Rais Mwinyi aanika mafanikio miaka mitano ya SMZ, baraza kuvunjwa Agosti 13

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amehutubia Baraza la 10 la Wawakilishi akibainisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali kwa miaka mitano akisema uwekezaji uliofanyika umeleta maendeleo na kuimarisha uchumi.

Dk Mwinyi amehutubia baraza hilo leo Jumatatu  Juni 23, 2025 katika ukumbi wa Baraza Chukwani huku akitangaza kulivunja Agosti 13, 2025 kupitia gazeti la Serikali.

Wakati akimalizia hotuba yake aliyoisoma kwa takribani saa moja, Dk Mwinyi amesema, “ili kutoa nafasi ya matayarisho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, kwa madaraka niliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 91(2)(a) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, natamka kuwa, Baraza la 10 la Wawakilishi nitalivunja rasmi Agosti 13, 2025.”

Baada ya kutangaza hivyo, ziliibuka shangwe za wawakilishi na kuanza kugonga meza na kuimba wimbo wa “tuna imani na Dk Mwinyi…oyaa oyaaa oyaaa…”

Dk Mwinyi amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa kiasi cha kuridhisha.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akikagua gwaride kabla ya kuhutubia Baraza



“Hadi kufikia mwaka 2024, umekua kwa kasi ya asilimia 7.1. Pato la Taifa kwa bei ya soko nalo limeongezeka kufikia thamani ya Sh6.57 trilioni mwaka 2024 kutoka Sh4.78 trilioni mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 63,” amesema.

Amesema pato la mwananchi limeongezeka na kufikia Sh3.22 milioni mwaka 2024, sawa na Dola 1,395 za Marekani kutoka Sh2.52 milioni mwaka 2020, sawa na Dola 1,099 za Marekani.

Kadhalika, ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeongezeka kutoka Sh856 bilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh2.104 trilioni mwaka 2023/24, sawa na ongezeko la Sh1.248 trilioni.

“Kwa lengo la kufanikisha utekelezaji mzuri wa mipango ya Serikali, bajeti ya Serikali imeongezeka kufikia Sh5.182 trilioni kwa mwaka wa 2024/25 kutoka Sh1.579 trilioni kwa mwaka wa 2020/21, sawa na ukuaji wa asilimia 228,” amesema Dk Mwinyi.

Kadhalika, amesema bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka Sh609.9 bilioni mwaka 2020/21 na kufikia Sh3.271 trilioni kwa mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 436.33.

Rais Mwinyi amesema kasi ya uwekezaji nchini imeongezeka, hadi kufikia Juni 2025, jumla ya miradi 485 yenye thamani ya Dola 6.2 bilioni  za Marekani imesajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar, (Zipa) inayotarajiwa kuzalisha ajira 25,470.

Dk Mwinyi amesema hadi kufikia Mei, 2025 mikopo 5,366 yenye thamani ya Sh39.4 bilioni ilitolewa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa wananchi 25,701 wakiwamo 1,560 wa makundi maalumu.


Katika kuwapatia mazingira bora ya kufanyia shughuli zao wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa masoko makubwa ya Mwanakwerekwe na Jumbi ambayo yameanza kazi huku Soko la Chuini likitarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Kwa upande wa viwanda, Rais Mwinyi amesema baada ya kukamilisha mazingira ya eneo maalumu la viwanda Dunga Zuze, tayari wawekezaji wameanza ujenzi wa miradi kikiwamo kiwanda cha kuzalisha dawa za magonjwa ya binadamu, kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki, kiwanda cha nguo, usindikaji wa mazao, uzalishaji wa nondo, waya na vifaa vya umeme na maabara za Taasisi ya Viwango Zanzibar.

Amesema kwa miaka mitano, viwanda 24 vimeanzishwa vikiwamo viwanda vya vipodozi, samani, vyakula, maji, vifungashio, vifaa vya ujenzi na umeme pamoja na kiwanda cha nguo.

Dk Mwinyi amesema mafanikio yamepatikana katika sekta kuu za uchumi wa buluu ambazo ni utalii, uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini, ukulima wa mwani, bandari, biashara zinazohusiana na usafiri wa majini na mafuta na gesi asilia.

“Mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya utalii kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii na kuimarika kwa sekta ya huduma hapa nchini. Idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 394,185 mwaka 2021 hadi watalii 736,755 kufikia mwaka 2024. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 86.9,” amesema.

“Jumla ya boti 1,027 za uvuvi na kilimo cha mwani zimetolewa na kuwanufaisha wananchi 32,000, kati yao asilimia 70 ni vijana na asilimia 90 ya boti za ukulima wa mwani wanufaika wake ni wanawake,” amesema.

Katika hotuba yake, amesema hadi Desemba 2024, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilometa 80.25 kati ya 100.9 za mjini kwa kiwango cha lami na zege huku kilometa 275.9 katika ujenzi wa barabara za ndani umefikia asilimia 71.

Dk Mwinyi amesema mageuzi yaliyofanywa na Serikali ya kushirikisha sekta binafsi, yamewezesha mapato ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuongezeka kutoka Sh12.9 bilioni mwaka 2021 na kufikia Sh40.2 bilioni mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 211.6.

Katika sekta ya umeme, amesema baada ya Serikali kupunguza bei ya kuunganisha umeme kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 50, imeongeza idadi ya wananchi waliounganishiwa umeme, hadi Julai 2024 jumla ya wateja wapya 138,065 wameunganishiwa huduma.

Amesema imefanikiwa kupeleka huduma za umeme katika vijiji 231 sawa na asilimia 76 ya lengo la kuunganisha vijiji 305 vilivyokusudiwa kufikishiwa huduma hiyo.


Dk Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 5,400 hadi tani 23,804 kwa mwaka na hatua hiyo imeanza kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde sita yenye ukubwa wa eneo hekta 1,053.

Wameongeza ukubwa wa eneo la umwagiliaji kutoka hekta 810 hadi kufikia hekta 2,164 na lengo ni kuongeza uzalishaji wa mpunga hadi tani 15 kwa hekta na kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua ambapo zaidi ya wananchi 20,000 wanatarajiwa kupata ajira kupitia mashamba hayo ya umwagiliaji.

Serikali imeimarisha miundombinu ya afya kwa kujenga hospitali kumi za kisasa za wilaya na moja ya Mkoa wa Mjini Magharibi zenye huduma bora za tiba zikiwamo za kibingwa pamoja na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi.

Kwa upande wa elimu, amesema: “Takwimu zinaonesha kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha pili kutoka asilimia 76.8 mwaka 2020 na kufikia asilimia 84.4 mwaka 2024, ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 56.1 mwaka 2020 hadi asilimia 85.7 mwaka 2023.”

Kuhusu sekta ya maji, amesema Serikali imefanikisha utekelezaji wa miradi miwili mikubwa ya maji ambayo ni mradi wa uhuishaji na uimarishaji wa huduma za maji Zanzibar wenye thamani ya Dola 92.18 milioni na Mradi wa Uimarishaji Huduma za Maji wa Fedha za Ahueni ya Uviko-19 wenye thamani ya Sh40.2 bilioni.

“Jumla ya matanki 15 yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 134 yamejengwa, visima 64 vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa lita za maji 177,000,000 kwa saa vimechimbwa pamoja na ulazaji wa mabomba kilomita 466.9,” amesema.

Rais Mwinyi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Tume za Uchaguzi INEC na ZEC zinaendelea na hatua za maandalizi ili kuhakikisha kazi hiyo muhimu linafanyika kwa misingi ya haki na sheria.

Awali, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Mulid amewashukuru wajumbe hao kwa ushirikiano waliomuonesha, akisema kazi hiyo ni ngumu, bila ushirikiano huo ingekuwa ngumu kufanikiwa.

Ameomba radhi kama kuna sehemu walitofautiana na kupishana lakini lengo ilikuwa ni katika kujenga.

“Limekuwa baraza la mfano na la kipekee, tunamaliza tukiwa wamoja, tumejadiliana mambo ya maendeleo,” amesema.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban amesema wamejitahidi kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yamefanikiwa.

Amesema sekta ya viwanda imechukua sura mpya kwa sababu wawekezaji wa viwanda wameanza kujitokeza na biashara inakuwa licha ya changamoto ndogondogo.

“Kuna ushindani wa biashara, sekta ya biashara inakua, tumefanya jitihada kuongeza aina za biashara kusafirisha kutoka kwenye karafuu, kwa sasa tunaongeza bidhaa za kilimo na baharini lakini muda si mrefu tutaanza biashara za viwandani,”amesema.

Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema wakati Rais Mwinyi analizindua baraza hilo Novemba 2020 aliahidi kuwa atafanya shughuli nyingi za ustawi wa jamii na kweli wameona utekelezaji wake.

“Amefanya mambo makubwa sana katika uhai wangu wa baraza, sikuwahi kuona mambo makubwa yanayofanyika katika kwa miaka mitano,” amesema mwakilishi huyo.

Related Posts