‘Ofisa wa polisi’ apewa ruksa kumshitaki IGP, RC Kagera

Bukoba. Mahakama Kuu imempa aliyekuwa ofisa wa Jeshi la Polisi nchini, Ally Hassan Muhamad, kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama dhidi ya mabosi wake wawili, kupinga kufukuzwa kazi jeshini Novemba, mwaka 2022.

Muhamad, aliyekuwa kachero mwenye cheo cha Sajini na namba za polisi G.7696, amepewa kibali cha kufungua maombi hayo dhidi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera (RPC), Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uamuzi huo umetolewa Juni 18, 2025, na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Immaculata Banzi, wakati akitoa uamuzi katika maombi namba 4053 ya 2025 ya kupatiwa kibali ili afungue maombi ya mapitio ya mahakama.

Katika uamuzi wake uliowekwa kwenye tovuti ya mahakama Juni 20, 2025, Jaji Banzi alisema baada ya kupitia hoja za pande mbili, ameona maombi hayo ya kibali yana msingi na ametoa siku 21 kwa muombaji kuyawasilisha.

Kwanini anataka kumshitaki IGP

Katika kiapo chake, Muhamad anakusudia kupinga uamuzi wa RPC Bukoba na IGP wa kumfuta kazi akidai walichukua uamuzi huo bila kufuata taratibu. Ataomba mahakama itoe amri IGP amrejeshe kazini na kumlipa stahiki zake.

Kulingana na maelezo yake, ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi alieleza kuwa Oktoba 5, 2020, akiwa amepangwa kituo cha Polisi Kyaka, alikamatwa kwa tuhuma za kupokea rushwa, lakini baada ya kukaa siku kadhaa mahabusu, aliachiwa huru.

Anasema baada ya kuachiwa aliambiwa aendelee na majukumu yake kama kawaida kwa kuwa hakuwa na kesi ya kujibu na aliendelea na kazi hadi Oktoba 2021 alipozuiwa kujiunga na kozi kwa tuhuma zilezile zilizomkabili mwaka 2020.

Baada ya kufuatilia na kufanya uchunguzi, RPC Kagera alimfahamisha kuwa shauri lake la kinidhamu lipo tayari kusikilizwa.

Anadai kuwa Novemba 11, 2022, alishangaa kupokea taarifa kuwa amefukuzwa kazi. Alipoomba nakala ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya kijeshi iliyomhukumu, RPC Kagera alikataa kumpa nyaraka hizo.

Novemba 14, 2022, aliwasilisha rufaa kwa IGP na kusubiri hadi Novemba 5, 2024, ambapo alijulishwa kufika kupokea uamuzi. Hata hivyo, alipoomba nakala ya uamuzi na mwenendo wa rufaa hiyo, jitihada zake hazikfanikiwa.

Kwa mujibu wa Muhamad, ana haki ya kupewa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kwa kuwa uchunguzi wa awali wa tuhuma dhidi yake haukufanyika.

Pia anadai mahakama ya kijeshi iliyomsikiliza haikuwa na muundo sahihi, alinyimwa hati ya mashtaka baada ya kufanyiwa marekebisho, na pia hakupata nakala za mwenendo na uamuzi.

Mbali na hayo, anadai uamuzi dhidi yake ulikuwa wa upendeleo kwani hakukuwa na mwendesha mashtaka huru, huku kamishna aliyesikiliza kesi hiyo akifanya majukumu yake akiwa katika “kofia mbili”.

Muhamad alieleza kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa kanuni ya msingi ya asili ya haki ya kusikilizwa, hivyo akaomba mahakama impe kibali ili afungue maombi ya mapitio.

Majibu ya IGP,  RPC Kagera

Katika majibu yao kupitia kiapo kinzani cha Inspekta Emmanuel Mavere, wajibu maombi walipinga madai ya Muhamad wakisema kufutwa kwake kazi kulikuwa halali kisheria na kulifanywa kwa kuzingatia taratibu.

Kwa mujibu wa Inspekta Mavere, uchunguzi wa awali ulifanyika kwa lengo la kuchunguza masuala ya kinidhamu na kijinai. Hata hivyo, alieleza kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka ya jinai.

Alisema mwenendo wa shauri la nidhamu ulisitishwa kwa muda ili kumwezesha kuhudhuria kozi ya cheo cha Sajini.

Baadaye, ofisa huyo alishtakiwa na alipewa haki ya kusikilizwa mbele ya ofisa mwandamizi aliyeteuliwa kwa mujibu wa Kanuni za Polisi (PGO) za mwaka 1995.

Wajibu maombi walikanusha kupokea barua yoyote ya maombi ya nyaraka, ikiwamo hati ya mashtaka na mwenendo wa uamuzi, na walisema uamuzi huo ulikuwa wa haki dhidi ya ofisa huyo.

Walisisitiza kuwa muombaji alipatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na kwamba hajajenga msingi wa kutosha kuhalalisha kupewa kibali hicho.

Katika shauri hilo, Muhamad aliwakilishwa na Wakili Derick Zephurine, huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Victor Mhana. Wote walikubaliana shauri hilo lisikilizwe kwa njia ya maandishi.

Uamuzi wa Jaji ulivyokuwa

Jaji Banzi alisema hoja kuu ilikuwa kama mleta maombi amekidhi vigezo vya kupewa kibali cha kufungua maombi hayo.

Kabla ya kushughulikia hoja hiyo, Jaji alisema ni muhimu kutoa maoni yake kuhusiana na suala lililoibuliwa na wakili wa Serikali kuwa maombi hayo ni batili kwa kutoambatanisha mwenendo na uamuzi ambao ndio msingi wa maombi.

Hata hivyo, Jaji alisema Kanuni ya 5(2) inamtaka muombaji ataje jina lake, unafuu anaoomba, sababu za maombi na aambatanishe kiapo, na kwamba Muhamad alitimiza matakwa hayo.

Jaji alisema, kulingana na hati ya kiapo cha mleta maombi, Novemba 11, 2022, alifukuzwa kazi jeshini, na siku mbili baada ya uamuzi huo, akakata rufaa ambayo ilikaa hadi Oktoba 28, 2024, ilipotolewa na kumfikia muombaji Novemba 5, 2024.

Kulingana na kumbukumbu za mahakama, Jaji alisema maombi hayo yalifunguliwa kwa njia ya mtandao Februari 21, 2025, na kwa msingi huo, maombi hayo yalifunguliwa ndani ya muda wa miezi sita kama sheria na kanuni zinavyoelekeza.

“Kuhusu kama mleta maombi amekidhi vigezo vya kisheria, ni wazi kupitia kiapo chake, alikuwa ni ofisa wa Polisi akifanya kazi katika vituo mbalimbali hadi mwaka 2022 alipofutwa kazi kutoka utumishi wa Jeshi la Polisi,” alisema Jaji Banzi.

“Rufaa yake kwa mjibu maombi wa pili (IGP) haikuzaa matunda. Mbali na hilo, ameibua masuala kadhaa, ikiwamo kunyimwa haki ya kusikilizwa katika hatua ya usikilizwaji wa suala lenyewe hadi hatua ya rufaa,” aliongeza kusema Jaji Banzi.

Jaji alisema ni jambo lililo wazi kuwa haki ya kusikilizwa ni takwa la kikatiba, na kwamba hoja kama alisikilizwa au la, kulingana na kanuni za Polisi, haiwezi kuhitimishwa katika hatua hiyo ya kutoa kibali cha kufungua maombi hayo.

“Itoshe tu kusema kuwa mleta maombi ameweza kujenga msingi wa shauri lake, ambalo linaweza kusikilizwa na mahakama, na ninatoa kibali cha yeye kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kupinga uamuzi anaoulalamikia,” alieleza.

Jaji alisema ajira ya mleta maombi iko njia panda, na kwa msingi huo, anatoa kibali kwa mleta maombi kufungua maombi hayo ndani ya siku 21 tangu uamuzi huo ulipotolewa, na kwa mazingira ya shauri lilivyo, kila upande utabeba gharama zake.

Related Posts