Dar es Salaam. Matukio ya wazazi kuua watoto wao na wenyewe kujiua yanazidi kushika kasi nchini, yakiripotiwa matano kati ya Januari hadi Juni 2025.
Kwa mujibu wa matukio ambayo Mwananchi limeyaripoti, watoto 10 wamefariki dunia pamoja na wazazi wawili, mmoja kwa kujiua na mwingine kuuawa pamoja na mwanaye.
Katika matukio hayo yaliyofanywa na wazazi, chanzo kinatajwa kuwa migogoro ya kifamilia, wivu wa mapenzi na changamoto ya afya ya akili.
Kati ya hao, wapo wazazi waliojiua baada ya kutekeleza matukio hayo, wengine wakinusurika baada ya kujaribu kujiua, huku wengine wakishikiliwa na Jeshi la Polisi.
Tukio la hivi karibuni ni la Ijumaa Juni 20, lililotokea mkoani Kilimanjaro ambako Mary Mushi (26), mkazi wa Kijiji cha Mungushi, wilayani Hai anadaiwa kuwaua wanaye wawili, wa miaka minne na wa miezi sita, kisha kujijeruhi, chanzo kikitajwa mgogoro wa kifamilia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Abel Mtagwa Juni 20, alisema baada ya tukio hilo mama huyo alijijeruhi kifuani, tumboni na kwenye koromeo kwa kitu chenye ncha kali.
Tukio hilo lilitokea siku moja baada ya jingine la Juni 19 mkoani Tabora, ambako mkazi wa Kata ya Lugubu, wilayani Igunga, Kang’wa Mahigi (25) aliwanywesha sumu ya kuua wadudu watoto wake wanne, kisha naye akajiua kwa sumu hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Richard Abwao akizungumzia tukio hilo alisema mama huyo alisubiri mumewe alipokwenda shambani, ndipo alipotekeleza tukio hilo, chanzo kikidaiwa kuwa wivu wa mapenzi.
Kang’wa aliyekuwa mke mkubwa, ilidaiwa hakuridhishwa na mwenendo wa mumewe kumpendelea mke mdogo, ikiwamo kumjengea nyumba ya kisasa.
Ukiachana na hayo ya wiki hii, Februari 26, 2025 katika Kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma mtoto wa miaka 11 alifariki dunia ikidaiwa ni baada ya kupigwa ngumi, mateke na kuvunjwa mkono na baba yake mzazi, Fidelis Nyoni.
Lingine ni la Februari 17, 2025, pale mkazi wa Kijiji cha Kisangile wilayani Kisarawe, Tanganyika Masele (32) alipokamatwa na polisi akituhumiwa kuwaua mke na mtoto wake wa miaka miwili, ikidaiwa ni kutokana na wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi mtuhumiwa huyo alitekeleza mauaji hayo kwa kuwakata mapanga kisha kutupa miili yao karibu na bwawa jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi.
Fungua dimba kwa mwaka huu ni tukio la Januari 11, 2025 la mkazi wa Kijiji cha Namsinde mkoani Songwe, Junge Jilatu kudaiwa kuwaua watoto wake wawili kwa kuwakaba kwa kamba wakiwa wamelala, kisha kuwachoma na kitu chenye ncha kali shingoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga alisema chanzo cha mauaji hayo ni msongo wa mawazo. Baada ya kuwaua, mwili wa mtoto mmoja aliutupa kwenye mtaro wa maji kando mwa barabara.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hili ni msongo wa mawazo baada ya baba wa watoto hao kumtuhumu mke wake kuwa amezaa na ndugu wa karibu wa familia yake,” alisema Kamanda Senga.
Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa Taasisi ya Mental Health Tanzania (MHT) na daktari wa magonjwa ya akili, Firmina Scarion amesema matukio ya aina hiyo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na changamoto ya afya ya akili.
Amesema kutokana na hali hiyo, ipo haja ya uwekezaji kufanyika kwenye utoaji wa elimu ya afya ya akili ili watu wengi wawe na uelewa na kuchukua tahadhari dalili mbaya zinapoanza kujitokeza.
“Tuna shida ya uelewa, kuna magonjwa yanayogusa utu kama vile hasira na ukatili, sasa hadi mtu anafikia kuua ujue fika kwamba kihisia, kifikra hata kimtazamo hayuko sawa. Inawezekana kabisa dalili zilikuwapo lakini kwa sababu watu wengi hawajui, imeshindikana kuepusha madhara hayo,” amesema.
Amesema magonjwa ya akili yapo ya aina mbalimbali, akieleza: “Kuna yale ambayo unasikia sauti, inawezekana zikawa zinakuhamasisha kufanya vitu vibaya, kwa mfano unaambiwa wewe hufai, familia yako haikujali hakuna anayekuthamini hapa duniani ni heri ujiue.
“Sasa kama mgonjwa atasikiliza sauti hizi ndiyo anaweza kufikia uamuzi wa kuua watoto na yeye kujia, anaona kama watu hawamjali hakuna sababu ya kuwaacha watoto wateseke, ni heri wote waondoke duniani. Hii ni shida kubwa ndiyo maana tunasisitiza kufahamu dalili za changamoto ya afya ya akili na kutafuta matibabu.”
Ukiacha hilo, Mwanasaikolojia Jacob Kilimba amesema hadi kufikia hatua ya kuua na kujiua ni matokeo ya mtu anayepitia msongo wa mawazo kwa muda mrefu bila kupata msaada.
Amesema mzazi anapopitia hali hiyo bila kupata msaada, huweza kufikia hatua ya kukata tamaa na hali huwa mbaya zaidi endapo msongo huo utakuwa mkubwa.
“Katika baadhi ya matukio, mzazi huanza kuamini maisha hayana tena maana na hufikiria kujiua. Kwa baadhi kuwahusisha watoto kwenye tukio hili huonekana kama njia ya kuwaondolea mateso au kuwakinga na maisha magumu yajayo,” amesema.
Wataalamu hao wakiwa na mtazamo huo, Mshauri wa masuala ya familia Getrude Kibela amesema hali hiyo pia inaweza kuchangiwa na migogoro ya kifamilia hasa pale talaka au kutengana kunapotokea, mzazi mmoja anaweza kuhisi amekataliwa au kupoteza nafasi ya kuwa karibu na watoto wake.
Amesema hisia hizo huweza kusababisha chuki, hasira na matamanio ya kisasi, hali inayoweza kumfanya aone kifo kama njia ya kumkomoa mwenza wake.
Anasema wazazi wengine huwachukulia watoto kama mali yao binafsi, hivyo hupata ugumu wa kukubali kuwa wanaweza kulelewa na mzazi mwingine au kuishi maisha yasiyo ya udhibiti wao.
“Katika hali hii, mzazi anaweza kuamua kwamba kama yeye hawezi kuwa na watoto, basi hakuna mwingine anayepaswa kuwamiliki, hatua ambayo humsukuma kufanya mauaji,” amesema.
Ukubwa wa tatizo la afya ya akili unabainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ripoti ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili, akisema walibani ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.
CAG alisema vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kupona, akieleza kati ya mikoa 28, ni mitano pekee ina vituo vya utengamo vya huduma hiyo.
Alisema mwaka 2022 iliripotiwa katika Hospitali ya Taifa ya Akili ya Mirembe, kulikuwa na ongezeko la idadi ya wagonjwa waliopatiwa matibabu ya magonjwa ya akili kutoka wagonjwa 3,472 mwaka 2019 hadi 5,060 mwaka 2022, sawa na asilimia 31 ya ongezeko.
CAG alisema kumekuwa na ukosefu wa umakini katika kutambua watu wenye changamoto, badala yake juhudi za utambuzi zinazingatia makundi mengine yenye udhaifu.
CAG alisema huduma za kisaikolojia na kijamii hazijaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera na programu katika ngazi mbalimbali za utawala.
Pia kuna uhaba mkubwa wa wataalamu, miundombinu, vifaatiba na dawa za kufanikisha utoaji wa huduma za afya ya akili.
Alipendekeza Wizara ya Afya iandae miongozo ya kliniki ya kitaifa na taratibu za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuunda miundombinu ya urekebishaji kwa huduma za afya ya akili.
Ihakikishe kuna upatikanaji wa wafanyakazi wenye uwezo na vifaa muhimu kwa huduma za afya ya akili.
Licha ta kasoro hizo, Serikali imepanua wigo wa huduma za ushauri na afya ya akili ambazo zinapatikana katika vituo 701 vya kutolea huduma nchini.
Akijibu swali bungeni Aprili 16, 2025 Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema huduma hizo zinapatikana katika hospitali za rufaa za mikoa na Hospitali ya Afya ya Akili ya Mirembe.
Alisema Serikali imewajengea uwezo wataalamu 2,840 wa afya wakiwamo madaktari na wauguzi ili waweze kutambua na kushughulikia changamoto za magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo matatizo ya afya ya akili.
Alisema Serikali imeanzisha huduma ya kituo cha simu za miito (Call Centre) kupitia namba 115, ambayo wananchi wanaweza kupata ushauri wa afya ya akili kwa njia ya simu, hatua inayochochea kupunguza unyanyapaa na kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Pia imeanzisha vituo 1,561 vya huduma rafiki kwa vijana katika mikoa yote, kupitia Mkakati Jumuishi wa Vijana (NAIA), ambavyo vinatoa huduma za afya ya akili kwa njia rafiki, inayozingatia mazingira ya vijana.