Huu hapa ujumbe kwa wastaafu

Dar es Salaam. Katika juhudi za kubadili mtazamo kuhusu nafasi ya wastaafu katika jamii, Taasisi ya Philemon Foundation imewakutanisha wastaafu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili namna ya kutumia maarifa na uzoefu wao kuendelea kuchangia maendeleo ya kijamii, huku wakiishi maisha yenye furaha na heshima.

Mkutano huo umewakutanisha wastaafu waliowahi kufanya kazi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, utumishi wa umma na mashirika binafsi.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa waasisi wa taasisi hiyo, Rodgers Mbagaamesema kuwa kwa muda mrefu wazee wamekuwa wakisahaulika baada ya kustaafu, hali ambayo hupelekea wengi wao kuishi katika upweke, hali ya kukataliwa na wakati mwingine hata msongo wa mawazo.

“Tunajaribu kutengeneza kitu ambacho kinaweza kuwaunganisha, lakini pia maarifa, uzoefu, busara na hekima zao zikaendelea kutumika kuendeleza jamii kwa njia mbalimbali.  Tukiwaacha hivi kwamba wakishatoka kwenye ajira wakae tu nyumbani wanaanza kuona maisha hayana maana.

“Tunatambua kuwa watu ambao wanafikia umri wa kulazimika kustaafu wengi wanakuwa bado na nguvu pia busara na hekima yao ndiyo inakuwa kwenye kiwango cha juu, hivyo siyo sahihi kwamba mtu akistaafu ndiyo hawezi tena kuwa na mchango,”amesema Mbaga.

Mbaga amebainisha kuwa kupitia mpango huo, taasisi hiyo inatarajia kuanzisha klabu ya wazeenakampuni ya kitaalamu ambayo itakuwa na wastaafu wabobevu katika kada mbalimbali ambao watakuwa wakitoa ushauri au huduma za kitaalamu kulingana na taaluma walizobobea.

“Wazee hawa wanaweza kutoa ushauri kutokana na taaluma zao ambazo wamezifanyia kazi kwa muda mrefu. Tunao walimu wakongwe, madaktari, wahandisi na watendaji wa serikali waliostaafu ambao bado wana uwezo mkubwa wa kutoa mchango, tunataka jamii iendelee kuchota hazina ya maarifa kutoka kwao,”amesema.

Wastaafu walioshiriki mkutano huo wameipongeza taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kuwatambua na kuwapa jukwaa la kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii.

Mariam Mtau (62) ambaye ni mwalimu mstaafu amesema kuwa hatua hiyo siyo tu inawapa fursa ya kuendelea kuwa na mchango chanya, bali pia inawapa sababu ya kuishi maisha yenye matumaini, uhai na furaha.

“Kuna tafsiri kwamba mtu akistaafu ndiyo amefika mwisho wa maisha yake na watu wengi wanakubali kuichukulia hivyo, kwangu mimi kustaafu sio mwisho wa maisha bali ni mwanzo mpya. Uzee ni hazina lakini kwanini ujiache uchakae kwa sababu wewe umestaafu.

“Kupanga ni kuchagua, ukikubali kuchoka na kuchakaa utachakaa kwelikweli, lakini ukiamua kuishi utakuwa na maisha mazuri. Nawashauri tutumie taaluma zetu ili jamii ivune maarifa tuliyonayo. Kujifungia ndani na kusubiri kufa hayo ni mawazo ya kizamani.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya mstaafu Mercy Sila (70) amesema licha ya takwa la kisheria kuweka umri wa kustaafu haimaanishi mtu aliyestaafu hawezi kuendelea kuitumia akili yake kufanya vitu vyenye tija katika jamii hivyo ni jukumu lao wastaafu kujishughulisha.

“Binafsi nafanya kazi sana hadi wakati mwingine siamini kama nina miaka 70, hii yote kwa sababu bado naendelea kutumia maarifa niliyonayo na watu wananiona na kunihitaji niwafanyie kazi. Unavyoniona hapa nahudumu kwenye bodi mbalimbali na bado nina biashara zangu, pia ni Rais wa chemba ya wanawake wafanyabishara Tanzania.

“Nayasema haya ili wastaafu wengine wajue kwamba kustaafu sio sababu ya kubweteka na kusubiri kulea wajukuu, hapana fanya kazi hayo mambo ya wajukuu iwe ni kwa muda tu lakini isiwe kizuizi cha wewe kuishi maisha yako,” amesema Mercy.

Related Posts