Uadilifu unavyotesa wanaume ndoa za mitala

Mwanza. Mitala au ukewenza ni mfumo wa ndoa ambapo mwanaume anaoa wake zaidi ya mmoja.

Ingawa mfumo huu umezoeleka katika baadhi ya jamii hasa za Kiafrika, bado unaibua mijadala mikali kuhusu haki, usawa, na ustawi wa familia.

Changamoto kubwa inayojitokeza katika ndoa ya ukewenza ni utekelezaji wa uadilifu kati ya wake.

 Kwa maana ya msingi, uadilifu ni hali ya kutenda haki bila upendeleo au ubaguzi. Katika mfumo huu wa ndoa, mara nyingi uadilifu unakuwa tatizo kubwa linalosababisha migogoro ya kifamilia, matatizo ya kisaikolojia, mmomonyoko wa maadili, na hata matatizo ya kisheria.

Makala hii inachambua kwa kina changamoto ya uadilifu katika ndoa ya ukewenza kwa kuzingatia mitazamo ya kijamii, kimaadili, kisaikolojia,  kisheria na kidini.

“Nilikuwa naishi na mume wangu kwa amani, hadi alipooa mke wa pili amani ya nyumba ndipo ikaanza kuyumba..nikawa naonekana sijui kufanya kila kitu,”anasimulia Hawa Abdallah, mkazi wa jijini Mwanza.

Hawa ambaye awali aliishi na familia yake mkoani Tabora, anasema baada ya mume wake(jina limehifadhiwa) kuoa mke wa pili, hali ya amani ndani ya nyumba ilibadilika ambapo aliishia kudharauliwa, kutukanwa na kunyanyaswa na mume wake huyo.

Anasema ilifikia hatua, hadi rangi yake nyeusi ilikuwa kero kwa mume wake ambaye hatimaye alihamia kwa mke mdogo,  aliyedai kuwa rangi yake nyeupe inaangaza nyumba.

“Alifikia hatua akanitelekeza akahamia kwa mke wake mdogo ambaye alikuwa mweupe. Mimi akawa ananiita giza, akaenda kwa mwanamke mweupe ambaye alikuwa anasema ni mwanga wa nyumba,”anasema Hawa.


Anasema manyanyaso yalivyozidi aliamua kuachika kwakuwa vitendo vya mume wake vilikuwa kama kafanyiwa mambo ya kishirikina,  kwakuwa hakusikiliza neno la mtu mwingine yeyote zaidi ya mke wake mdogo.

“Niliamua kurudi kwetu, baadaye nikaenda kuishi kwa kaka yangu hukohuko Tabora, ndipo mdogo wangu aliyekuwa akiishi Mwanza akaniita nije niishi naye..hadi leo nipo hapa, sina ndoa na sikutaka kuolewa tena,”anaeleza.

Katika jamii nyingi za Kiafrika, ukewenza umechukuliwa kama ishara ya heshima, uwezo wa kifedha, au uanaume.

Hata hivyo, taswira hii inazidi kubadilika kadri jamii zinavyoendelea na kupokea usawa wa kijinsia kama sehemu ya maendeleo ya kijamii.

Uhalisia unaonyesha kwamba ndoa ya ukewenza huathiri mshikamano wa kifamilia. Pale ambapo uadilifu hukosekana, wake huanza kushindana, wivu huzuka na familia kugawanyika.

Watoto wanaozaliwa katika familia za ukewenza hukua katika mazingira yenye migogoro ya mara kwa mara. Wake hujaribu kuwapendelea watoto wao kwa matumaini ya kupata nafasi kubwa kwa mume. Matokeo yake ni kutokea kwa makundi  ndani ya familia ambayo hudhoofisha mshikamano wa kifamilia na kuvuruga malezi ya watoto. Hali hii huathiri hata uhusiano wa kijamii kati ya familia na jamii inayowazunguka.

Kiini cha maadili katika ndoa yoyote ni usawa, heshima na uaminifu. Katika ndoa ya wake wengi, maadili haya huwekwa shakani hasa pale ambapo mwanaume hushindwa kugawa mapenzi, muda, au mali kwa usawa. Upendeleo unaotokana na mapenzi ya moyoni au maslahi binafsi, huvunja maadili ya ndoa.

Kwa mfano, mume anaweza kumpendelea mke mdogo kwa sababu ya umri au mvuto wa kimwili, na kumdharau mke wa kwanza au wengine.

Hii huibua hisia za kutothaminiwa kwa wake waliodharauliwa, jambo linalokinzana na maadili ya utu na heshima ya mtu.

Wakati mwingine wake walioachwa nyuma hujikuta wakijihusisha na vitendo visivyofaa kwa lengo la kulinda heshima yao au kujipatia faraja, na hii inaweza kuchochea mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii.

Ukosefu wa uadilifu katika ndoa ya wake wengi huleta madhara makubwa ya kisaikolojia kwa wake, mume na hata watoto.

Mke anayehisi kutengwa au kupuuzwa hujawa na huzuni, msongo wa mawazo,  hasira zisizodhibitika, au hata chuki dhidi ya wake wenzake. Mabadiliko haya ya kihisia yanaweza kumfanya kuwa na matatizo ya kiafya au tabia zisizo za kawaida.

Kwa upande mwingine, mwanaume pia huweza kuathirika kisaikolojia hasa pale anapojikuta akishindwa kutatua migogoro kati ya wake zake au kubeba mzigo wa kifedha kwa familia kubwa. Wanaume wengi huingia katika ukewenza wakiwa na taswira ya kimapokeo bila kutathmini hali yao ya kisaikolojia na uwezo wa kusimamia hisia za wake zaidi ya mmoja.

Watoto wanaoishi katika mazingira haya nao huathirika. Wanaweza kukua wakiwa na hofu, kukosa kujiamini, au hata kuwa na tabia za kikatili kutokana na mazingira ya ushindani, chuki na mivutano ya kila mara nyumbani.

Kisheria, ndoa ya ukewenza inaruhusiwa au kupigwa marufuku kutegemeana na nchi. Katika baadhi ya mataifa kama kwetu Tanzania,  Afrika Kusini, Kenya, na Nigeria, ukewenza umetambuliwa katika sheria za ndoa za kimila na kidini.


Hata hivyo, sheria hizi zimeweka masharti kadhaa kuhakikisha wake wote wanapewa haki zao sawa. Uislamu kwa mfano, umeweka masharti maalumu kwa mtu anayetaka kuingia kwenye ndoa ya mitala.

Licha ya kuwepo kwa sheria hizi, utekelezaji wake ni changamoto. Ni vigumu kuthibitisha kisheria kama mwanaume anatenda haki kwa wake wote, hasa katika mambo ya kihisia au mgawanyo wa muda.

Sheria nyingi hazina mifumo ya ufuatiliaji wa maisha ya ndani ya familia, hivyo ukosefu wa uadilifu mara nyingi hauwajibishwi kisheria isipokuwa pale mke mmoja atakapofungua kesi mahakamani, jambo ambalo ni gumu kwa wengi kwa sababu ya hofu, aibu au utegemezi wa kiuchumi.

Katika nchi nyingi za Magharibi, ukewenza ni kosa la jinai. Sheria za ndoa katika mataifa hayo zinaegemea zaidi kwenye usawa na haki za wanawake, na hivyo kutambua ndoa ya wake wengi kama ukiukaji wa maadili ya kijamii na haki za binadamu.

Kwa Tanzania Uislam ni moja ya dini kubwa inayoruhusu ndoa ya ukewenza. Ni muhimu kuitazama ndoa hii kwa mtazamo wa dini hiyo.

Shekh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa, anasema  Sheria ya kiislamu imetoa ruhusa ya mtu kuoa wake wanne, lakini hiyo ni ruhusa na sio wajibu huku ikiwa na masharti kadhaa.

‘’Kuoa mwanamke zaidi ya mmoja inategemeana na uwezo wako wewe mwanaume, kama una uwezo ambao utaweza kutosheleza kukutana nao, kuwapa matumizi, makazi na huduma mbalimbali kama hauna huo uwezo jambo hili siyo la lazima kwako wala siyo la wajibu, unatakiwa ubakie na mke wako mmoja tu ndiyo sawa,’’ anasema.

Anasema ili uwe na mke zaidi ya mmoja,  kuna mambo  lazima uyazingatie, ambayo ni haki na wajibu kwa wenza wote.

‘’Lazima uwe na uadilifu kwa maana lazima wapate haki sawa sawa usiwe unapendelea baadhi yao,’’ anaeleza.

Uadilifu katika muktadha wa ndoa ya ukewenza katika Uislamu,  ni pamoja na kutoa haki sawa kwa wake wote katika mambo kama malazi, matunzo ya kifedha, matumizi ya nyumbani, mavazi na mahitaji mengine ya msingi.

Pia inasisitizwa upendo na hisia.  Ingawa mapenzi ni jambo la ndani la moyo, mwanaume anatakiwa kujitahidi kutoonyesha upendeleo wa dhahiri. Aidha, kila mke ana haki ya kuwa na uhusiano wa karibu na mume wake bila ubaguzi.

Licha ya masharti haya  wazi kutoka kwa Qur’an na mafundisho ya Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie), utekelezaji wa uadilifu kwa wake wote ni changamoto kubwa.

Mara nyingi, wanaume wanaingia katika ndoa ya pili au zaidi bila maandalizi ya kisaikolojia, kiuchumi, au hata kijamii, hali ambayo huwafanya kushindwa kuwahudumia wake kwa usawa.

Uadilifu ni moyo wa haki, na katika ndoa ya ukewenza, ni changamoto kubwa inayovuruga msingi mzima wa familia na jamii.

Ingawa mfumo wa ukewenza umepewa nafasi katika baadhi ya jamii, utekelezaji wa uadilifu kwa wake wote ni jambo gumu ambalo mara nyingi linasababisha migogoro ya kifamilia, matatizo ya kisaikolojia, na madhara kwa watoto.

Mtazamo wa kijamii, kimaadili, kisaikolojia na kisheria unaonesha wazi kuwa bila uadilifu, ndoa ya wake wengi huwa mzigo badala ya baraka.

Kwa hivyo, kabla ya mtu kuamua kuingia katika mfumo huu wa ndoa, ni muhimu kutafakari kwa kina kuhusu uwezo wa kiakili, kisaikolojia, kifedha na kiadili katika kusimamia uhusiano wa wake zaidi ya mmoja. Vinginevyo, ndoa hiyo hugeuka kuwa chanzo cha mateso kwa wote waliohusika badala ya kuwa muunganiko wa upendo, heshima na amani.

Kiongozi wa kimila, Mtemi Domina Musiba wa Tatu kutoka Buchosa mkoani Mwanza, anasema  ni mazoea ndiyo yanayosababisha wanaume kushindwa uadilifu wa  ndoa za uke wenza.

Related Posts