Arusha. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki (EAC) ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki na Nyanda Kame wa Kenya, Beatrice Moe ameliomba Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kuidhinisha Dola za Marekani 109.33 milioni (Sh295.2 bilioni) kwa ajili ya matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika kikao cha bajeti kilichofanyika kwa njia ya mtandao, jana Juni 22, 2025, Moe amesema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mpango wa sita wa mkakati wa maendeleo unaozingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Baraza la Mawaziri wa EAC na maagizo ya wakuu wa nchi wanachama.
Waziri huyo amesema vipaumbele vya bajeti hiyo ni kuimarisha amani, usalama, michakato ya kisiasa na kuimarisha mifumo ya dharura kuimarisha mazingira mazuri kisiasa, kuendeleza Umoja wa Forodha wa EAC ili kuongeza shughuli za biashara miongoni mwa nchi wanachama.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha utekelezaji wa malengo ya kanda kulingana na Itifaki ya Soko la Pamoja na mifumo mingine kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa jumuiya.
Pia, kuhakikisha mchakato wa uanzishwaji wa taasisi ya uoanishaji wa sarafu na sera za fedha kuanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo ili kufikia hatima ya kuwa na sarafu moja katika nchi za EAC.
Waziri Moe ameongeza kuwa bajeti hiyo itazingatia mikakati thabiti ya kuwa na miundombinu inayozingatia mabadiliko ya tabianchi na matumzi ya kidijitali kukuza shughuli za biashara na mtangamano wa EAC, sambamba na kuijengea uwezo mihimili pamoja na taasisi zake kutimiza malengo yake.
“Mheshimiwa Spika, matarajio tuliyonayo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kuzingatia viumbaumbele vyetu, kwa mtazamo wa kidunia, ni kuweka mkazo katika kuweka mazingira rafiki ya kisiasa kwenye kanda yetu na kuhimiza maendeleo,” amesema Moe.
Kuhusu bajeti hiyo ya dola za Marekani 109.3 milioni, amesema dola 67.7 milioni ambazo ni sawa na asilimia 62, zinatarajiwa kutoka nchi wanachama, dola 41.5 milioni ambayo ni sawa na asilimia 38 kutoka kwa wadau wa maendeleo.

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC)ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Kenya,Beatrice Askul Moe akisoma hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 makao makuu ya EAC jijini Arusha leo,kulia ni Spika wa EALA,Joseph Nkakirutimana.Picha na EALA
Waziri Moe amesema mgawanyo wa bajeti hiyo unaelekezwa kwenye mihimili mitatu na taasisi zake ambayo ni Sekretariati ya EAC, iliyotengewa dola 55.2 milioni, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliyotengewa dola 5 milioni wakati Bunge la Afrika Mashariki (Eala) likitengewa dola 20.5 milioni.
Mgawanyo uliolekezwa kwenye taasisi za EAC ni Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (dola 7 milioni), Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki – IUCEA (dola 10.8 milioni huku taasisi ya Uvuvi ya Afrika Mashariki ikitengewa dola 2.43 milioni na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki (Eesteco) dola 2.21 milioni.
Taasisi zingine ni Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) iliyopo Zanzibar (dola 1.6 milioni), Kamisheni ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki – EAHRC (dola 2.35 milioni) na Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki (EACCA) imetengewa dola 1.52 milioni.
Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo ni dola 109.3 milioni imekua pungufu ya dola 5.08 milioni, ukinganisha na bajeti ya mwaka fedha 2024/2025.