Unguja. Baraza la Wawakilishi la Kumi linafikia tamati ya uhai wake baada ya kipindi cha miaka mitano, likiacha kumbukumbu ya kumaliza majukumu yake chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), mfumo wa utawala unaojumuisha vyama vikuu vya siasa viwili, CCM na ACT-Wazalendo.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Hussein Mwinyi, anatarajiwa kulihutubia Baraza la Wawakilishi la Kumi na baadaye kulivunja Jumatatu ya Juni 23, 2025.
Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Mselem, amesema kuwa Rais Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kulivunja rasmi Baraza hilo Jumatatu, Juni 23, 2025, saa nne asubuhi.
Tukio hilo litatanguliwa na gwaride maalumu litakalofanyika katika viwanja vya Baraza kama sehemu ya hafla ya kufunga shughuli za Baraza la Kumi.
Amesema kukamilika kwa uhai wa Baraza la Wawakilishi kunatokana na masharti ya Kifungu cha 92(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachoeleza kuwa:
“Maisha ya Baraza la Wawakilishi yataendelea kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia tarehe ile ile ilipotangazwa rasmi kuanzishwa kwa mkutano wake wa kwanza.”
Raya amesema kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 91(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar, miongoni mwa sababu zinazompa Rais wa Zanzibar uwezo wa kulivunja Baraza ni pale ambapo uhai wa Baraza unamalizika.
“Hivyo, Ofisi ya Baraza inapenda kuujulisha umma kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, anatarajiwa kulihutubia Baraza na baadaye kulivunja rasmi siku ya Jumatatu, Juni 23, 2025,” amesema Raya.
Amesema kuwa pamoja na tukio la kuvunjwa kwa Baraza, shughuli nyingine zitakazofanyika siku hiyo jioni ni pamoja na sherehe za kuwapongeza na kuwaaga wajumbe wa Baraza la Kumi.
Katika kipindi chake cha miaka mitano, Baraza limetunga sheria mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar (2021), ambayo ilianzisha mamlaka maalumu ya kudhibiti matumizi na ununuzi wa dawa za kulevya katika Visiwa vya Zanzibar.
Baraza pia lilitunga Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (2023), iliyounda mfuko maalumu wa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha, Baraza lilitunga sheria nyingine kadhaa ikiwemo Sheria ya Mahakama za Kadhi (2023), iliyotambua rasmi mahakama za dini (Kadhi) Zanzibar, pamoja na Sheria ya Wakala wa Uwekezaji Zanzibar (2023), ambayo ilianzisha mfumo rasmi wa kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji ndani ya Zanzibar.
Tofauti na Baraza la Wawakilishi la Kumi, ambalo limeendesha shughuli zake kikamilifu chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Baraza la Tisa lilikuwa na hali tofauti.
Ingawa SUK ilianza kutekelezwa rasmi mwaka 2010, wakati Rais wa Awamu ya Saba, Dk Ali Mohamed Shein, alipomaliza muda wake na kulivunja Baraza hilo mwaka 2020, hakukuwa na wajumbe wa upinzani walioteuliwa kushiriki katika Serikali hiyo ya mseto.
Hali hiyo ilitokana na msimamo wa upinzani kususia ushiriki wao katika uchaguzi wa marudio kufuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Katika uchaguzi huo, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) alijitangaza kuwa mshindi wa urais kupitia Chama cha Wananchi CUF, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wakati huo, Jecha Salim Jecha (marehemu), alifuta matokeo ya uchaguzi huo na kutangaza uchaguzi wa marudio.
CUF, chini ya Maalim Seif, waligomea kushiriki uchaguzi huo wa marudio, hali iliyosababisha nafasi ya upinzani katika SUK kubaki wazi kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Wakati huo, SUK ilikuwa inaundwa na CCM na CUF, kabla ya uongozi wa CUF ulioongozwa na Maalim Seif kuhamia chama kipya cha ACT-Wazalendo, kilichochukua nafasi ya CUF kama chama mshirika katika SUK kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.
Pia, Baraza la Kumi linamaliza muda wake huku likiwa limepoteza wawakilishi watatu waliokuwa sehemu ya baraza hilo, baada ya kufariki dunia, mmoja wao akiwa hajawahi kuapishwa tangu kuteuliwa.
Tukio jingine lililoacha alama katika baraza hili ni uamuzi wa aliyekuwa Mwakilishi, Panya Abdalla (marehemu), kususa na kutoka kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kwa kupinga baadhi ya hoja zilizowasilishwa.
Tukio hilo lilijitokeza wakati Baraza hilo lilipokuwa likijadili na hatimaye kupitisha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ambapo Abdalla hakuafiki msimamo wa Baraza juu ya vipengele fulani vya sheria hiyo.
Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka kupitia CCM, Issa Haji Ussi (maarufu kama Gavu), aliwahi kukumbana na hatua za kinidhamu kutoka kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, ambaye alimtangaza rasmi kuwa mtoro wa Baraza na kuwasilisha taarifa zake kwa chama chake ili zichukuliwe hatua stahiki.
Spika Maulid alitumia masharti ya Kanuni ya 79(6) ya Baraza la Wawakilishi, ambayo inaelekeza kuwa mwakilishi yeyote asiyehudhuria vikao vitano mfululizo bila sababu za msingi atatangazwa na Spika kuwa mtoro, na taarifa zake zitawasilishwa kwa chama chake ili kuchukuliwa hatua stahiki.
Kanuni hiyo pia inaelekeza kuwa mwakilishi atakayebainika kuwa mtoro hatastahili kulipwa posho kwa kipindi chote cha utoro wake.
Kwa mujibu wa masharti hayo, Spika Maulid alimtangaza rasmi Gavu kuwa mtoro wa Baraza na kuwasilisha taarifa zake kwa chama chake ili zichukuliwe hatua stahiki.
Hata hivyo, inafahamika kuwa Gavu alikuwa ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa msaidizi wake, hali iliyomlazimu kutumia muda mwingi kutekeleza majukumu ya kitaifa nje ya Baraza.
Mkurugenzi wa shughuli za Baraza, Othman Ali Haji, akizungumzia baraza hilo la kumi, mesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa Baraza hilo hadi kuahirishwa kwake na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, tarehe 19 Juni 2025, jumla ya hoja binafsi nane zimewasilishwa, huku miswada ya sheria 42 ikijadiliwa na kupitishwa na Baraza.
Baraza la Wawakilishi la 10 Zanzibar lilianza rasmi kazi zake kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, na mkutano wake wa kwanza ulifanyika mnamo Novemba 2020, ukiashiria mwanzo wa shughuli za kibunge kwa kipindi cha miaka mitano.
Kwa mujibu wa Haji tangu kuzinduliwa kwa baraza hilo mpaka linaahirishwa kwa kuhutubiwa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla Juni 19, 2025, zimewasilishwa hoja binafsi nane na miswada ya sheria 42 imejadiliwa na kupitishwa.
“Yameulizwa maswali ya msingi 2,558 na maswali ya nyongeza 5497 kwa kipindi chote hicho kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,” amesema.