Arusha. Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya mwaka wa fedha 2025/2026 inatarajiwa kusomwa kesho Jumatatu katika kikao kitakachofanyika kwa njia ya mtandao (virtual meeting) kutokana na ukata wa kifedha unaoikabili jumuiya hiyo.
Katika makadirio ya mwaka huu wa fedha, kiwango cha fedha kinatarajiwa kuwa pungufu kwa kile cha mwaka wa fedha uliopita kilichokua dola 112 milioni za Marekani (Sh302.4 bilioni), ambazo ni michango kutoka nchi wanachama na washirika wa maendeleo.
Miaka ya hivi karibuni, nchi wanachama wa EAC zimekua hazichangii ipasavyo hali inayosababisha kukwama kwa baadhi ya mipango iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha husika.
Kutokana na nchi wanachama kushindwa kutimiza wajibu wa kimkataba, baadhi ya vikao vya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) viliahirishwa au kufanyika kwa njia ya mtandao ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Hivi karibuni, Bunge hilo lilikutana kwa njia ya mtandao na kuidhinisha nyongeza ya bajeti ya Dola 660,690 za Marekani (Sh1.8 bilioni) kwa ajili ya mwaka wa fedha unaoisha wa 2024/2025 na kamati ya bajeti kujadili na kuchambua makadirio ya mwaka wa fedha 2025/2026
Itakua ni mara ya kwanza kwa kikao cha bajeti kufanyika kwa njia ya mtandao tangu mwaka 2021 dunia ilipokumbwa na janga la Uviko 19 lililosababishwa kuwapo masharti ya kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima.
Ofisa Habari Mwandamizi wa EALA, Nicodemus Ajak akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Juni 22, 2025, amethibitisha kikao hicho cha bajeti kufanyika kesho bila kutoa ufafanuzi zaidi.
“Nathibitisha mkutano wa pili, kikao cha tatu Bunge la tano, kikao cha bajeti kitafanyika kesho mchana kwa njia ya mtandao kuhusu makadirio ya mwaka wa fedha 2025/2026. Tutafahamu kesho wakati Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, Beatrice Askul akisoma bajeti hiyo lakini itakua pungufu ya mwaka uliopita,”amesema Ajak.
Kwa mujibu wa takwimu za mapema Juni zinaonesha nchi tatu pekee ndizo zilikuwa zimekamilisha kwa asilimia 100 michango yake ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda wakati nchi zingine zilikua zimechangia viwango tofauti.
Bajeti hiyo hugawanywa kwa mihimili mitatu ambayo ni Sekretariati ya EAC, Bunge la EALA na Mahakama ya EACJ pamoja na taasisi zake zilizopo kwenye nchi wanachama.