Dar es Salaam. Kibano kingine kimewashukia wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), baada ya chama hicho kutangaza kusitisha matukio yanayowahusisha wajumbe wanaopiga kura za maoni.
Matukio yaliyotangazwa kusitishwa na chama hicho ni ziara, semina na makongamano yanayowahusisha wajumbe wa vikao vinavyowapigia kura za maoni wagombea.
Kibano hicho kinaongeza makali kwa wagombea kupitia chama hicho, baada ya kile cha awali kilichohusisha mabadiliko ya Katiba ya CCM ili kuongeza idadi ya wajumbe watakaopiga kura za maoni kwa watiania.
Hayo yote yanafanywa na chama hicho, ikiwa imesalia miezi michache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Tayari CCM imeshatangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji fomu za ubunge, udiwani na uwakilishi kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025.
Hata hivyo, ratiba hiyo ilitanguliwa na ya awali iliyoeleza kuwa uchukuaji na urejeshaji fomu ungeanza Mei 15, kabla ya baadaye mchakato huo kusogezwa mbele.
Taarifa kuhusu kibano hicho imetolewa leo, Jumatatu, Juni 23, 2025, ikitiwa saini na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi.
Kwa mujibu wa Nchimbi kupitia taarifa hiyo, kwa kuwa chama hicho kinatarajia kuanza michakato ya ndani ya kuwateua wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi, matukio hayo yote yamesitishwa.

Mchakato huo wa ndani ya CCM, amesema, utahusisha uchukuaji na urejeshaji wa fomu, vikao vya awamu ya kwanza vya uchujaji na uteuzi kwa ajili ya upigaji wa kura za maoni.
Vikao hivyo, Dk Nchimbi kupitia taarifa hiyo, amesema, vitafuatiwa na vikao vya uchujaji na uteuzi wa mwisho wa wagombea wa CCM kwa nafasi husika.
“Kwa kuzingatia hilo, CCM inasitisha mara moja ziara, mikutano, semina na makongamano yanayohusisha wajumbe wa vikao vinavyopigia kura za maoni wagombea kwa ngazi zote, mpaka baada ya kura za maoni,” amesema.
Amelisisitiza hilo akisema mwanachama yeyote anayetarajia kugombea, au wakala wake, wanapaswa kuepuka kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni kinyume cha katiba, kanuni na miongozo ya chama hicho.
Amewataka viongozi, watendaji na wanachama kuendelea kusimamia maadili na nidhamu ya chama hicho wakati wote wa maandalizi ya mchakato wa ndani na utekelezaji wa shughuli za uteuzi wa wagombea kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Ni wajibu wa kila mwanachama wa CCM kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, kwa kuzingatia dhamana na imani kubwa tuliyopewa na Watanzania,” amesema.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda, amesema kilichofanyika kinalenga kuweka uwanja sawa wa mapambano kati ya wabunge wanaotaka kugombea na wagombea wapya.
Amesema wabunge, madiwani na wawakilishi walikuwa na nafasi ya kuendelea kukutana na wajumbe hao kupitia vikao mbalimbali, lakini tangazo la chama hicho linazuia rasmi.
“Atakayeumizwa na kibano hicho ni yule mbunge, diwani au mwakilishi anayetaka kuendelea kugombea. Kwa sasa hatakuwa tena na nafasi ya kufanya matukio, tofauti na wagombea wapya,” amesema.
Kwa mtazamo wa Dk Mbunda, pengine tangazo hilo limetokana na malalamiko ya watiania wapya, baada ya kushuhudia wabunge wanaotaka kuendelea wakifanya matukio ambayo, kimsingi, yanatengeneza mazingira ya ushindi.