Mwanza. Licha ya kuwa mkoa wa pili kwa kuchangia pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 7.2, nyuma ya Dar es Salaam inayoongoza kwa asilimia 14, Serikali imeweka mkakati mahsusi wa kuufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kinara wa uchumi nchini.
Hili litawezekana kupitia mipango madhubuti ya maendeleo ya viwanda, biashara, uvuvi, usafirishaji na miundombinu, hasa kwa Mwanza inaelekezwa kuwa kitovu kipya cha ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.
Mkoa wa tatu ni Arusha unaochangia kwa asilimia 4.7, Mbeya asilimia 5.7 na Tanga asilimia 4.7 kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu msingi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mwaka 2023.
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, mchango wa Mwanza katika pato la Taifa umeongezeka kwa kasi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ukichangiwa zaidi na sekta za uvuvi wa Ziwa Victoria, biashara ya kati ya mikoa na nchi jirani, pamoja na ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati na shughuli za usafirishaji kupitia bandari ya Mwanza, reli, pamoja na barabara kuu zinazoiunganisha na mikoa mingine na nchi za Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda anasema kiu iliyopo ni kuufanya mkoa huo kuwa kinara kiuchumi zaidi ya Dar es Salaam, jambo analosema liko mbioni kutimia kutokana na miradi mbalimbali ya miundombinu inayotekelezwa.
Mkoani Mwanza ndiko lilipo Daraja la JP Magufuli lililoanza kutumika jana Juni 19, 2025, lenye urefu wa kilomita 3.2, likiwa la kwanza kwa urefu Afrika Mashariki na Kati na la sita kwa Afrika.
Mtanda aliyezungumza na Mwananchi ofisini kwake, anasema pamoja na daraja hilo, mageuzi ya miundombinu yanayoshuhudiwa mkoani humo, yanaongeza matumaini ya kufikiwa lengo la kuwa mkoa shindani kiuchumi dhidi ya Dar es Salaam ndani ya miaka 10 ijayo.
Ukiacha miradi inayotekelezwa, anasema mkoa huo upo katika eneo la kimkakati na una rasilimali nyingi, likiwamo Ziwa Victoria linalochukua asilimia 53 ya ardhi ya Mwanza.
Kutoka asilimia 7.2 zinazochangiwa na Mwanza katika GDP, Mtanda anasema mwaka 2035 mchango wa mkoa huo utazidi asilimia 10.
“Lengo letu ni kuvuka asilimia 10 ya mchango katika pato la Taifa,” anasema Mtanda na kuongeza:
“Tuna ardhi ya kutosha, ziwa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali na mipango madhubuti ya miundombinu. Hatulengi tu kuifikia Dar, bali tuna nia ya kuipita.”
Daraja la JP Magufuli lenye thamani ya Sh718 bilioni ambalo ni refu zaidi Tanzania, limeanza kutumika rasmi hivyo kuondoa utegemezi wa vivuko na kupunguza muda wa safari kati ya maeneo muhimu.

Mradi mwingine mkubwa kwa mujibu wa Mtanda ni upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa gharama ya Sh28 bilioni, ambao utaufanya uwanja huo kuwa wa kimataifa, wenye uwezo wa kuhudumia abiria 4,000 kwa wakati mmoja, kutoka chini ya 100 wa sasa.
“Ndege zitakuwa zinaingia moja kwa moja kutoka nje ya nchi kuchukua nyama na samaki waliochakatwa kwa ajili ya kuuza nje,” anasema.
Mwingine ni mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka, ambao umefikia asilimia 60 ya utekelezaji ambao unaendelea, ili kuunganisha na Tabora – Dodona – Dar es Salaam.
Anasema reli hiyo itaunganisha Mwanza na ukanda wa Kati na na Pwani pamoja na nchi jirani za Rwanda na Burundi na kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo na abiria.
Mradi huu pia unalenga kuunganisha barabara, bandari na viwanja vya ndege kwa pamoja, kupitia mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kaskazini (Northern Port), wenye thamani ya Sh18 bilioni.
“Tunajenga mfumo wa mawasiliano wa kisasa. SGR, bandari, viwanja vya ndege hii ni nguvu ya pamoja inayobadili sura ya Mwanza kuwa lango kuu la biashara Afrika Mashariki,” amesema.
Wafanyabiashara wadogo tayari wanaanza kuona nuru. Soko la kisasa linalojengwa jijini Mwanza kwa gharama ya Sh123 bilioni, linatarajiwa kufanya kazi saa 24 kwa siku.
“Hili litakuwa Kariakoo yetu,” amesema Rehema Salum, mfanyabiashara kutoka Geita.
Anasema kwa sasa watakuwa na sehemu salama na yenye shughuli nyingi ya kuuza bidhaa na wateja kutoka mikoa mingine na nje ya nchi watafika kwa urahisi.
Mmiliki wa kiwanda cha kuchakata samaki, Emmanuel Kileo amesema miradi inayotekelezwa mkoani humo ikiwamo ya SGR na upanuzi wa uwanja wa ndege itachochea mabadiliko ya jiji hilo.


“Uwanja wa ndege ukikamilika tutaweza kusafirisha samaki kwenda kwenye soko la Ulaya moja kwa moja kutoka Mwanza badala ya kupitia Dar es Salaam. Hii itapunguza gharama na muda kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Kileo, Mwanza tayari inasafirisha nyama na samaki waliochakatwa, huku wawekezaji wa uvuvi wa vizimba wakiwa na matumaini makubwa.
Serikali imewekeza Sh4.1 bilioni katika mikopo isiyo na riba kwa ajili ya uvuvi wa kisasa wa vizimba.
Kuhusu hilo, Mtanda anasema Serikali inafanya operesheni ya kuondoa magugu maji kwa kutumia Sh600 milioni na kununua mtambo maalumu wa kukata magugu hayo kwa Sh1.5 bilioni.
Kitovu cha biashara kikanda
Kwa wafanyabiashara kutoka Afrika Mashariki, Mwanza inazidi kujipambanua kama kitovu cha biashara na usafirishaji wa kikanda kama anavyoeleza Peter Hidar, mfanyabiashara ya nyama kutoka Kenya.
“Upanuzi wa uwanja wa ndege utasaidia kupeleka bidhaa zinazoharibika haraka. Mwanza inakuwa kituo muhimu sana kwetu,” anasema.
Naye James Wafula, mfanyabiashara kutoka Uganda aliyekuwa mkoani Mwanza kushuhudia uzinduzi wa Daraja la JP Magufuli, anasema:
“Mwanza ipo sehemu nzuri kijiografia. Kupitia SGR na usafiri wa meli katika Ziwa Victoria, tunaweza kusafirisha bidhaa kwa haraka na uhakika.”
Uzinduzi wa meli mpya ya Mv Mpungu yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 ambayo inaunganisha Mwanza, Bukoba hadi Uganda, ni hatua nyingine kubwa itakayoongeza ushindani wa Mwanza kiuchumi, huku meli nyingine kubwa ya Mv Mwanza itakayosafirisha abiria na mizigo baina ya nchi tatu – Tanzania, Kenya na Uganda, ikiwa mbioni kukamilika.
Sambamba na maendeleo ya miundombinu, huduma za kijamii pia zinaboreshwa. Kwa mujibu wa Mtanda, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa maji wa Butimba wenye thamani ya Sh71 bilioni.
Anasema mradi huo utazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku na kunufaisha zaidi ya wakazi 400,000.
“Jiji lenye zaidi ya watu milioni tatu haliwezi kuendelea huku likikumbwa na uhaba wa maji. Mradi huu ni uhai kwa wakazi wetu,” anasema.

Katika hatua nyingine, anasema mradi wa umeme wa jua kwa vijiji 23 vya visiwani umeshaanza ukiwa na thamani ya Sh4.7 bilioni, ukitarajiwa kutoa nishati ndani ya mwezi mmoja na kuchochea uchumi wa maeneo hayo.
Mtanda anasema makadirio ya idadi ya watu yanaonyesha Mwanza itakuwa na wakazi milioni tano ndani ya miaka 10 ijayo, idadi inayokaribia ile ya sasa ya Dar es Salaam.
“Jiji limeanza mipango ya kupanua barabara zake kuwa njia nne, ikiwamo barabara ya Mwanza–Usagara ili kupunguza msongamano na kuunganisha vijiji na masoko makuu,” anaeleza.
Kwa mtazamo wa kiuchumi, mtaalamu wa uchumi, Dk Abella Ngassa anasema ingawa Dar es Salaam imepigwa hatua, Mwanza ina kila sababu ya kuizidi.
“Dar imeweka viwango, lakini Mwanza ina kila sababu ya kuvuka hapo. Ni mkoa pekee ulio na uunganisho wa anga, reli, maji na barabara kwa pamoja,” anasema.