Zungu awashukuru wabunge akiwapa siri ya kukutana tena Novemba

Dodoma. Zikiwa zimesalia siku nane kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia Bunge, Naibu Spika Mussa Zungu amewashukuru wabunge, huku akisisitiza masuala matano muhimu ambayo, kwa maoni yake, yanaweza kuwarejesha tena katika Bunge la 13.

Zungu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 20, 2025 baada ya kipindi cha maswali na majibu alipokuwa akiwatambulisha wageni na kueleza hitimisho la miaka yake mitano ndani ya Bunge la 12.

Rais Samia anatarajiwa kulihutubia Bunge Juni 27, 2025, wakati ambapo shughuli za Bunge la 12 zitakuwa zinahitimishwa.

Baada ya hotuba hiyo, atatangaza kupitia Gazeti la Serikali tarehe rasmi ya kulivunja Bunge, ili kupisha mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mambo ambayo ameyataja Zungu kuwa yanaweza kuwarejesha wabunge hao katika nafasi zao ni: adabu, heshima, uvumilivu, kuwajali yatima na watu wenye kipato cha chini, pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia takwimu.

Zungu ametoa kauli hiyo akieleza kuwa hatakuwepo siku ya kuhitimisha rasmi shughuli za Bunge, ingawa hakufafanua atakuwa wapi. Hivyo, alisema ameamua kutumia fursa hiyo kuaga rasmi wenzake mapema.

“Kikubwa namshukuru sana Spika wa Bunge namna tulivyofanya kazi pamoja, nilijitahidi kutii maelekezo yake na kazi zikaenda, lakini nawashukuruni ninyi wabunge jinsi mlivyokuwa pamoja nasi maana bila ninyi mambo hayaendi,” amesema Zungu.

Naibu Spika amewashirikisha wabunge siri ya ushindi, akiwahimiza kuwa watulivu na kuepuka kushindana kwa matusi au fujo na wale wanaofanya hivyo.

Amesisitiza kuwa wale walioko madarakani wasijibizane kwa mtindo huo, bali waendelee kuwa na ustaarabu na busara.

Zungu ameongeza kuwa wanayo nafasi ya kurejea madarakani kwa kuwa wana kiongozi ambaye, kwa maelezo yake, ni “nusu mtu, nusu chuma”  akimaanisha uimara na uthabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, na hivyo watarejea kwa ushindi pamoja naye.

“Kasemeni mazuri ya mama na kama hamna takwimu nendeni kwa mawaziri watawapeni hizo takwimu ili mkazisemee kwa wananchi, jalini mayatima ili mpate pepo,” amesema.

Kwa upande mwingine amewapongeza wananchi wa Jimbo la Ilala akisema wamekuwa ni watu wema kwake pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambapo ameomba Rais atambue kuwa Ilala inatembea na wako pamoja.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, amesema ni muhimu watu waende na uchaguzi wa mafiga matatu ambayo ni Rais, wabunge na madiwani.

Related Posts