Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha limethibitisha kuwashikilia watu wawili wanaotuhumiwa kwa makosa ya kimtandao ambao awali kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zilisambaa taarifa za kudaiwa kutekwa na wasiojulikana.
Taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa jana Jumamosi, Juni 21,2025 imewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jackson Kabalo (32) na Joseph Mrindoko (37) wajasiriamali na wakazi wa eneo la Maji ya Chai wilaya ya Arumeru walikamatwa kwa makosa ya matumizi mabaya mitandao.
“Katika baadhi ya mitandao ya kijamii kumekuwepo kwa taarifa ikieleza juu kukamatwa kwa watu wawili na watu wasiojulikana, ukweli ni kwamba Jeshi la Polisi Juni 20,2025 liliwakamata hao kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mitandao,” alisema.
Kupitia taarifa hiyo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo ilisema upelelezi wa tuhuma hizo unaendelea na utakapokamilika hatua za kisheria zitachukulia mara moja na kuwaonya waendeshaji wa mitandao ya kijamii kujiridhisha kabla ya kuchapisha taarifa zinazoweza kusababisha taharuki kwa jamii.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi aliandika kwenye mtandao wake wa X akilaani tukio hilo kwamba watu hao wawili walikamatwa na hawakuwa kwenye kituo cha Polisi Usa River walikodaiwa kupelekwa.
“Nimezungumza na kiongozi wa Chama cha Mawakili kanda ya Kaskazini, Wakili David Shillatu kufuatilia kwa haraka jambo hili kupitia viongozi wa ofisi ya Arusha,” ilieleza taarifa hiyo.
Mwabukusi aliongeza kuwa sanaa ni taaluma na ni njia ya kufikisha ujumbe na hatarajii kuchukuliwa kuwa kosa la jinai na hakuna sheria yeyote inayokataza wananchi kukosoa viongozi, kuwapenda au kumchukia mtu na kuwa huo ni utashi binafsi.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani mara moja au kuwapa haki yao ya dhamana iwapo wanatuhumiwa kwa kosa lolote na kuwapa haki ya kuwasiliana na ndugu au mawakili wao.