Babati. Wasichana kutoka jamii za wafugaji katika mikoa mitatu ya Manyara, Singida na Dodoma wamepatiwa fursa ya kujifunza ujuzi wa fani mbalimbali kupitia Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Wasichana hao kutoka jamii za kifugaji watapata fursa ya kupata ujuzi na utaalamu kupitia Chuo cha Veta cha Gorowa, ambacho kinalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika fani za ufundi.
Lengo ni kuhakikisha Taifa linakuwa na idadi ya kutosha ya wataalamu wa kike na kukuza usawa wa kijinsia katika sekta ya kiufundi.
Mwaka jana Veta ilieleza kuwa imedhamiria kutoa kipaumbele katika kudahili wasichana wanaoomba kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo vyake, ili kukuza uwiano wa kijinsia na kufikia shabaha ya asilimia 50 ya udahili wa wasichana.
Kipaumbele hicho kinaenda sambamba kutoa ufadhili au ruzuku kwa wasichana wanaotoka kwenye mazingira magumu na kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na wafadhili kuimarisha mazingira ya ujifunzaji kwa wasichana.
Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati inajumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara, Ramadhani Mataka ameeleza kuhusu ushiriki wa wasichana kutoka jamii za wafugaji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 21, 2025, katika Chuo cha Veta Gorowa, kilichopo wilayani Babati.
Amesema kuwa wameamua kukiteua Chuo cha Veta Gorowa kuwa kituo pekee kinachotoa elimu ya ufundi kwa ngazi ya tatu kwa wanawake pekee, ikiwa ni mkakati wa kuongeza idadi ya wanawake wanaosomea fani za ufundi nchini, pamoja na kupanua wigo wa fursa za ajira kwao.
Amesema wameamua kuanzisha utoaji wa elimu hiyo kwa wanawake wa Mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwa kuwa kuna wafugaji waliokuwa hawatoi kipaumbele kwa watoto wa kike kusomea ufundi.
“Chuo cha Veta Gorowa kitaanza kupokea wanafunzi Julai mwaka huu ambapo wanafunzi 80 wa hatua ya tatu watakuwa wanaishi bweni na kulipia Sh120,000 kwa mwaka ila kwa watakaokosa nafasi za bweni wanaruhusiwa kupangisha mitaani na kulipa Sh60,000 kwa mwaka,” amesema Mataka.
Amesema watakaokuwa wanalala kwenye mabweni watapata huduma zote za kijamii ikiwemo chakula na kutumia karakana bila malipo.
Mataka amesema kuwa wahitimu watakaomaliza kwa mafanikio mafunzo ya ngazi ya tatu katika chuo hicho, watapata nafasi ya kujiendeleza kwa mwaka mmoja katika Chuo cha Ufundi Stadi Morogoro. Baada ya kuhitimu, wataajiriwa kufundisha masomo ya amali katika shule za sekondari, sambamba na utekelezaji wa sera mpya ya elimu.
Pia, amewaita wahitimu wa vyuo vikuu akiwataka waende Veta wakapate ujuzi wa muda mfupi na baada ya hapo wataweza kuwa walimu wa Veta.
Amesema vijana waache kupoteza muda mitaani wakiwa na shahada zao waende Veta baada ya kupewa ujuzi watakuwa wataalamu wazuri na kuajiriwa na viwanda na taasisi za umma.
Mataka ametaja fani ambazo watakuwa wanazitoa kwa wanawake ni umeme, ufundi bomba, ushonaji, ubunifu, mitindo na teknolojia ya nguo.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo cha Veta Gorowa, Joshua Matagane amesema wanawake watakaopata fursa ya kusoma hatua ya tatu watakuwa na fursa ya kuwa walimu katika shule za sekondari kufundisha masomo ya amali.
Matagane amesema chuo hicho kitaweza kupokea wanafunzi 80 wa kike ila baada ya hapo mwaka 2026 kitaongeza wanafunzi wengine 80 wa kike kwa bweni.
Pia, amesema kuanzia Januari mwaka 2026 chuo hicho kitaanza kufundisha fani za kilimo cha mbogamboga, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), uandaaji wa matunzo ya mifugo na mapishi.
Mmoja kati ya wasichana wa jamii ya kifugaji anayesomea ushonaji, Husna Boay, ameeleza kwamba kupitia ujuzi huo ataweza kufanya kazi yake kwa umahiri na ujuzi.
Boay amesema wasichana wa jamii ya kifugaji wanapata fursa nzuri kupitia chuo hicho cha Veta katika kupata utaalamu ili baadaye wafanye kazi yao kwa ufasaha.