Dar es Salaam. Wizi wa nyaya za shaba zilizo ndani ya transfoma zimelisababishia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hasara ya Sh700.5 milioni katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2024 kufuatia kuharibiwa kwa transfoma 63.
Kati ya transfoma hizo 63 zilizoharibiwa, Wilaya ya Mkuranga inaoongoza kwa kurekodi matukio 36 ya uharibifu huo ikifuatiwa na mikoa ya Morogoro yenye matukio 12, Kilimanjaro 9, Iringa 2, Singida 2 na wilaya ya Kinondoni yenye matukio mawili ya uharibifu wa transfoma.
Katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu matukio matatu ya wizi na uharibifu wa aina hiyo yameripotiwa tena kutokea Mkuranga yakisababisha hasara ya Sh62 milioni na tayari wahusika wamekamatwa.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 20,2025 Ofisa Usalama Mwandamizi wa Tanesco, Richard Damas amesema uharibifu huo unafanywa na watu wanaovamia transfoma kwa lengo la kuiba nyaya za shaba zilizomo ndani ya miundombinu hiyo.
Damas amesema hasara hiyo inajumuisha gharama za kurejesha transfoma mpya na kukosekana kwa mauzo ya umeme katika maeneo husika ambayo umefanyika wizi huo.

Mojawapo ya transfoma wilayani Mkuranga ikiwa imeangushwa na kutolewa nyaya za shaba.
Amesema, “Transfoma ikiharibika inachukua kati ya siku tatu hadi saba ili kupata kupata nyingine na kurejesha huduma, hii ni kwa sababu nyingi zinaazigwa kutoka nje ya nchi. Hivyo katika kipindi hicho cha kusubiri eneo husika linakosa huduma na Tanesco haiuzi umeme kwa wateja hivyo kuna hasara inatengenezwa.
Mbali na hasara hiyo ya fedha, wizi huo unaweka hatarini maisha ya watu akitolea mfano wa matukio mawili moja likiwa la Morogoro na lingine la Mkuranga ambapo watu wawili walipoteza maisha wakitekeleza uhalifu huo.
Damas ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa matukio hayo hutokea kwenye transfoma zilizo maeneo ya pembezoni ambapo hakuna mwingiliano mkubwa wa watu hasa maeneo yenye viwanda.
Vijiji vya Mwarusembe, Kimanzichana na Kisiju vilivyo katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani vinatajwa kuongoza kwa matukio ya transfoma kuvamiwa na kutolewa shaba.
Operesheni iliyofanywa na shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ilifanikisha kukamatwa watu nane wakihusishwa na uhalifu huo na kesi zao bado zinaendelea mahakamani.
Kwa mujibu wa ofisa usalama huyo ili kupata nyaya hizo ni lazima transfoma iharibiwe na kazi hiyo hufanywa na watu ambao angalau wana utaalamu wa umeme hata hivyo kuna uwezekano wa transfoma kulipuka na kusababisha madhara.
“Wizi huu haufanywi na mtu mmoja, kuangusha transfoma ni kazi ya mtu zaidi ya mmoja na kati yao lazima awepo anayeufahamu umeme, kwa sababu kinachofanyika ni lazima fyuzi inayoleta umeme ifyatuliwe.
“Ukifyatua fyuzi ndiyo unakuwa umeutoa umeme kwenye transfoma hapo sasa ndipo wanapofungua na kutoa utumbo wa ndani ambao ndiyo una hizo nyaya za shaba. Baada ya kuondoa umeme wanasukuma ili kuidondosha transfoma kisha kufanya uhalifu huo,” amesema.
Damas anakiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa uhalifu huo kufanywa na watu wanaofahamu fika umeme ndiyo sababu hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ndani ya shirika hilo.
“Inawezekana baadhi yetu wakawa wanashiriki kwenye michezo hii michafu hili linashughulikiwa ndani lakini pia kuna miradi mingi ya umeme inaendelea ambayo inahusisha wakandarasi, hawa wanaajiri vijana wanaofahamu umeme.
“Kuna uwezekano hawa vijana pia wakawa wanahusika kwa sababu, matukio mengine yanatokea kwenye transfoma ambazo hazijaingiziwa umeme bado sasa utajiuliza mtu wa kawaida anawezaje kujua kama pale hakuna umeme hili pia tunalifanyia kazi kuhakikisha miundombinu yetu inabaki salama,”amesema.
Katika kukabiliana na hilo Damas amewataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapoonekana watu wanaojifanya kuwa mafundi bila kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji au mtaa husika.
“Tumetoa maelekezo kwa viongozi wa vijiji na mitaa, matengenezo yoyote yanayohusu transfoma ni lazima hao mafundi waripoti ofisi ya kijiji kabla ya kuanza kazi, ikitokea kinyume na hivyo watoe taarifa Tanesco,”amesema.
Baadhi ya wachumi waliozungumza na Mwananchi wamesema wizi huo ni janga la kiuchumi linalohitaji kuchukuliwa kwa uzito mkubwa kuepusha hasara na kutishia kasi ya uwekezaji hasa katika maeneo ya viwanda vilivyopo pembezoni ambayo transfoma zake zinawindwa zaidi.
Mtalaamu wa uchumi, Dk Gibson Kihalala amesema Serikali, wananchi na sekta binafsi wanapaswa kushirikiana kwa dhati katika kuzuia vitendo hivi kwa kuweka mikakati ya ulinzi wa miundombinu ya umeme, kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara yake, na kuanzisha sheria kali dhidi ya wahalifu.
“Taifa haliwezi kufikia maendeleo ya kweli ikiwa miundombinu muhimu kama ya nishati itaendelea kuvamiwa na kuharibiwa. Vitendo vya aina hii vinaligharimu taifa mamilioni ya fedha kila mwaka kwa ajili ya ukarabati na urekebishaji wa transfoma zilizoharibiwa.
“Fedha hizi ambazo zingeweza kutumika katika kuboresha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu, hulazimika kuelekezwa katika kugharamia uharibifu uliosababishwa na wachache. Kwa maana hiyo, maendeleo ya kijamii huzorota na kupunguza ubora wa maisha kwa wananchi walio wengi.
Mchumi mwingine, Rogatus Moshi amesema uharibifu huo usipokomeshwa huenda ukaathiti uwekezaji kwa kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika ni jambo linalopewa kipaumbele kabla ya uwekezaji kufanyika.

“Wawekezaji huangalia mambo kama upatikanaji wa nishati ya uhakika kabla ya kuwekeza mitaji yao katika nchi fulani. Sasa inapotokea uharibu wa aina hii unaosababisha nishati ya umeme kukosekana huwatisha wawekezaji, na hivyo kupunguza kasi ya uwekezaji mpya na kukuza hali ya ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana. Matokeo yake ni kudorora kwa uchumi na kuongezeka kwa umasikini.