Dar es Salaam. Timu ya madaktari bingwa wa upasuaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya imefanikiwa kufanya upasuaji wa kipekee kwa mtoto mchanga mwenye umri wa siku 15, aliyezaliwa na baadhi ya viungo vya ziada.
Upasuaji huo uliofanyika Juni 20, 2025 ulihusisha viungo hivyo kwa kitaalamu ‘polymelia’ vilivyounganika katika sehemu ya mgongo ya mtoto huyo ukiwemo mguu wa ziada, sehemu ya siri na sehemu ya utumbo uliojitenga.
Kiongozi wa timu hiyo, Daktari bingwa bobezi wa upasuaji wa watoto, Lazaro Mboma amesema viungo hivyo vya ziada vinaweza kusababisha changamoto kubwa katika utendaji kazi wa mwili, ikiwa ni pamoja na ugumu wa kutembea, kufanya kazi za kila siku, maumivu na kuathiri ubora wa maisha yake.
Dk Mboma ametaja athari nyingine kuwa inaweza kusababisha sintofahamu kijamii ikiwemo pia changamoto ya kisaikolojia kwa mtoto na familia yake.
“Upasuaji huu ni mchakato mgumu ambao unahitaji ujuzi wa hali ya juu na umakini mkubwa uliotumia takriban saa moja na dakika kumi, na umefanyika kwa mafanikio makubwa bila kuathiri afya ya viungo vingine na hali ya mtoto huyu inaendelea vizuri,” amesema Dk Mboma.
Ameeleza kuwa upasuaji huo ni hatua kubwa kwa huduma za afya za Mkoa wa Mbeya, na wataendelea kutoa huduma zaidi za kibingwa bobezi kwa watoto na wagonjwa wengine.
Wakati huohuo, familia ya mtoto aliyefanyiwa upasuaji imeelezea furaha yao na kuishukuru timu ya madaktari na watoa huduma wote hospitalini hapo, kwa jitihada zao za kuhakikisha mtoto wao anapatiwa matibabu bora na salama.
“Natoa shukurani zetu za dhati kwa timu ya madaktari na wauguzi kwa msaada wao katika matibabu ya mwanangu. Kwa sasa mtoto wetu anaendelea na matibabu na afya yake inaendelea kuimarika,” amesema Lina Kasanya mama wa mtoto huyo.