule ya Msingi Kivule.

“Ukiacha madarasa, lakini pia nimejenga ofisi za walimu na shule ya chekechea na sasa watoto wanasoma katika mazingira yaliyo bora na karibu na wanapoishi,” amesema.

Kwa upande wa afya, amesema ameweza kusimamia vilivyo ujenzi wa hospitali ya Kivule, ambapo sasa badala ya wananchi kufuata huduma zinazomhitaji daktari bingwa wa Amana au Muhimbili wanazipata hapo.

Hata hivyo, kwa upande wa barabara licha ya kupata mradi wa DMDP, amesema bado kuna changamoto kubwa ya ubovu wa barabara na ni suala linalomnyima usingizi.

“Hata hivyo, nashukuru mkandarasi tayari yupo site, alichokuwa anasubiri ni kumalizika kwa mvua zilizokuwa zinanyesha lakini muda si mrefu Kivule mitaa yaje yote itaunganishwa na barabara,” amesema Getama.

Diwani wa Zingiziwa, Maige Maganga amesema moja ya mafanikio anayojivunia katika uongozi wake ni kujengwa kwa kituo cha afya cha kata kutoka zahanati iliyokuwa imechakaa hadi kukaribia kuanguka, ambapo zamani wananchi wa kata hiyo walilazimika kwenda Chanika kupata huduma za kibingwa.

Kutokana na hilo walijikuta wakiingia gharama za usafiri lakini sasa hivi wanapata huduma hizo kwa ukaribu.

Pia, amesema kata hiyo mitaa mingi ilikuwa haina umeme, lakini kwa kupitia mradi wa Rea, sasa karibu mitaa yote inapata nishati hiyo na hivyo kuchangia kukua kwa shughuli za kiuchumi na kubadilisha maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

“Ukiacha umeme na hospitali, lakini tunaweza kujenga soko kubwa ambalo awali lilikuwa ni vibanda tu lakini sasa hivi limewekwa mashedi, yaliyogharimu Sh300 milioni na kufanya hata magari kutoka mikoani kuja kushusha mazao hapo,” amesema.

Amesema wameweza kuibadilisha Shule ya Gogo kuwa ya mchepuo wa Kiingereza, awali wananchi walilazimika kuwapeleka watoto wao shule za Olimpio au Diamond zilizopo Upanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kufanikiwa kutengenezwa kwa barabara kutoka Chanika hadi kwa Makamu wa Rais, Maige amesema bado barabara ni changamoto kubwa lakini anaamini siku za usoni changamoto hizo zitapungua kama sio kwisha kwa kuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.


Diwani wa Buyuni, Athuman Ally amesema pamoja na mafanikio mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya na kuongeza madarasa kwenye shule, bado kata za pembezoni zinakabiliwa na ubovu wa barabara, jambo linalowafanya wananchi kushindwa kuzifikia kirahisi huduma hizo za kijamii.

Ally amesema kwa kuwa wabunge ndio watunga sheria, ameshauri wanapokaa katika vikao vyao kuliangalia suala la barabara kwa jicho la karibu kwani mbali ya kuwarahisishia wananchi kutoka eneo moja kwenda jingine, lakini ndilo linachochea kukua kwa uchumi.

Related Posts