Dodoma. Katika juhudi za kuishika mkono elimu ya Tanzania kupitia Teknolojia ya Habari na Masiliano (Tehama), shule 30 za sekondari jijini Dodoma zimenufaika na vifaa vya intaneti ya bure yenye kasi.
Vifaa hivyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya kidijitali vimetolewa na Kampuni ya Airtel Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kupitia mradi wa kijamii wa Airtel SmartWASOMI.
Vifaa hivyo vitawawezesha walimu na wanafunzi kupata huduma ya intaneti bure, ili kujisomea bure kupitia Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)na majukwaa ya elimu.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Mtemi Mazengo, mwishoni mwa wiki mkoani Dodoma, Meneja wa Kanda ya Airtel Tanzania Dodoma, Salum Ngururu amesema SmartWASOMI siyo tu mtandao, bali ni mfumo wa kidijitali unaoleta vifaa, maudhui ya kielimu yanayolingana na mtaala, na jukwaa la usomaji na ufundishaji wa kisasa.
“Mpango huu unaunga mkono jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano katika kutumia teknolojia ya mawasiliano kwenye sekta ya elimu,” amesema meneja huyo.

Grace Samwel akizungumza wa niaba ya Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, ameishukuru Airtel akisema:“Shule zetu sasa zinaweza kusoma kidijitali kwenye Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu au kupata maudhui kutoka maktaba mtandao ya Shule Direct bila gharama ya bando.”
“Tunawashukuru Airtel kwa kuwezesha elimu ya kidijitali kufika hadi kwa wanafunzi wetu bila gharama yoyote,” amesema.
Mwalimu Florian Kashasila amesema:“Vifaa vya intaneti ya kasi ya Airtel tulivyopatiwa leo vitasaidia sana walimu na wanafunzi kupata nyenzo za kufundishia na kujifunzia, ambazo awali hazikupatikana kirahisi shuleni.”
Kwa mujibu wa Airtel, mradi wa Airtel SmartWASOMI tayari umeshatekelezwa katika mikoa ya Zanzibar, Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mbeya na sasa Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuunganisha shule 3,000 nchini kwa kushirikiana na Serikali na Unicef.
Imeeleza kuwa, dhamira yake ni kuendelea kuwa sehemu ya mabadiliko ya elimu nchini kwa kuhakikisha shule haziachwi nyuma katika safari ya ujumuishaji wa kidijitali.