Wataalamu wasio na kampuni wapigiwa chapuo

Dar es Salaam. Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), ipo katika hatua za mwisho za kutekeleza kanuni ya mwaka 2024, itakayoruhusu wataalamu wa fani hiyo wasio na kampuni, kusimamia miradi ya ujenzi kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa.

Awali, sheria ilikuwa inamtaka msimamizi wa mradi awe na kampuni au atoke kwenye kampuni, lakini mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya AQRB Namba 4 ya mwaka 2010, pamoja na kanuni zake za mwaka 2024, yameruhusu wataalamu binafsi kusimamia miradi.

Hatua hii inatarajiwa kupanua wigo wa Watanzania kupata huduma hizo kwa gharama nafuu kulingana na uwezo wao.

Kaimu Msajili wa AQRB, Dk Daniel Matondo akizungumza leo Jumatatu Juni 23, 2025 jijini Dar es Salaam, amesema: “Tutawapangia madaraja yatakayoeleza ni miradi ipi watalaamu binafsi wanaweza kusimamia. Si kila mtu binafsi ataweza kufanya mradi wowote. Haya ni mabadiliko makubwa katika Sheria ya AQRB.”

Dk Matondo amebainisha hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu semina ya siku mbili yenye mada isemayo; ‘Kujenga Utalaamu Endelevu, Viwango na Mikakati,’ itakayofunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Juni 25 na 26 jijini Dar es Salaam.

Amesema semina hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na wadau zaidi ya 600, wakiwamo wawakilishi wa taasisi za kifedha, wabunifu, wakadiriaji majenzi, wadau wa maendeleo, mabenki, mashirika ya kitaifa na kimataifa, wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa za viwandani, pamoja na wanataaluma wengine wa sekta ya ujenzi, mipango, na ardhi.

Amesema mchakato wa mabadiliko hayo upo katika hatua za mwisho, kwani sheria imekwishapitishwa, na hivi sasa wanakamilisha miongozo itakayotumika.

“Miongozo hii itawaelekeza wataalamu ni aina gani ya miradi wanayoweza kusimamia, thamani yake, namna ya usimamizi, na jinsi bodi itakavyopata taarifa, kwani utaratibu huu umekuwa ukifuatwa na makampuni. Kwa kuwa ni jambo jipya, kupitia semina hii ya siku mbili tutawaelekeza wataalamu hawa na kuwaandalia miongozo kamili. Tunatarajia Julai mwaka huu tuanze rasmi utekelezaji wake,” amefafanua Dk Matondo.

Ameongeza kuwa semina hiyo itasaidia kukuza uelewa wa wataalamu kuhusu mabadiliko hayo, matakwa ya soko la sasa, pamoja na nafasi ya AQRB kuboresha ujuzi na maarifa ya wadau wa sekta ya ujenzi.

Kuhusu mada zitakazowasilishwa wakati wa semina hiyo, Dk Matondo amesema zitaangazia masuala ya kimkakati kama usimamizi wa biashara na fedha kwa wataalamu wa ujenzi, na mwelekeo wa ubunifu na usimamizi wa miradi ya majengo.

Mtaalamu wa fani hiyo, Goliath Mwacharandula, almesema mabadiliko hayo yataongeza fursa kwa wataalamu binafsi waliohitimu na kusajiliwa, wasio na kampuni, kufanya kazi kwa kujitegemea kisheria na kitaaluma.

Amesema hatua hiyo itapunguza utegemezi wa kampuni kubwa na kusaidia vijana wapya kuingia sokoni.

“Itawawezesha wataalamu binafsi kuwajibika moja kwa moja kwa kazi zao na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji,” amesema Mwacharandula.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa AQRB, Bundala Robert amesema  mwaka wa fedha 2024/25 bodi imewafutia usajili wataalamu tisa kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kushindwa kulipa ada zao za mwaka.

Meneja wa Huduma Saidizi wa AQRB, Mariam Chiponda amewataka wataalamu wa fani hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye semina hiyo, akibainisha kuwa ni muhimu kwa ajili ya kuongeza uelewa na kuboresha taaluma ya wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi nchini.

Related Posts