CRDB yaanza kutoa asilimia 10 za halmashauri, vikundi 25 vyaanza

Dar es Salaam. Baada ya kukamilisha maandalizi yote muhimu ya kuwawezesha wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imezindua utoaji wa mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Uzinduzi huo ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ulifanyika mwishoni mwa wiki umekuja baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha.

“Miaka minne iliyopita, Ilala ilikuwa inakusanya Sh61 bilioni kwa mwaka lakini sasa mapato yamepanda mpaka Sh138 bilioni hivyo fedha zinazotengwa kwa ajili ya wajasiriamali ni nyingi na zitaendelea kuongezeka kila mwaka. “Tunashirikiana na CRDB Bank Foundation kuwafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo. Niwaombe wajasiriamali walio tayari, jitokezeni ili kunufaika na mikopo hii,” amesema Mpogolo.

Akieleza utayari uliopo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amesema jumla ya Sh18 bilioni zipo tayari kukopeshwa hivyo akawataka wananchi kujitokeza, akibainisha kuwa kuna vikundi 945 vilivyojitokeza mpaka sasa.


“Asilimia nne ya fedha hizi ni kwa ajili ya wanawake na asilimia nne nyingine zimeelekezwa kwa vijana na asilimia mbili zilizobaki ni za watu wenye ulemavu. Wanawake mmepewa nafasi kubwa zaidi kwani ndani yenu kuna vijana na watu wenye ulemavu pia hivyo ukichambua kwa umakini unaweza kukuta ninyi mnapata mpaka asilimia 80 ya kiasi chote kilichopo hivyo niwasihi muichangamkie fursa hii iliyo mbele yenu,” amesema Mabelya.

Hata hivyo, walengwa wa mikopo hiyo walikumbushwa umuhimu wa kutimiza wajibu wao kwa kuepuka udanganyifu wanapotoa taarifa zao, waunde vikundi kwa nia halisi ya ujasiriamali, kusajili biashara zao na waombe mkopo kwa biashara wanazozimiliki.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, Meneja Mawasiliano wa benki  hiyo, Julius Mnganga amesema mpaka sasa wameshavifikia vikundi 120 vilivyowasilisha maombi ya mikopo yenye thamani ya Sh3 bilioni.

Hata hivyo, Mnganga amesema baada ya kuvitembelea vikundi hivyo pamoja na wanachama wake wamekuta 25 ndivyo vinakidhi vigezo vya kunufaika na mikopo hiyo kwa sasa.

“Vikundi hivi 25 vimeleta maombi yenye thamani ya Sh735 milioni. Tunaendelea kutoa elimu ili kuviwezesha vyote vilivyoleta maombi ili vikamilishe vigezo vinavyohitajika kunufaika na mikopo hii nafuu. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wajasiriamali wengine ndani ya Manispaa ya Ilala kuja kuomba uwezeshaji huu ili wakuze biashara zao,” amesema Mnganga.

Katika vikundi 120 vilivyojitokeza, Mnganga amesema 75 ni vya wanawake, 43 vya vijana na viwili ni vya watu wenye ulemavu. Kuhusu vikundi  vilivyokidhi vigezo, amesema 13 vya vijana, vimeomba jumla ya Sh532 milioni huku vikundi 11 vya wanawake vikihitaji Sh198 milioni na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu Sh5 milioni.

Taasisi ya CRDB Bank Foundation imeahidi kuendelea kushirikiana na maofisa maendeleo wa Manispaa ya Ilala pamoja na viongozi wa vikundi husika kuwasaidia wanachama wao kurekebisha kasoro zilizopo ili wote wenye nia njema wanufaike na mikopo hiyo.

“Jambo muhimu kulizingatia muda wote ni kurejesha fedha hizi kwa wakati. Wote mtakaopewa mikopo hii msisahau kuirejesha kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatoa nafasi kwa wengine nao kukopa,” amesisitiza Mnganga.

Related Posts