Askari waliomuua muuza madini wahukumiwa kunyongwa

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, imewahukumu kunyongwa hadi kufa maofisa wawili wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi (25), mkazi wa Kijiji cha Ruponda, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu, Juni 23, 2025 na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara chini ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Hamidu Mwanga.

Maofisa waliokutwa na hatia ni Mrakibu wa Polisi, Gilbert Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Mtwara na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Onyango, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa wakati wa shauri hilo, mauaji hayo yalifanyika Januari 5, 2022 katika Kituo cha Polisi cha Mitengo mkoani Mtwara, mfanyabiashara huyo alichomwa sindano yenye sumu.

Baada ya kuuawa, mwili wake ulichukuliwa na kutupwa kwenye Msitu wa Hiari uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Mahakama imejiridhisha kwamba washtakiwa hao namba moja na mbili, walihusika moja kwa moja katika tukio hilo, kutokana na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo.

Mauaji hayo yalitokana na marehemu enzi za uhai wake kudai fedha zake, Sh33,748,980, ambazo inadaiwa maofisa hao walizichukua wakati wakimfanyia upekuzi.

Kesi hiyo, yenye namba 15 ya mwaka 2023, ilisikilizwa na jopo la mawakili 17, tisa wa upande wa Jamhuri na wanane wa upande wa utetezi.

Mahakama hiyo pia imewaachia huru maofisa watano wa Jeshi hilo la Polisi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Walioachiwa huru ni Mrakibu wa Polisi Msaidizi Nicholaus Kisinza, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi John Msuya Mganga, Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mkoa wa Mtwara, Mkaguzi wa Polisi Msaidizi Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi Shirazi Mkupa, pamoja na Koplo Salimu Mbalu.

Related Posts