Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetoa ufafanuzi kuhusu mwelekeo wa mpango wa bima ya afya kwa wote, ukibainisha kuwa gharama kwa kaya moja yenye watu sita itakuwa Sh150,000 kwa mwaka, sawa na Sh25,000 kwa kila mwanakaya.
Kifurushi hicho chenye jumla ya huduma 277, kitamuwezesha kiongozi wa kaya kulipa kwa mkupuo au kupitia kampuni za simu, kwa kuanza na malipo ya awali ya Sh14,000, kisha mtumiaji atakatwa kiasi kidogo kidogo hadi kukamilisha jumla ya Sh150,000.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi, baada ya kuwasilisha mada kuhusu mwelekeo wa bima ya afya kwa wote kwenye kongamano la kitaifa la tiba, lililofanyika wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), jijini Arusha.
Dk Isaka amesema katika utekelezaji wa mpango huo, NHIF itashirikiana na kampuni za simu, benki, pamoja na mawakala, ambao pia watashiriki kwenye usajili wa wanufaika.
“Mawakala watakuwa na nembo ya NHIF ya usajili, watasambaa nchi nzima na watashirikiana nasi kusajili wanufaika, pamoja na madalali wa bima na mabenki,” amefafanua Dk Isaka.
Aidha, amesema kifurushi cha ‘Tarangile’ kitakuwa Sh168,000, kikiwalenga wananchi wenye uwezo wa kumudu gharama hizo, wakiwamo wa sekta rasmi na isiyo rasmi.
“Lakini pia kuna kifurushi cha bima kwa wote kwa kaya masikini, chenye huduma 277, ambacho kitaanza kutumika kwa gharama ya Sh150,000 kwa kaya ya watu sita, sawa na Sh25,000 kwa kila mtu kwa mwaka. Hii ni gharama nafuu ukilinganisha na gharama halisi ya bima,” amesisitiza Dk Isaka.
Amefafanua zaidi kuwa kifurushi cha ‘Tarangile’ kimeanzishwa kwa lengo la kuwavutia wananchi, kwa kuruhusu uchangiaji wa Sh14,000 kila mwezi.
“Unaweza kwenda katika kampuni ya simu ukasajiliwa, kisha ukaanza kukatwa kidogo kidogo hadi utakapokamilisha malipo na kuanza kupata bima,” amesema mkurugenzi huyo.
Amesema mchakato huo unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo mifuko mingine inayotoa huduma ya bima, huku wastaafu wanaotoka kwenye mifuko ya NSSF, PSSSF na mingineyo, wakiendelea kupata bima ya afya kupitia NHIF.
Dk Isaka amesema bima ya afya kwa wote ambayo kanuni zake tayari zimekamilika, itakuwa na makundi matatu. Ya kwanza ni kwa kaya maskini zisizochangia, ambazo zitafidiwa na Serikali.
“Kwa mujibu wa sensa, kuna kaya zipatazo 3,600,000, ambapo awamu ya kwanza tunatarajia kuanza na kaya 1,200,000 ambazo zimehakikiwa na Tasaf kwa kushirikiana na Tamisemi. Hii ni kazi ya NHIF kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Tamisemi na Tasaf,” ameeleza.
Amefafanua zaidi kwamba kundi la pili ni kwa wanufaika wa sekta rasmi (umma na binafsi), mwajiriwa atachangia asilimia 3 na mwajiri asilimia 3, hivyo jumla kuwa asilimia 6.
Kundi la tatu ni la hiari, likihusisha vifurushi vinavyotolewa na NHIF, Jubilee, Strategy, Assembly na mifuko mingine kama NSSF, kwa ajili ya sekta isiyo rasmi.
Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa NHIF inalipa watoa huduma kwa utaratibu wa ‘Fee for Service’, yaani wanatuma malipo baada ya kudhibitisha huduma iliyotolewa.
Lakini kwa bima ya afya kwa wote, Dk Isaka amesema mfumo utabadilika kuwa malipo kabla ya huduma.
Amesema vituo vitalipwa kabla ya kutoa huduma, kwa kuzingatia idadi ya wagonjwa na uzito wa maradhi wanayohudumia.
“Baada ya mahesabu hayo, kituo kitapewa fungu la fedha ambalo litatumika kwa kipindi kilichokubaliwa, kama ni miezi miwili au mitatu, kisha wanapokea malipo mapya,” amefafanua Dk Isaka.
Amesema bima ya afya kwa wote itakapoanza kutekelezwa, michango itakusanywa kwa mwaka mzima, lakini malipo kwa vituo yatatolewa kwa awamu badala ya mwaka mzima kwa wakati mmoja, ili kuruhusu ufuatiliaji mzuri.
Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na utekelezaji huo wa NHIF, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Tanzania (APHFTA), Dk Samwel Ogillo, amesema mfumo wa malipo ya kabla si mpya.
Amesema mfumo huo umekuwa ukitumiwa na wanachama wa NSSF na una manufaa kwa matibabu madogo madogo.
Hata hivyo, ameeleza changamoto zake kwa matibabu makubwa, hasa pale mtoa huduma anapopokea fedha na kuishiwa wakati wagonjwa bado wanahitaji matibabu.
“Jambo la muhimu ni kuboresha hesabu, kudhibiti mfumo wa rufaa na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bila kikwazo. Mfumo ukifika kwetu, tutatoa maoni yetu,” amesisitiza Dk Ogillo.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amesisitiza kuwa madaktari wanatamani wananchi wote washiriki kuchangia kwenye mfuko huo, kwa sababu bila kufanya hivyo, matokeo bora hayatafikiwa.
“Tunapaswa kuwahamasisha wananchi kujiunga. Kiwango kilichowekwa ni kidogo ukilinganisha na nchi nyingine. Rwanda na Zimbabwe wanatoza Dola 20 (takribani Sh53,117), wakati hapa ni nafuu zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa ni muhimu kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kuchangia, kutumia mifumo nafuu ya ulipaji na kubuni vyanzo vipya kama kodi kwenye vinywaji vyenye sukari, vilevi na madini.
“Pia ni muhimu kufanya utafiti wa kiuchumi kubaini kila Mtanzania anahitaji kiasi gani kwa mwaka ili kupata huduma bora za afya, kisha kuweka utaratibu wa kila mmoja kuchangia kwa wakati. Pia ni muhimu kuwa na sera thabiti ya kuulinda mfuko huu, ili kudhibiti mtikisiko wowote unaoweza kusababisha watu kukosa huduma,” amesisitiza Dk Nkoronko.
Kuhusu Tehama, Dk Isaka amesema NHIF imeboresha mifumo yake kwa kiwango kikubwa. Amesema awali, wanachama walilazimika kwenda kwenye ofisi za NHIF kujisajili, lakini sasa wanaweza kujisajili kwa kutumia simu.
Amesema hata ukusanyaji wa michango nao umeboreshwa na sasa unafanyika moja kwa moja kupitia mifumo ya kidijitali na mchakato wa malipo ya madai umehamia mtandaoni.
Amesema awali, daktari mmoja alichakata fomu 800 kwa siku, lakini kwa kutumia mfumo mpya anatumia dakika 45 hadi saa moja pekee.
“Tulichukua siku 90 mpaka 100 kulipa madai, lakini sasa tunalipa ndani ya siku 55, wakati sheria inatutaka tulipe ndani ya siku 60. Lengo letu ni kufika siku 45,” amesema.
Amefafanua zaidi kuwa mfumo mpya unapunguza mzigo kwa madaktari, unarahisisha ulipaji wa madai, na una uwezo wa kubaini mapungufu au udanganyifu.