Baba azika wanaye akiwa chini ya ulinzi

Hai. Wakati watoto Precious miezi 6 na Glory(4) Evance wakizikwa, baba yao mzazi Evance Kileka ameshiriki mazishi hayo akiwa chini ya ulinzi wa Polisi huku mama yao akiendelea na matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC.

Watoto hao ambao wanadaiwa kuuawa na mama yao mzazi kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao, wamezikwa leo Juni 24, 2025 nyumbani kwao, katika  Kijiji cha Mungushi, Wilaya ya Hai,  mkoani Kilimanjaro.

Katika mazishi hayo, ambayo yalitawaliwa na vilio na simanzi baba huyo mzazi alifika akiwa na askari wawili waliokuwa wamevalia kiraia ambapo baada ya maziko hayo waliondoka naye.

Akihubiri katika ibada hiyo ambayo imefanyika katika kanisa Katoliki, Parokia ya Familia takatifu Hai mjini, Padre Juvenal Kimario amesema kilichotokea wanafamilia wanapaswa kuomba sana na kudumu kwenye maombi,  kumwomba Mungu moyo wa uvumilivu ili kupita katika kipindi hiki kigumu.

“Tunatambua familia hii kwa sasa inapita kwenye kipindi kigumu sana kwa hiki kilichotokea, waumini tuendelee kuwaweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili wawe wavumilivu na kuwa na subira, tusikuhukumu maana hatujui kilichotokea,  tumwachie Mungu,” amasema padre Kimario

Akizungumza katika mazishi hayo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mungushi kati, Joachim Mbowe ameitaka jamii kuepuka kuchukua maamuzi wakati wakiwa na hasira kwa kuwa yanaweza kugharimu maisha ya watu ambao hawana hatia.

“Tunamshukuru Mungu kwa kuwapumzisha watoto wetu salama Precious na Glory, kwa kweli ni tukio la huzuni na majonzi makubwa hapa kitongojini kwetu juu ya tukio hili,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema “Wito wangu kwa jamii ni kwamba tujifunze kuacha kufanya maamuzi wakati wa hasira kwa sababu tunaamini kama mama alikuwa na ugomvi na mume wake basi asingehamishia hiyo hasira kwa watoto wake maana walikuwa hawana hatia yoyote,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

“Tuna majonzi makubwa  na matukio kama haya tulikuwa tukiyasikia kwa wenzetu lakini leo yametukuta, niwaombe wananchi tuendelee kuwa wavumilivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wake,” amesema Mbowe

Akitoa salamu kwa niaba ya Mbunge wa Hai Saashisha Mafuwe, Braison Munis amesema familia hiyo imepata pigo kubwa kutokana na msiba wa watoto hao ambao umeendelea kuibua maswali mengi.

Aidha amesema ipo haja ya jamii kuendelea kuiombea familia hiyo kutokana na msiba huo ikiwa ni pamoja na kuonyana pindi kunapoonekana viashiria vya matukio maovu.

“Hali hii sasa hivi mmesikia mambo mengi ambayo kwa sasa inafikia kule kwa sodoma na gomora. Kama hatutajirudi mapema mambo yatakuwa mabaya zaidi, kwani vijana wanategemewa katika ndoto zao za maisha na kila mmoja kwa nafasi yake,” amesema.

Ameongeza kuwa “Tuendelea kuombeana kwa sababu familia hii imepata msiba ambao unafanya watu tujiulize maswali mengi. Tuwape pole sana muendelee kuvumilia na kuombeana,” amesema.

Related Posts