Njombe. Mkazi wa Mji wa Njombe, Yokebeti Sindila (29), ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kwenye paji la uso, eneo la Mnarani, Mtaa wa Mji Mwema, Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Juni 22, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Kamanda Banga amesema Sindila alikuwa kondakta wa mabasi ya Kampuni ya Kalubandika, yanayofanya safari zake kutoka mkoani Njombe kwenda maeneo mbalimbali nchini.
Amesema tukio hilo lilitokea Juni 20, 2025, saa nne usiku, eneo la Mnarani, Mtaa wa Mji Mwema akidaiwa kushambuliwa kwa kupigwa na kitu kizito kwenye paji la uso.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hili na tunawaomba wananchi wenye taarifa zozote kuhusu tukio au wahusika watoe ushirikiano ili kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kamanda Banga.
Ametoa wito kwa watuhumiwa kuacha kutenda vitendo hivyo wakidhani wapo salama, akibainisha jeshi hilo linaendelea na doria kali ili kuhakikisha Mkoa wa Njombe unabaki salama.
Mkazi wa Njombe, Alfred Mgimwa amesema hata kama marehemu alikuwa amekosea, adhabu ya kifo si suluhisho.
“Hata kama kulikuwa na ugomvi, njia sahihi ni mazungumzo yanayoweza kuleta muafaka,” amesema Mgimwa.
Naye Prisca Chaula ameliomba Jeshi la Polisi kuongeza doria kwenye maeneo mbalimbali mkoani Njombe, akibainisha kuwepo kwa viashiria vya matukio ya watu kupigwa na nondo usiku.
“Kumekuwa na taarifa kwamba, wakati wa usiku kuna watu wanapigwa na nondo, hali hii inatutia hofu. Nadhani polisi wanapaswa kuongeza doria kudhibiti matukio haya,” amesema Chaula.