Dodoma. Bangi imeendelea kuwa tishio kati ya dawa kulevya ambazo zimekuwa zikikamatwa na Mamlaka ya Udhibiti wa dawa za kulevya.
Katika kipindi cha 2024, tani 2,307.37 zilikamatwa na kati ya hizo, tani 2,303.2 ni bangi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi ametoa takwimu hizo leo Jumatatu Juni 23, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mamlaka ya Dawa za Kulevya nchini kuwawasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa mwaka 2024.
Lukuvi amesema kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa ndani na nje ya nchi na jamii kwa ujumla, imepata mafanikio makubwa katika kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa hizo hatarishi.
Kwenye mafanikio hayo, dawa za kulevya aina ya skanka kilichokamatwa kimeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambayo ni ishara kuwa kumekuwa mafanikio makubwa.
Katika kipindi hicho mirungi ni dawa ya kulevya ya mashambani iliyokamatwa kwa kiasi cha tani 18.45, ambapo tani 1.7 za methamphetamine zilikamatwa, kilogramu 433.02 za heroin na gramu 853 za cocaine.

“Kwa mara ya kwanza, Serikali ilikamata kilogramu tano za dawa mpya ya kulevya inayojulikana kamamethylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV) ambayo ilikuwa ikiingizwa nchini,amesema Lukuvi.
Waziri amesema Serikali imeimarisha ufuatiliaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya ili zisichepushwe na kutumika kama mbadala au kutengeneza dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Waziri,mwaka 2024 kiasi cha kilogramu 19.2 na lita 22,682.4 za kemikali bashirifu,dawa tiba zenye asili ya kulevya kiasi cha kilogramu 56.78 na mililita 200 zilikamatwa.
Kwa kutumia mifumo ya Kieletroniki amesema Serikali kupitia mifumo ya kielektroniki ilifanikiwa kuzuia uingizwaji wa tani 29.6 na lita 125 za kemikali bashirifu.
Katika taarifa yake waziri amesema vituo 16 vilivyosajili kwa ajili ya waraibu ni 17,975. huku nyumba 62 za upataji nafuu (sober houses) ziliendelea kutoa huduma kwa waraibu 17,230.
Kamishna wa Mamlaka ya Kupambana na dawa za kulevya Areta Lyimo amesema mapambano amesema kwa sasa Mamlaka hiyo inaendelea kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa na wananchi na ndiyo chanzo cha kupata mafanikio hayo.
Lyimo amesema wanaendelea kuongoza mapambano hayo na hakuna mtu atakayesalia katika biashara hiyo.
Hata hivyo ameeleza kuwa watu wanaotunga nyimbo za kuhamasisha uvutaji au matumizi ya dawa hizo zimepigwa marufuku pamoja na wanaovaa nguo za kuhamasisha.
Kingine amesema wanaendelea kuzungumza na wasanii ili waache kabisa hamasa ya kutumia dawa hizo kwani Tanzania kwa sasa ni miongozi mwa nchi ambazo zinatajwa kuonyesha juhudu katika mapambano hayo.