MAT yaitaka Serikali kuja na suluhisho ajira za madaktari, ubora wa huduma

Arusha. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kupitia mkutano wake mkuu, kimetoa maazimio manne ya kisera yanayolenga kuboresha sekta ya afya nchini.

Maazimio hayo yanaitaka Serikali kuongeza kasi ya ajira kwa wataalamu wa afya, kuongeza bajeti ya afya, kuboresha ubora wa huduma, pamoja na kuimarisha hatua za kinga dhidi ya magonjwa kwa manufaa ya wananchi.

Kwa mujibu wa MAT, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuwaandaa wataalamu wa afya na kwa sasa idadi yao inaridhisha.

Hata hivyo, changamoto iliyopo ni jinsi wataalamu hao watakavyotekeleza kwa ufanisi majukumu ya taaluma waliyoisomea, ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya.

Maazimio hayo yametolewa leo Ijumaa, Juni 20, 2025 wakati wa kufungwa kwa Kongamano la Kitaifa la Tiba na Maadhimisho ya miaka 60 ya MAT.

Akitoa maazimio hayo, Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko amesema nchi haiwezi kuwa na ubora wa huduma, ikiwa na vituo vingi vinavyowekwa bila kuwa na watoa huduma za afya.

Dk Nkoronko amesema katika sekta ya afya kuna upungufu wa zaidi ya asilimia 55, na katika hilo wote wanawajibika kwa pamoja kuona namna gani upungufu huo utazibwa.

Hata hivyo akifungua kongamano hilo Juni 18, 2025 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema sekta ya afya itaendelea kuwa kipaumbele muhimu na kwamba Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya.


“Mpaka sasa tayari imeajiri watumishi 48,633 wa sekta ya afya na kufanya idadi ya watumishi wa sekta kufikia 177,711 ambayo imewezesha kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta hiyo kutoka asilimia 64 hadi 55,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia changamoto hiyo, Dk Nkoronko amesema nchini kuna shule 12 zinazofundisha shule ya udaktari na hizo zote zinazalisha madaktari 1,500 kila mwaka ambao huingia kwenye soko.

“Tunao madaktari tarajali ambao kwa mwaka huu wamesajiliwa 3,500 na hawa wote ni madaktari ambao tayari tunao, hivyo kwa sasa hatuna shida na kusomesha na kupata wataalamu sasa hivi tuna shida na kuajiri.

“Tunashkuru jitihada za vibali vya ajira ambavyo vinatoka mara kwa mara kwa kada hii, ushauri wetu kama madaktari, tuongeze kasi katika kuajiri tuone tutakuza uchumi kwa kiasi kikubwa, japokuwa unakua baada ya Uviko-19 umekua kwa asilimia 4.6 endapo utakua kwa asilimia 8 mpaka 10, tutakuwa na uwezo wa kuajiri Zaidi,” amesema Dk Nkoronko.

Amesema ili kufanikisha changamoto zilizopo Serikali iongeze bajeti ya kushughulikiwa afya kama ilivyokuwa kwenye makubaliano ya Abuja, kwamba Serikali zote zitenge kiasi cha asilimia 15 katika bajeti yake kushughulikia afya.

Dk Nkoronko amesema miaka ya hivi karibuni kumekuwa na asilimia 5.6, asilimia 5.8 na asilimia 5.4 za bajeti zinazotolewa hivyo nchi iko chini ya asilimia 10.

“Tunajua keki ya Taifa matatizo yetu ni mengi, lakini endapo watu wetu wasipokuwa na afya hatuwezi kuzalisha uchumi na wala kuwahudumia. Tunaomba Serikali iongeze bajeti angalau tufikie asilimia 10 kwa miaka mitano ijayo ili tuweze kusogea kutoka hapa tulipo tunapoifikia 2050 tufikie malengo yaliyowekwa,” amesema.

Akizungumzia mambo mengine muhimu ya kisera amesema katika mkutano huo, yameibuka masuala mengi kwamba bado huduma za afya bora, rafiki na salama hazipatikani maeneo yote nchini.

Dk Nkoronko amesema bado kuna mapungufu katika baadhi ya maeneo ya utoaji huduma, hivyo ametoa wito kwa mamlaka husika, wananchi na wadau kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha huduma bora zinatolewa na malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Amesisitiza umuhimu wa kudumisha ubora wa huduma kuanzia ngazi ya msingi hadi Hospitali ya Taifa, akiwataka wataalamu wa afya, wakiwemo madaktari, kutoa huduma kwa viwango stahiki.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika elimu ya kinga kwa wananchi, akibainisha kuwa licha ya kuwepo kwa kitengo maalum wizarani, bado nguvu zimeegemea zaidi kwenye tiba kuliko kinga.

Ameonya kuwa ifikapo mwaka 2040, magonjwa yasiyoambukiza kama ajali, kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo yatakuwa changamoto kubwa, lakini yanaweza kuzuilika endapo juhudi za kinga zitapewa kipaumbele.

Related Posts