ZDCEA yatangaza dau Sh10 milioni kumnasa mtuhumiwa dawa za kulevya

Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) imetangaza kutaifisha mali za mtuhumiwa wa dawa za kulevya Said Seif Salum zenye thamani ya Sh966 milioni kuwa mali ya Serikali.

Pia imetangaza dau la Sh10 milioni kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.

Akitoa tamko hilo leo Juni 20, 2025 kwa vyombo vya habari, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhani Zuberi Nassoro, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya watuhumiwa wawili kukamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroini na kumtaja mtuhumiwa huyo.

“Novemba 5, 2024 Mamlaka ilifanya operesheni maalumu katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kufanikiwa kukamata watuhumiwa wawili wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroini,” amesema.

Watuhumiwa hao walipohojiwa walieleza kuwa wanapewa dawa za kulevya na bosi wao anayefahamika kwa jina la Said Seif Salum, maarufu kwa jina la Said Obama mkazi wa Zanzibar, Dar es Salaam na Kenya.

”Mtuhumiwa huyo bado tunaendelea kumtafuta na akitiwa mikononi atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Kanali Burhani amesema atakayefanikisha mtuhumiwa huyo kukamatwa pamoja na kubaini mali zake zilizopo Zanzibar na nje ya Zanzibar, atazawadiwa Sh10 milioni.

Amesema imebainika kuwa mtuhumiwa huyo anafanya uhalifu wa dawa za kulevya katika eneo la Afrika Mashariki na amekuwa akishirikiana na mitandao mikubwa ya kihalifu ya kimataifa, kuingiza dawa za kulevya kutoka Afghanistan na kuzisambaza katika nchi za Afrika Mashariki kwa muda mrefu.

Kanali Burhani mesema kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 73 (1) cha Sheria ya namba nane ya mwaka 2021 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar,
na kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 71 cha sheria hiyo, anaitafishwa nyumba iliyopo Mtendeni Wilaya ya Mjini kuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata hivyo, mtu yeyote ambaye hajaridhika na tamko hili anaweza kuiomba Mahakama kufanya mapitio na ombi lake ambalo linatakiwa kuwasilishwa mahakamani ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya leo kama inavyoelekezwa na kifungu cha 73 (4) cha Sheria Nambari 8 ya mwaka 2021 cha Sheria ya Zanzibar.

Baadhi ya wananchi wamehoji usalama wa wale wanaotoa taarifa za siri kwa mamlaka hiyo kwa madai kwamba watu wanaojihusisha na mtandao wa dawa za kulevya wana nguvu kubwa, hivyo wanaweza kuwafanya chochote.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo Kanali Zuberi amesema sheria inayohusika inaitaka Mamlaka kumlinda mtoa taarifa za siri.

Amesema kupitia sheria hiyo mtendaji wa taasiis hiyo anyevujisha siri za mtoa taarifa anaweza kufungwa au kutozwa faini ya Sh15 milioni.

Wakati huo huo, amesema mamlaka hiyo ipo katika wiki ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Katika kuendelea kusaidia jamii kupunguza tatizo la waraibu wa dawa za kulevya, Mamlaka inatangaza nafasi 10 kwa vijana waliyoamua kwa hiari yao kuacha matumizi ya dawa za kulevya, wenye umri kuanzia miaka 18 – 35.

“Vijana watakaojitokeza watapatiwa matibabu bure ya upataji nafuu pamoja na kufundishwa stadi za maisha kama ufugaji, kilimo, ufundi chereheni na ufundi wa gereji katika kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni – Zanzibar.

Related Posts