Arusha. Serikali imeamua kuwaachia madiwani wote nchini vishkwambi walivyogaiwa kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji wa vikao vya mabaraza, licha ya kuwa vilitakiwa kurudishwa wakati wa kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani baada ya kumalizika kwa muda wao wa uwakilishi.
Baadhi ya vishkwambi hivyo vilivyotolewa mwaka jana na vingine Januari mwaka huu kwa mabaraza yote nchini vilitakiwa kurudishwa leo Juni 20, 2025, wakati wa kuvunjwa rasmi kwa mabaraza ya madiwani.
Akizungumza kupitia simu ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda wakati wa kuvunja Baraza la Jiji la Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameagiza madiwani hao waachiwe vishkwambi hivyo.
Mchengerwa amesema lengo la kufanya hivyo ni kutukuza mema na makubwa waliyotenda madiwani hao, kipindi cha uongozi wao kwa kufanikisha mambo makubwa yaliyopo nchini.
“Mmefanya kazi kubwa na yenye mafanikio, na najua mlipewa vifaa vya kazi ambavyo si mali ya halmashauri, ikiwemo vishkwambi vya kurahisisha shughuli za mabaraza.
“Sasa naagiza vishkwambi hivyo viendelee kubaki mikononi mwenu kote nchini, kwani mmevizoea na mmehifadhi siri zenu, barua zenu pamoja na mawasiliano ya watu wa karibu.
“Napenda kutumia jukwaa hili kumwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi ashirikiane na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, ambao tayari wamevunja au watavunja mabaraza, kuhakikisha madiwani wanaruhusiwa kubaki na vishkwambi hivyo,” amesema.

Awali, Makonda alipovunja baraza hilo, aliwataka madiwani wa Jiji la Arusha na mkoa mzima kuendelea kuhifadhi hadhi na heshima ya amani, utulivu na chama kilichowapitisha madarakani.
“Tusikubali kwenye kata zetu kutokea vurugu za aina yoyote, katumieni uzoefu wenu kuhakikisha nchi inabaki na amani na utulivu na chama kinabaki imara kwa ajili ya watoto wetu na watoto wa watoto wetu,” amesema.
Pia, amewataka kukubaliana na matokeo yatakayopitishwa na chama katika kura za maoni baada ya kuchukua fomu za kuwania nafasi zao tena.
“Kumbuka wakati unapata hiyo nafasi kuna mtu alikuwepo akakupisha na wewe kama imejitokeza kugombea na jina lako limerudi au halijapitishwa kubali matokeo, tusifanye mambo ya kuumiza chama au kuvuruga amani kwenye maeneo yetu,” amesema.
Katika baraza hilo amewataka wakurugenzi wote wa halmashauri saba za Mkoa wa Arusha kuwalipa madiwani mafao yao kwa wakati.
“Wakurugenzi hakikisheni baraza linapovunjwa tu madiwani wote walipwe mafao yao kwa wakati kama ilivyo kwa wabunge, kwani si hisani ni haki yao na kama kuna shida lipelekwe kwa katibu tawala mkoa na likishindikana liletwe kwangu, lakini si kuwazungusha waheshimiwa hawa,” amesema Makonda.
Mbali na hilo ameagiza wenyeviti wa mitaa, kijiji na vitongoji kuanzia sasa malipo ya mishahara yao yaingizwe kwenye akaunti zao, tofauti na sasa zinavyoingizwa kwenye akaunti za kata.
“Lengo ni kuwaondolea usumbufu wa kumchekea mtendaji ili amlipe fedha zake, lakini pia hii itaongeza uwajibikaji na kupunguza usumbufu.
“Pia, kuanzia sasa nataka wenyeviti wapewe nakala ya taarifa za bajeti yote iliyosomwa bungeni, ili wajue miradi gani inatekelezwa kwenye maeneo yao na washirikishwe kwenye kila hatua inayotekelezwa wakati ukifika,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka madiwani hao kuendelea kuishi kwenye jamii kwa maadili na nidhamu kubwa ya utumishi wa umma ili kuleta mfano mzuri kwa watu wanaowazunguka.
“Kuvunjwa kwa baraza haimaanishi wewe sio sehemu ya jamii yenye jukumu la kutunza amani, usalama, na utulivu, la hasha hakikisheni mnapoona jambo sio sawa tunajulishana mapema na kuchukua hatua Ili kuendelea kufaidi matunda ya amani yetu,” amesema.
Diwani wa Ngarenaro, Issaya Doita amesema wamevunja baraza hilo wakiwa na mengi ya kujivunia ikiwemo kuongeza mapato ya jiji na kukwamua miradi mingi iliyokuwa imekwama na kuacha mingine ikiwa katika hatua ya utekelezaji.