Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema utalii ambao inawekea mikakati kuukuza lazima uendane na uhifadhi wa mazingira na wadau wote washiriki katika utekelezaji wa mpango huoili kuimarisha utalii endelevu.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, ametoa kauli hiyo leo Juni 21, 2025 alipofungua maonyesho ya pili ya utalii na uwekezaji katika kituo cha maonyesho ya biashara Nyamanzi, Unguja.
Amesema utunzaji wa mazingira ni nguzo muhimu katika kuhakikisha Zanzibar inabakia kuwa kivutio bora cha utalii wa kimataifa ili sekta ya utalii iwe endelevu.
Amesema mkakati huo unalenga kushirikisha wadau wote – wananchi, sekta binafsi, taasisi za elimu na mashirika ya kimataifa ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaoweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya utalii.
“Hatua hii muhimu ya kulinda rasilimali za asili zilizopo Zanzibar, zikiwamo fukwe, misitu na viumbe hai vya baharini ambavyo vina mchango mkubwa katika kuvutia watalii na kuinua uchumi wa nchi,” amesema.

Amesisitiza kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa taka zake kwa kuwa wanahitaji visiwa viwe safi mjini na maeneo ya pembezoni ambako shughuli za utalii zinaongezeka.
Waziri Soraga amesema licha ya mafanikio yanayoonekana katika sekta hiyo, Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa maeneo ya kufikia wageni kutokana na kasi kubwa ya ujio wao, hivyo kunahitajika uwekezaji zaidi katika nyumba za wageni na hoteli za kisasa.
“Ni wakati wa kujipambanua zaidi kwa kuwaita wawekezaji katika miradi mikubwa ya hoteli zenye hadhi ya kimataifa,” amesema.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Aboud Jumbe amesema maonyesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya utalii endelevu inayolenga kuimarisha utalii wa Zanzibar katika soko la kimataifa.

“Maonyesho haya yanaonyesha maendeleo tuliyoyafikia katika sekta ya utalii ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Hussein Mwinyi. Sekta hii inachangia theluthi moja ya pato la Taifa,” amesema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waongoza Watalii Zanzibar (Zato), Khalifa Mohammed Makame amesema maonyesho hayo ni nyenzo muhimu kwa sekta ya utalii, kwani yanawapa watoa huduma fursa ya kubadilishana uzoefu na kujitangaza, hivyo kusaidia kukamilisha mnyororo mzima wa huduma za utalii.
“Tunaipongeza Serikali kwa mkakati huu wa usafi kwani utasaidia kuhifadhi fukwe, misitu na mazingira kwa ujumla, ambavyo ni bidhaa muhimu kwa sekta ya utalii,” amesema.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Arrif Abas Manji amesema hafla hiyo haikuwa tu maonyesho, bali pia sehemu ya majadiliano ya kina kuhusu sekta ya utalii, changamoto zake na fursa zinazopatikana, kwa kushirikiana na nchi zilizoshiriki.
Arrif amesema wanunuzi 57 wa kimataifa kutoka Ugiriki, Uholanzi, Hispania, Ujerumani, Kenya, Marekani, Mauritania, India, Uganda, Afrika Kusini na Dubai wameshiriki ikiwa ni ishara ya kuongezeka kwa mwonekano wa kimataifa wa Zanzibar na umuhimu katika duru za utalii na biashara.
Amesema Zanzibar imerekodi jumla ya wageni 736,755 wa kimataifa mwaka 2024 na kuashiria ongezeko la asilimia 15.4, ikilinganishwa na wageni 638,498 walioingia mwaka 2023. Ongezeko hili amesema linaelezea juu ya mvuto wa Zanzibar katika utalii.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga (wa pili kushoto), akiangalia bidhaa wanazotengeneza wanawake kutoka kikundi cha mama’s group wakati wa maonyesho ya Utalii na Uwekezaji katika viwanja vya maonyesho Nyamanzi Mkoa wa Mjini Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Baadhi ya washiriki wa maonyesho hayo wamesema ni fursa adhimu kujitangaza na kubadilishana uzoefu hasa kuonyesha uhalisia wa utamaduni wa Zanzibar, yakiwamo mapishi.
Maskat Shineni Abdalla, kutoka taasisi ya Mama’s of Zanzibar amesema maonyesho hayo yanasaidia kutangaza vivutio vya utalii wa utamaduni na hata wajasiriamali wadogo, hasa kina mama kujitangaza zaidi kibiashara.
Ofisa Masoko, Bodi ya Utalii Tanzania, Nassor Hassan Garamatatu amesema maonyesho hayo yana manufaa makubwa ambayo yamewawezesha kukutana na wadau, ambao watawasaidia kuongeza idadi ya watalii.
Amesema kwao ni fursa ya kujitangaza na hata kutangaza utalii, hayo yakitokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Mwinyi kutangaza utalii duniani.
Amewashauri wananchi kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vyao vya utalii vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar, ili vizazi viweze kufahamu mapema historia ya nchi yao kupitia rasilimali zilizopo.
Maonyesho hayo yamehusisha wadau wa sekta ya utalii, wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji, ambao wamepata nafasi ya kujionea bidhaa na huduma za utalii na kuimarisha ushirikiano wa biashara.