MSD yataja hatua za mageuzi katika uzalishaji wa ndani

Arusha. Bohari ya Dawa (MSD) imesema uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya nchi unahitaji kuimarishwa ili viwanda vizalishe zaidi kukidhi mahitaji ya nchi na kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Imesema utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za afya, unatokana na uwezo hafifu wa viwanda vya ndani, uwekezaji katika sekta ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa hizo, hali inayosababisha zaidi ya asilimia 80 huagizwa kutoka nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati wa kongamano la kitaifa la tiba na maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) linalofanyika jijini Arusha.

Tukai amesema ili kupambana na changamoto hiyo, MSD imeanza michakato mbalimbali ya kuhakikisha dawa muhimu zinazalishwa ndani ya nchi kupitia viwanda vilivyopo, kwa kuvielekeza bidhaa zipi viongeze kulingana na uwezo wa uzalishaji na hivyo wamekuwa wakifanikiwa kupunguza utegemezi wa nje.


Tukai amesema nchi za Jangwa la Sahara zina uhitaji mkubwa wa bidhaa za afya, lakini ili kufikia matarajio walifanya tafiti kadhaa.

“Ili kufikia uzalishaji wa ndani, tuliangalia maeneo manne au matano, tuligundua kwa Tanzania pekee yake tunatumia bidhaa za afya za thamani ya Dola za Marekani 1 bilioni (Sh23.6 bilioni) ambazo karibu hizi zote zinaagizwa kutoka nje.

“Lakini tukaangalia kulinganisha nchi mbili, zingine kama Kenya na Uganda tulitafuta takwimu za kuanzia mwaka 2015 ambazo zilionyesha kwa Tanzania tulikuwa tunazalisha bidhaa za afya za Dola 970,000 (Sh2.5 bilioni) lakini tulikuwa tunaingiza bidhaa za afya za Dola 403 (Sh1.06 bilioni),” amesema.

Tukai amesema walipofanya mlinganisho na majirani kwa nchi za Kenya na Uganda waligundua wakati Tanzania inazalisha bidhaa za afya za Dola 970,000 (Sh2.5 bilioni ) Kenya walikuwa wanazalisha zenye thamani ya dola milioni 71 (Sh186 bilioni) na wanaingiza zenye thamani ya Dola 572 milioni (Sh1.5 trilioni).

Amesema walipoangalia Uganda ambao walidhani ni wadogo kwao walikuwa tayari wanazalisha bidhaa za Dola milioni 12 wakabaini wako mbele ya Tanzania mara 10 zaidi wakilinganisha na takwimu ambazo waliziangalia ndipo wakaanza mikakati ya nini kifanyike.

Amefafanua kuwa waliamua kuanza uhamasishaji kwa viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa za afya zenye ubora ili kukidhi vigezo vya MSD na kuhamasisha wawekezaji zaidi ili kupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo kuagiza bidhaa na kusubiri kwa muda mrefu.

“Tukaona tunaweza kunyanyuka na kufanya jambo, wakati tunaangalia hilo pia tukaangalia soko letu la ndani katika maeneo makubwa, la kwanza sera zetu za ndani ambapo tayari kwa wazalishaji wa ndani zipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Na katika ubunifu tuliangalia kugundua baadhi ya bidhaa ambazo ni muhimu sana kuzalishwa na hazipatikani kirahisi, tukagundua kama dawa za kawaida zikiwemo za vidonge mzalishaji anaweza kubadilisha na kuzalisha, kwa kuwa mashine zipo pale, hivyo tukagundua tatizo si mashine bali kipaumbele kile ambacho sisi tunakiweka,” amesema.

Pia amesema waliangalia nini kinaweza kuhitajika na labda kikatoka nje, wakagundua eneo ambalo linayumba kidogo ni kwenye kuiga, hivyo katika kujipanga namna gani watatumia vifaa walivyonavyo kuzalisha zaidi.

Tukai amesema wakagundua kwa sasa asilimia 80 ya bidhaa wanaagiza nje, lakini ndani ya muda mfupi wanaweza kuzalisha asilimia 50 ya mahitaji ya nchi, kwa kufanya uwekezaji na kuanza uzalishaji wa bidhaa muhimu ambayo haitahitaji fedha nyingi sana iwapo zingeagizwa.

“Tukianzisha uzalishaji huu ndani ya nchi kwa kuboresha viwanda vyetu na kuanzisha uzalishaji wa bidhaa mpya, inaweza kutuingizia hadi Dola bilioni 200 kwa haraka,” amesema.

Amesema katika kushauriana zaidi waliona ni muhimu kuanza na bidhaa zinazohitajika zaidi, akitaja mifano vitendanishi vinavyotumika kwa ajili ya dialysis, dawa zinazonunuliwa katika mitungi au vitendanishi vingine vya maabara ambavyo huilazimu MSD kusafirisha makontena mengi kutoka nje.

Hata hivyo amesema ambayo nayo ukiangalia wanalipia fedha nyingi si kwa kununua, bali gharama kubwa inakuwa kwenye kusafirisha hivyo waliangalia nini wafanye kuondokana na hiyo gharama.

“Tukaangalia tukaona ili tufike hiyo asilimia 80 hatuhitaji kuwekeza fedha nyingi tukagundua kwamba katika zile bidhaa 20 zinatufanya tutumie gharama kubwa ambazo ukiangalia tunaweza kuzizalisha ndani,” amesema.

Amesema eneo jingine waliangalia vitendanishi vya kuchukulia sampuli za mkojo na zinginezo za maabara ziliOzalishwa nje, na mpaka kufikia mwaka jana mwanzoni hawaagizi tena nje, walitoa maelekezo kwa wazalishaji na sasa wananunua ndani.

“Serikali pia tuna viwanda vipo vya gloves, Kejo Pharmaceutical na kile cha Arusha hivyo tunaendelea kuangalia nini tufanye ili kuzalisha zaidi ndani.”

Pamoja na hayo amesema wanawahamasisha wazalishaji wa ndani wazalishe bidhaa za afya hasa dawa zinazohitajika zaidi nchini kulingana na changamoto za magonjwa yaliyopo na matumizi ya nchi.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa bado changamoto ipo kwenye uwekezaji: “Tuna mashamba makubwa ya mpira ekari mpaka 40,000 Tanga, Pwani, Pemba na Morogoro lakini kinachosababisha bado tunaagiza nje ni kwa sababu ya uwekezaji hafifu.”

Awali, akizungumzia hali halisi ya huduma za afya nchini na uelekeo kufikia mwaka 2030, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema ufikiwaji wa huduma za afya nchini, asilimia 75 ya idadi ya watu wanaweza kufikia huduma ndani ya kilomita tano.

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea 
akizungumzia hali halisi ya huduma za afya nchini na uelekeo kufikia mwaka 2030, kwenye  Kongamano la Kitaifa la Tiba



Amesema mafanikio hayo yamesaidia kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga.

Related Posts