Moshi. Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Baraza la Madiwani, ndoto ya kuipandisha hadhi Moshi kuwa jiji, suala hilo limeendelea kuwa changamoto.
Ndoto ya kuifanya Moshi kuwa jiji imekuwa katika mchakato tangu mwaka 2012, baada ya Rais wa Nne, Jakaya Kikwete kuagiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi (MMC) na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (MDC) kukaa meza moja na kutatua tofauti zao.
Lengo lilikuwa kuhakikisha mji huo unapandishwa hadhi na kuwa jiji ifikapo mwaka 2015. Hata hivyo, hadi sasa ndoto hiyo haijatimia.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuagana kwa madiwani baada ya kumalizika kwa muda wao wa uongozi jana Juni 20, 2025, Meya Kidumo amesema moja ya matarajio makubwa waliyoingia nayo madarakani mwaka 2020, ilikuwa ni kuona Moshi inapandishwa hadhi kuwa jiji.
Hata hivyo, ameeleza kuwa lengo hilo halijafikiwa kutokana na changamoto zinazohusiana na vigezo vya msingi, hasa katika ukusanyaji wa mapato.
“Tumekuwa na ndoto kubwa ya Moshi kuwa jiji, lakini tumeshindwa kulitekeleza hilo kwa miaka hii mitano. Tumekosa baadhi ya vigezo, hasa katika mapato, ukubwa wa eneo la manispaa na idadi ya watu. Hivyo, kwa sasa tulielekeza nguvu zetu katika kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kufikia hadhi hiyo,” amesema Kidumo.
Akitathmini mafanikio ya kipindi hicho, Kidumo ameeleza kuwa Manispaa ya Moshi imepiga hatua kubwa katika makusanyo ya mapato ya ndani ambapo yameongezeka kutoka Sh6 bilioni mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh10 bilioni kwa mwaka 2025/2026.
“Ongezeko hilo ni ishara ya usimamizi mzuri wa rasilimali na ufanisi wa utendaji wa halmashauri. Haya ni mafanikio makubwa kwa muktadha wa manispaa yetu yenye eneo dogo na idadi ndogo ya watu. Tunapaswa kuendelea kushirikiana kuhakikisha mapato yanazidi kuongezeka,” amesema Kidumo.
Aidha, ametaja miradi mikubwa iliyotekelezwa ndani ya kipindi hicho kuwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi mpya katika kata nane, ujenzi wa shule mpya, vituo vya afya, upanuzi wa mtandao wa barabara za lami, pamoja na ujenzi wa soko la kisasa la Mbuyuni.
Hata hivyo, Kidumo amesema baadhi ya miradi waliyoikusudia haijakamilika na kuwa wanaamini watendaji chini ya Mwajuma Nasombe, mkurugenzi wa mtendaji wa halmashauri hiyo itakamilika kama ilivyokusudiwa.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza kipindi hiki salama, pia tunawaomba watendaji wasibweteke. Kuna kazi ambayo haijakamilika, na ni wajibu wao kuikamilisha kwa manufaa ya wananchi,” amesema.
“Lakini, pia nitoe shukrani kwa madiwani wenzangu na watumishi wa halmashauri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi chote cha uongozi wangu, kwani mafanikio yaliyopatikana ni zao la mshikamano, maono ya pamoja na kujitoa kwa dhati kwa ajili ya maendeleo ya Moshi”.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amewataka viongozi na watendaji wote wa manispaa kuimarisha mahusiano ya kikazi na kijamii, huku akionya tofauti za kisiasa na binafsi zisiathiri kazi ya kuwahudumia wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya pia amewataka viongozi wote wa kuchaguliwa, kuteuliwa na watendaji kuungana na kushirikiana kwa bila kuleta makundi wala matabaka, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki na kuifanya Moshi kuwa eneo la fahari kwa wote.
“Tumepewa watu wa kufanya nao kazi. Hatuwezi kukwepana. Sisi sote tunawahudumia wananchi wale wale wa Moshi. Tuwe na tofauti zetu binafsi, lakini kazi inapotuita hatuna budi kushirikiana,” amesema Mnzava.
Amehimiza kuwa uhusiano mwema kazini si hiyari bali ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma, ingawa kila mmoja anaweza kuwa na mitazamo tofauti au kutoelewana binafsi, lakini suala la kazi linapaswa kupewa kipaumbele.
“Tunaweza tusielewane katika mambo mengine, lakini si kazi. Tusifanyiane fitina wala kuumizana. Collective responsibility (uwajibikaji wa pamoja) inaanzia kwenye mahusiano,” amesema.
Mkuu huyo wa wilaya pia amezungumzia kipindi cha uchaguzi kinachokaribia na kuonya dhidi ya migawanyiko na chuki zinazoweza kujitokeza kati ya viongozi na makundi mbalimbali ya kisiasa.
“Najua tunaelekea kwenye uchaguzi. Kila mmoja atakuwa na timu yake, ndiyo mambo ya uchaguzi hayo. Lakini isifike mahali tukaumizana au kujeruhiana kwa sababu ya uchaguzi.
“Tutambue hata baada ya uchaguzi kuna maisha yatapaswa kuendelea. Isije ikafika mahali tukashindwa hata kusalimiana baada ya uchaguzi. Si utamaduni wetu wa Kitanzania. Twende kwa heshima, upendo na mshikamano,” ameongeza Mnzava.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Jumanne Nasombe, amesema mapato ya halmashauri yameendelea kuongezeka, na kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026, makadirio ya ukusanyaji mapato ni Sh11.2 bilioni ikilinganishwa na Sh6.1 bilioni tulizokusanya wakati Baraza hili linaingia madarakani. Hii inaonyesha ongezeko la Sh5.1 bilioni,” amesema Nasombe.