Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa taasisi zote za umma kwamba ifikapo Julai 30, 2025 wawe wamejiunga katika mfumo wa GovESB, vinginevyo hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Juni 23, 2024 wakati akifunga maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yaliyofanyika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Mfumo wa G0vESB umetengenezwa maalumu na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ili kuwezesha mifumo hiyo kusomana na kubadilishana taarifa kwa wakati kwa lengo la kupunguza adha na shida wanazopata wananchi na watumishi.
Maadhimisho hayo yalianza Juni 16, 2025 na kushirikisha wizara 23 kati ya 26 pamoja na taasisi zaidi ya 140 ambapo walikuwa na kaulimbiu ya “Himiza matumizi ya kidigiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchangiza uwajibikaji”.
Waziri Mkuu amesema mfumo huo umetengezwa bure na kila anayejiunga hatozwi gharama lakini inashangaza kwa muda mrefu sasa watu wanaambiwa wajiunge hawataki.
“Agizo la saba, nazitaka taasisi zote za umma kuhakikisha ifikapo Julai 30 wawe wamejiunga katika mfumo huu, lazima tupate taarifa sahihi na ninyi muingie kwenye mfumo wa kubadilishana taarifa,” amesema Majaliwa.
Waziri amekemea lugha za ukali na kukosekana kwa ukarimu kwa watumishi wa umma jambo alilosema linadidimiza maendeleo lakini akatoa maagizo kwa viongozi kutenga bajeti ili watumishi waweze kushiriki kwenye maadhimisho ya mwakani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amesema mfumo umekuwa na thamani kubwa na umerahisisha mambo mengi yaliyokuwa nje ya utaratibu.
Simbachawene amesema hivi sasa dunia inakwenda katika utandawazi wa kiteknolojia, hivyo lazima vijana watumie chombo hicho kusafiri na dunia.
Akizungumzia mfuko wa uwekezaji kwa watumishi amesema umekuwa na manufaa kwani wanaweka kwa kudunduliza hadi kufanikiwa kununua nyumba.
“Mbali na hilo, watu wanaweka fedha kwenye mfumo huo kidogokidogo kulingana na kipato chao lakini siyo hivyo, bali unawasaidia hata kupata faida ya hadi asilimia 13 ya uwekezaji wao,” amesema Simbachawene.
Hata hivyo, Simbachawene amesema wataendelea kuwahamasisha taasisi zingine kujiunga kulingana na maagizo ya Serikali ili kuifanya Serikali ipate taarifa kwa wakati na muda sahihi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema mafaili yamepungua maofisi kutokana na matumizi ya mifumo hiyo.