Matukio ya ukatili yazidi kukithiri Zanzibar

Unguja. Idadi ya matukio ya ukatili na udhalilishaji imeongezeka kwa asilimia 4.9, kutoka matukio 102 yaliyoripotiwa Aprili, 2025 hadi kufikia matukio 107 Mei mwaka huu, kisiwani hapa.

Akitoa takwimu za matukio hayo leo Jumapili, Juni 22, 2025, Mtakwimu Ahmada Hassan Suleiman kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amesema miongoni mwa matukio hayo, waathirika wengi walikuwa watoto, sawa na asilimia 88.8, wakifuatiwa na wanawake kwa asilimia 9.3 na wanaume asilimia 1.9.

“Idadi ya matukio kwa mwezi imeongezeka kwa asilimia 4.9, kutoka matukio 102 yaliyoripotiwa Aprili 2025 hadi kufikia matukio 107 ya Mei 2025. Hata hivyo, matukio ya kubaka, shambulio la aibu au kukashifu, pamoja na kutupa watoto, yamepungua katika kipindi hicho,” amesema Ahmada.

Hata hivyo, amesema idadi ya matukio kwa mwaka imepungua kwa asilimia 37.8, kutoka matukio 172 yaliyoripotiwa wakati kama huu mwaka 2024, hadi matukio 107 Mei 2025.

Ahmada amesema matukio ambayo yameongezeka zaidi ni yale ya kulawiti, kunajisi, pamoja na shambulio la aibu au kukashifu.

Wilaya ya Magharibi A imeongoza kwa kuwa na matukio mengi zaidi, ikiwa na matukio 23 sawa na asilimia 21.5, ikifuatiwa na Magharibi B yenye matukio 22 sawa na asilimia 20.6.

Wilaya za Chakechake na Mkoani zimeripoti matukio machache zaidi, kila moja ikiwa na matukio mawili pekee, sawa na asilimia 1.9.

“Wilaya ya Magharibi B imeongoza kwa matukio ya kubaka, ikiwa na matukio 14 sawa na asilimia 20.6 kati ya matukio yote ya kubaka yaliyoripotiwa,” amesema Ahmada.

Kati ya matukio 68 ya kubaka yaliyoripotiwa Mei 2025, matukio 62 sawa na asilimia 91.2 yamewahusisha wasichana, wakati matukio sita sawa na asilimia 8.8 yamewahusisha wanawake.

Amefafanua kuwa matukio 93 kati ya 107 yaliyoripotiwa yapo chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi, sawa na asilimia 86.9, wakati matukio 11 yamepewa hati ya mashtaka (asilimia 10.3), na matukio matatu yapo mahakamani (asilimia 2.8).

Hassan Ali, kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar amesema jamii inapaswa kubadilisha mtazamo wake kuhusu masuala ya ukatili na udhalilishaji, kwa kuwa vitendo hivyo vinaharibu heshima ya jamii.

Ofisa kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Farid Ali Muhamed amesema wizara hiyo imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa wanafunzi ili kutokomeza ukatili na udhalilishaji.

Akizungumzia hayo, Abdulikarim Said Abdalla kutoka Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, amesema wanaendelea kutoa elimu kwa walimu wa madrasa kuhusu masuala ya ukatili na udhalilishaji, sambamba na kutoa leseni maalumu  kwa walimu hao kabla ya kuruhusiwa kufundisha.

Related Posts