Moussa Camara kipa bora 2024/25

Nyota wa Simba, Moussa Camara ameibuka kipa bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, baada ya kufikisha ‘Clean Sheets’ 19, ikiwa ni msimu wake wa kwanza hapa nchini tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Horoya AC ya kwao Guinea.

Camara ameibuka kipa bora baada ya mshindani wake mkubwa, Djigui Diarra wa Yanga kukosekana katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, kufuatia kucheza nyota wenzake, Aboutwalib Mshery.

Diarra amekosa tuzo hiyo kwa msimu wa pili mfululizo baada ya msimu uliopita wa 2023-2024, kumaliza na ‘Clean Sheets’ 14, akizidiwa ujanja na aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Mkongomani Ley Matampi aliyeibuka kidedea kwa kufikisha 15.

Matampi aliyejiunga na Coastal Union Aug 31, 2023, akitokea Jeunesse Sportive Groupe Bazano ya kwao DR Congo, aliondoka Desemba 10, 2024, kwa makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba wake na kikosi hicho, uliokuwa unaisha msimu huu.

PRISONS, FOUNTAIN KUCHEZA PLAY-OFF

Timu za maafande wa Tanzania Prisons na Fountain Gate, zimemaliza msimu huu kwa vichapo na kuzifanya kuangukia ‘Play-Off’, ili kusaka nafasi ya kusalia Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku zikitarajiwa kucheza mechi ya kwanza Juni 25, 2025.

Prisons iliyotoka kuchapwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga nyumbani, ilijikuta ikimaliza msimu huu kwa kutoka sare ya mabao 3-3, ikicheza ugenini na Singida Black Stars, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti mjini Singida.

Mabao ya Singida yamefungwa na Serge Pokou dakika ya 43 na Marouf Tchakei dakika ya 45 na Jonathan Sowah dakika ya 47, huku ya Prisons yakifungwa na Ismail Ally dakika ya 63 na 76 kwa penalti, kabla ya Mussa kupachika la tatu dakika ya 84.

Matokeo hayo yameifanya Prisons kumaliza msimu nafasi ya 13 na pointi 31, baada ya kushinda mechi nane tu, sare saba na kupoteza 15.

Kwa upande wa Fountain ikiwa kwenye Uwanja wa Tanzanite kwaraa uliopo mjini Babati, Manyara, ilichapwa mabao 3-2, dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC hivyo, kuifanya kumaliza msimu huu ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 29.

Mabao ya matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam, yamefungwa na Zidane Sereri dakika ya 3, huku Jackson Shiga akijifunga dakika ya 23, kabla ya Fountain Gate kupata bao la kufutia machozi kwa penalti lililofungwa na Elie Mokono dakika ya 45.

Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliihakikishia Azam FC ushindi ugenini baada ya kupachika bao la tatu dakika ya 90 kwa penalti na kumaliza msimu ikiwa nafasi ya tatu na pointi 63, nyuma ya Simba iliyo ya pili na pointi 78 na vinara Yanga yenye 79.

Kitendo cha Prisons na Fountain kumaliza nafasi ya 13 na 14, kimezifanya timu hizo kucheza ‘Play-Off’ ili kubakia Ligi Kuu Bara, ambapo mechi ya kwanza itapigwa Juni 25, 2025, huku ile yaa marudiano ikitarajiwa kupigwa tena Juni 29, 2025.

Mshindi wa jumla baina ya timu hizo atasalia Ligi Kuu msimu ujao, huku itakayopoteza itaenda kujiuliza tena kwa kucheza ‘Play-Off’ na Stand United ‘Chama la Wana’ ya Championship, iliyofika hapo kwa kuitoa Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2.

KARIAKOO DERBY KUAMUA BINGWA

Kitendo cha Yanga na Simba kushinda mechi zake za raundi ya 29, kimezifanya kusubiria hadi Jumatano ya Juni 25, wakati wa pambano la ‘Kariakoo Derby’, litakapopigwa ili kupata bingwa mpya wa Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025.

Simba ikiwa kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Steven Mukwala dakika ya 17 na kukifanya kikosi hicho kushika nafasi ya pili baada ya kumaliza na pointi 78.

Kwa upande wa Yanga inayosaka ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo, ikicheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, iliendeleza wimbi la vichapo baada ya kuibuka tena na ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya Dodoma Jiji.

Mabao ya Yanga yamefungwa na Clatous Chama dakika ya 4, Duke Abuya dakika ya 50 na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ dakika ya 61, huku Joash Onyango akijifunga la nne kisha Maxi Mpia Nzengeli kuongeza la tano na kushinda mabao 10 katika mechi mbili.

Ushindi kwa Yanga umeifanya kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kufikisha pointi 79, pungufu ya moja tu na Simba yenye 78.

Kwa maana hiyo, pambano la ‘Kariakoo Derby’ ndilo litakaloamsha hisia za mashabiki wengi wa soka ndani na nje ya nchi kwani Yanga inahitaji ushindi au sare ili itwae ubingwa huo, huku kwa upande wa Simba ikihitaji ushindi tu ili ichukue taji.

Kwenye Uwanja wa Majaliwa, mwenyeji Namungo FC iliibuka na ushindi wa mabao 5-0, dhidi ya kikosi cha KenGold ambacho tayari kimeshuka daraja, kwa mabao yaliyofungwa na Meddie Kagere ‘MK14’ aliyefunga mawili dakika ya 7 na ile ya 29.

Mabao mengine yamefungwa na Hassan Kabunda dakika ya 41, Erasto Nyoni dakika ya 45 na Salehe Karabaka dakika ya 90, huku kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wenyeji, Coastal Union ililazimishwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Tabora United.

Emmanuel Mwanengo aliifungia Tabora United bao dakika ya 53, kabla ya Coastal Union kusawazisha dakika ya 90 kupitia kwa Lucas Kikoti kwa mkwaju wa penalti, huku kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Mashujaa FC ilitoka suluhu na JKT Tanzania.

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Pamba Jiji ilitoka sare ya bao 1-1, dhidi ya KMC, ambapo bao la wenyeji lilifungwa na Mkenya Mathew Momanyi dakika ya 34, kisha kikosi cha Kinondoni kikachomoa kupitia kwa Redemtus Mussa dakika ya 84.

Related Posts