Makocha 29 wapigwa msasa Arusha

Makocha 29 wamemaliza kozi ya awali ya ukocha wa soka maarufu kama Fifa Grassroots Football Coaching Course kwa ajili ya kufundisha vijana na watoto.

Mafunzo hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Royal eneo la Sinoni Unga Ltd na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid yakiandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA)  yakiendeshwa na mkufunzi wa TFF, Raymond Gweba.

Washiriki 29 kutoka mikoa ya Arusha, Tanga, Kagera, Mwanza na Kilimanjaro wanawake wakiwa 13 na wanaume 19 walishiriki kwa siku tano kupatiwa mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa ARFA, Zakayo Mjema akizungumza na Mwanaspoti wakati wa kufunga mafunzo amewashauri washiriki kutafuta taasisi za soka, shule na timu za vijana na watoto kwenda kutoa maarifa na ujuzi walioupata.

“Badala ya kuweka vyeti vyako kwenye droo tumieni elimu mliyoipata kuwainua wachezaji wajao wa soka nchini kwa ngazi ya chini na hiyo pia itatengeneza fursa nzuri kwenu,” amesema Mjema.

Ameongeza kuwa anapanga kutembelea takriban vituo 24 ambavyo vilipeleka washiriki ili kuona namna gani wanaendelea kuibua vipaji ambapo kama kutakuwa na changamoto ikiwemo vifaa vya michezo ARFA itakuwa tayari kuwasaidia.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Gweba amesema yalitolewa kwa nadharia na vitendo kwa kutumia wanafunzi wa Shule ya Royal kama kielelezo cha kufundishia.

“Kumekuwa na matokeo chanya kutokana na kozi hizo kwani kwa sasa kuna vituo vingi vya mafunzo ya soka vinavyoanzishwa kote nchini,” amesema Gweba.

Amesema kinachopatikana ndani ya mafunzo hayo ni kumwezesha kocha wa soka kupata elimu ya awali kufundisha mchezo huo ambapo kozi hiyo imejikita kwa watoto kuanzia umri wa miaka minne hadi 12.

“Ndani ya kozi hii pia kuna eneo la pili la Fifa Football for Schools ambayo inamwezesha mwalimu kuweza kufanya programu hizi kuanzia miaka minne mpaka 14,” amesema.

“Ikimaanisha kwamba kwa mtoto wa kidato cha kwanza hadi kidato cha pili naye anaweza kupata elimu akiwa amefundishwa na mwalimu wake.”

ARFA kwa kushirikiana na TFF inapanga kuendesha kozi nyingine ya ukocha ya leseni ya CAF Diploma D ambayo itaanza Julai Mosi, mwaka huu.

Related Posts