Watahadharishwa kuchunga ndimi zao kuelekea uchaguzi mkuu

Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimewaonya wanasiasa kuepuka mihemko kwenye majukwaa katika kipindi hiki ikiwa imebaki miezi minne kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Hatua hiyo imetajwa kusababisha uvunjifu wa amani na kuwagawa Watanzania wenye nia njema na Serikali yao.

Hayo yamebainishwa leo Juni 23, 2025 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (Mnec) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela wakati akifungua kongamano la maombi na maombezi ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan lililofanyika jijini Mbeya.

“Niwaombe wanasiasa nchini, nikiwepo mimi mwenyewe, tulinde hekima kama za Mfalme Suleman, tutumie ndimi zetu vizuri. Tusiende kwenye majukwaa tukiwa na mihemko ili kulinda amani, upendo na mshikamano,” amesema.

Amesema kama chama wana imani ushindani katika kinyang’anyiro cha nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu utakuwepo na kuwataka watakaoomba ridhaa wamtangulize Mungu, wasiwe sehemu ya kuwagawa Watanzania.

“Ukitaka kulijua tunda la Amani, huwezi kuliona kirahisi, wachungaji mnafahamu, leo tunaabudu tuko salama. Tanzania ni nchi ya Amani, tunapaswa kutambua yupo Mungu aliyeileta na kuiweka ikiwa na amani kwa watu wote,” amesema.

Amesema wataendelea kushirikiana na viongozi wa dini kuliombea Taifa na Rais Samia, lakini pia wanasiasa tumuombe Mungu kwa kutambua madaraka hutoka kwake.

Baadhi ya wachungaji na waumini wa madhehebu mbalimbali ya Dini Mkoa wa Mbeya , walioshiriki kongamano la kuombea uchaguzi na Rais Samia Suluhu Hassan  katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.Picha na Hawa Mathias.



Mwaselela amesema umefika wakati viongozi wajao wawe chachu ya kumcha Mungu ili kutengeneza Watanzania wamoja na kuepuka uvunjifu wa amani unaotokana na mihemko ya kisiasa.

Mshiriki wa kongamano hilo, Samweli Waya amesema sababu ya kufanya kongamano ni kuombea amani katika kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

“Taifa lazima liongozwe na nguvu za maombi ili livushwe katika kipindi kilichopo usoni cha uchaguzi mkuu,” amesema.

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa TAG, Baraka Ulumi amesema maombi ya kumuombea Rais na uchaguzi mkuu ni mwendelezo kama sehemu ya kufikisha sauti za waumini na wachungaji mikononi mwa Mungu.

“Huu ni mwanzo tu, tunatarajia kuungana na wachungaji na waumini wengine maeneo mbalimbali nchini kufanya maombi na kuona Watanzania wanachagua viongozi sahihi,” amesema.

Wakati huohuo, Mwaselela alichangia cha Sh 2 milioni kwa ajili ya kwaya zilizohudumu katika kongamano hilo.

Awali, Juni 20, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ziarani mkoani Mwanza, aliwaeleza wananchi kuwa Tanzania ina Amani, utulivu na utashi wa kisiasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kudumisha amani.

“Niwaombe ndugu zangu kutunza amani na utulivu. Tulete utulivu wa kisiasa, nchi yetu ibarikiwe kuwa na amani, tufanye kazi tulete maendeleo,” amesema Rais Samia.

Ameongeza: “Mkianza kutawanyana hapa, hakuna litakalofanyika na hili ndilo wengine wanapenda litokee, niombe sana ndugu zangu tuweke sifa ya nchi yetu Tanzania ni salama twendeni tukafanye kazi,” ameongeza Rais Samia.

Related Posts