Kisa Simba, Dube aongezewa dozi

YANGA imemalizana na Dodoma Jiji katika mechi ya Ligi Kuu Bara na sasa inajiandaa kwa mechi ijayo ya kufungia msimu dhidi ya Simba inayopigwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mechi hiyo ya Dabi ya Kariakoo iliyoahirishwa mara mbili kutoka Machi 8 na Juni 15, imepangwa kupigwa kuanzia saa 11:00 jioni ambapo Kombe litakuwa uwanjani kutokana na timu hizo kufukuzana kileleni mwa msimamo wa Ligi hiyo, Yanga ikiongoza kwa pointi 79, Simba ikiwa na 78.

Hata hivyo, kuna kitu kinafanyika kwa sasa kwa straika mahiri wa Yanga,Prince Dube ili aliwahi pambano hilo la marudiano la Dabi baada ya awali Simba kulala 1-0 katika mechi iliyopigwa Oktoba 19 mwaka jana.

Kuna hatihati kwa Yanga kuikosa huduma ya Dube aliye majeruhi kwa sasa baada ya kuumia na kutolewa uwanjani dakika ya 22 walipocheza dhidi ya Tanzania Prisons Jumatano iliyopita na nafasi yake ikachukuliwa na Clatous Chama aliyechangia bao moja katika ushindi wa 5-0.

Mshambuliaji huyo aliumia nyama za paja wakati anawania mpira wa kichwa na wakati anatua ndipo alipata shida hiyo iliyomfanya aukose mchezo dhidi ya Dodoma Jiji uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kwa sasa Yanga inapambana Dube awe tayari kwa mchezo huo dhidi ya Simba na wala hawajakata tamaa licha ya kuonekana kuna nafasi ndogo ya kuwepo uwanjani siku hiyo, ndiyo maana imeongeza matibabu zaidi ili kuhakikisha anakuwa fiti.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba, matibabu hayo ambayo yanafanywa kwa usimamizi na usiri mkubwa yameongezewa nguvu na madaktari wengine ili kupambana mshambuliaji huyo kuwa tayari kwenye mechi ya watani.

“Dube tunapambana acheze mechi dhidi ya Simba, awali ilionekana kama tatizo ni kubwa lakini aliporudi Dar es Salaam na kufanyiwa vipimo zaidi kuna matumaini akarudi mapema uwanjani na sasa tunapambana hilo liwezekane,” alisema bosi mmoja wa Yanga na kuongeza.

“Tumepewa asilimia kwamba anaweza kuwahi lakini tutajua zaidi ikifika Jumapili au Jumatatu, kama itawezekana itakuwa safi lakini kama itashindikana bado tuna timu bora ambayo inaweza kupambana na tukashinda.”

Awali daktari wa Yanga, Mosses Etutu akielezea majeraha ya Dube, alisema mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe aliumia nyama za paja kwenye mguu wake wa kushoto na alionyesha kuendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu ya awali.

“Nyama za paja zilivutika wakati aliporuka na baada ya kumpatia matibabu ya awali, alionekana kuendelea vizuri lakini tunapambana kumpa matibabu zaidi ili aweze kuwahi mechi zijazo,” alisema Etutu.

Huu ukiwa ni msimu wa kwanza Dube anaitumikia Yanga, mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango bora akifunga mabao 13 katika Ligi Kuu Bara na kutoa asisti nane akicheza mechi 25 kwa dakika 1,704.

Related Posts