Mwanza. Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amesema vijana wengi wa Kitanzania wanakosa juhudi za kutafuta ukweli na kuchambua taarifa sahihi, badala yake wamekuwa wakitegemea taarifa zisizo sahihi kutoka vyanzo visivyoaminika.
Profesa Kilangi ametoa kauli hiyo leo Juni 20, 2025, wakati akihudhuria maadhimisho ya kumbukumbu ya maisha ya Mtakatifu Agustino, yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Tanzania (SAUT) jijini Mwanza.
Profesa Kilangi, mtafiti na mshauri mwenye uzoefu ndani na nje ya nchi, amesema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya kutosoma vitabu na machapisho, na hivyo wanapaswa kuiga nyayo za Mtakatifu Augustine katika kutafuta ukweli ili kuleta maendeleo katika jamii.
“Hiyo ndiyo changamoto ambayo mimi naiona kwa kizazi cha sasa, kwamba kuna uvivu mkubwa sana wa kutafuta taarifa, kusoma vitabu, maandiko na machapisho, nadhani kama tukiweza kulifanyia kazi hilo tutakuwa tumepiga hatua sana na hicho ndicho kitu ambacho nadhani tunaweza kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Augustine,” amesema Profesa Kilangi aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania Brazil.
Profesa Kilangi amesema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, wananchi hawatakiwi kufuata mkumbo wa maneno wanayoambiwa na wanasiasa majukwaani bali wanapaswa kuyachuja na kujiridhisha.
“Sasa katika uchaguzi ni jambo lilelile, kwamba watu wetu watafute taarifa wajiridhishe juu ya taarifa ziwe ni hasi au chanya, wazitafute wajiridhishe wasiambiwe tu jambo kwenye majukwaa na mwanasiasa nao wakakubali na kufuata na kushangilia,” amesema.

Naye, mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo cha Mtakatifu Augustine Tanzania tawi la Mwanza, Kasimir Kasimir amewaomba vijana kuhudhuria na kushiriki kwenye matamasha ya kisiasa ili kujenga wigo mpana wa elimu ya maisha.
“Vijana tumekuwa hatushiriki kwenye majukwaa ya wanasiasa ambapo kampeni hizo ndiyo zinatupa dira ya kumchagua mgombea sahihi, pili hatusikilizi sera wala kushiriki katika uchaguzi kwa hiyo nitoe wito awamu hii tushiriki kikamilifu,” amesema Kasmiri ambaye ni rais mstaafu wa Serikali ya Wanafunzi Chuo cha Mtakatifu Agustino Tanzania (Sautso).
Beatrice Thomas, mwanafunzi wa chuo hicho, amesema vijana wengi wamekuwa wategemezi wa kuamuliwa na wengine, badala ya kujisimamia, jambo linalowafanya kuzama katika mitego ya wanasiasa.
Ameendelea kuwaomba vijana wajitambue na kufanya maamuzi sahihi.
“Sisi kama vijana tunaitumia siku hii kumuenzi Mtakatifu Augustine katika kuimarisha upendo na kupeana hamasa ya elimu, hasa tunapoelekea katika uchaguzi. Rai yangu vijana tujitambue tusije tukatumiwa katika siasa bila kujali jambo hilo litaleta madhara gani kwetu,” amesema Beatrice.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Padri George Nzungu amesema Mtakatifu Augustine aliamini katika maarifa na watu wenye bidii ya kazi ambayo itawahamasisha vijana kutafuta maarifa.
“Binadamu anapaswa kulelewa kimaadili, kielimu, kiutu na kiroho hayo yakizingatiwa katika jamii, tunaamini mji wa Mungu unaweza kutengenezwa kwa falsafa ya jamii ya Mungu ambapo watu wataishi kwa upendo haki na kuheshimiana,” amesema. Nzungu.