Janga la Kiingereza vyuoni, Waziri ataja mbinu

Ni balaa. Ndivyo unavyoweza kueleza kuhusu hali ya umilisi wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu nchini.

Hali hii inaweza kuwa ishara tosha kwa watunga sera, kutazama kwa jicho la pili ufanisi wa mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji wa lugha hii katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wakati Kiswahili kikiwa na ahueni pengine kwa kuwa ni lugha mama au ya pili kwa wanafunzi wengi, Kiingereza kama lugha ya tatu na ya kigeni kimeendelea kuwa mlima mrefu kwa walio wengi.

Ni tatizo lenye mizizi iliyojikita tangu ngazi za chini za elimu. Wanapofika vyuoni hali ndiyo hii ambayo makala haya inaiangazia; nayo ni kufurutu kwa ada ya kubananga lugha hii muhimu duniani.

Si tu wanafunzi wengi vyuoni wanashindwa kukizungumza, lakini hata katika maeneo ya uandishi na uzingativu wa sarufi, wanaonekana ‘wamechoka’ mno.

Mwananchi limeona mitihani ya baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu kimoja nchini wanaosomea kozi za lugha ya Kiingereza na kubaini udhaifu usiomithilika wa wao kutumia Kiingereza.

Sehemu ya tafsiri ya mwanafunzi mmoja kuhusu ushauri wa Profesa Kitila Mkumbo kuhusu ajira.



Katika moja ya majaribio, wanafunzi walitakiwa kutafsiri sehemu ya ushauri uliowahi kutolewa kwa lugha ya Kiswahili na Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo kuhusu tatizo la ajira nchini.

Sehemu ndogo ya majibu ya baadhi ya wanafunzi ambayo Mwananchi imeyaona yalikuwa kama ifuatavyo:

ProFFesor Kitila Mkumbo who is the PRIME MINISTER OF UBUNGO RESIDENCE, has explained that the problem of employment in the country COMES FROM OUTDATED system of education….

‘’Professor Kitila Mkumbo who is ASSEMBLIES MAN of Ubungo in Dar es Salaam has explained that the problem OF JOB HAS BEEN CAUSED BY PASSING OVER TIME OF educational system….’’

THE EXECUTIVE PARLIAMENT of Ubungo in Dar es Salaam city, Professor  Kitila Mkumbo has described the problem of employment in our country is caused by education system…

Katika uchunguzi huo ilibainika si tu wanafunzi hao wana uwezo mdogo wa sarufi ya Kiingereza kama inavyojidhihirisha katika maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa, lakini hawakuwa na maarifa ya jumla ya masuala kadhaa ikiwamo majina ya vyeo.

Huyu naye ni mwanafunzi mwingine na hiki ndicho Kingereza chake



Msimamizi wa mtihani huo (jina limehifadhiwa) alisema katika zoezi hilo takribani wanafunzi wote darasani walishindwa kutafsiri ipasavyo cheo cha ubunge.

Mfano mwingine kwa mujibu wa uchunguzi ni kipande cha tafsiri kilichohusisha maneno: “Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.” Wanafunzi watatu walitafsiri maneno hayo ifuatavyo: “The Government Revolution of Zanzibar” badala ya “The Revolutionary Government of Zanzibar.’’

Kipande cha matini walichotakiwa kutafsiri kilisema:

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Makamu wa Pili wa Rais, imeeleza dhamira yake ya kuimarisha zaidi kilimo cha mwani ili kiweze kusaidia katika kuondoa umasikini na kuinua maisha ya Wazanzibari wanaotegemea maliasili za bahari kujikimu kimaisha.’’

Tafsiri ya mwanafunzi mmoja ilikuwa:

The government of revolution of Zanzibar through the second vice president, explains their purpose of strengthening more the Agriculture of mwani in order to help the elevation of poverty and to empower the life of people from Zanzibar whose depending from ocean resources in order to Live.

Utafiti wa George Shumbusho

Katika makala ya utafiti uitwao  Problems of communicating through the English Languages in Tanzanian Universities kama ilivyochapishwa katika Jarida la  Advances in Social Sciences Researches Journal  Vol. 7 No. 9  la mwaka 2020, George Shumbusho anatoa mifano ya ubanangaji wa lugha ya Kiingereza kwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya umma nchini.

Anatoa mifano ya baadhi wanafunzi walioandika barua kwa uongozi wa vitengo vyao na namna walivyoshindwa kujieleza kisarufi.

Mwanafunzi wa kwanza (mwaka wa pili)

“I was request for my supplementary results for … and … which I was done in October 2013’’

Mwanafunzi wa pili (mwaka wa tatu)

“I hereby state reasons to the following which made to failure of exams… my mom passed I was busy a following up with her estate… I humble ask for another chance to repeat the incompleted subject.’’

Mwanafunzi wa tatu (mwaka wa pili)

“My father have been seriously sick for eighteen months. My mother is a mere flow worker at

I fore thank and hoping that my request are going to be considered.’’

Kama haitoshi, Shumbusho anatoa pia kielelezo cha barua iliyoandikwa na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili. Sehemu ya barua hiyo inasema:

RE: APPLICATION FOR CONTINUOS WITH STUDY

Kindly refer on above heading,

I’m a master student of (mentions the programme) my result somehow not well perform due to time, materials accessibility and the nature of this course (mentions the course) is so much tough, but I tried the best while unfortunate and shamed to me as Discontinuous…..

Mhadhiri wa lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus aliwahi kuandika katika  Mwananchi siku za nyuma kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia umahiri mdogo wa Kiingereza kwa wanafunzi wengi ni lugha hiyo kutofundishwa kwa mbinu sahihi za kimawasiliano.

“Nilisema kumbe mfumo huu wa ufundishaji ungewawezesha wanafunzi wanapomaliza darasa la saba kuwa na uwezo mzuri wa Kiingereza, lakini inashangaza kuwa wengi hawana uwezo wa kuitumia lugha hiyo kabisa,’’ aliandika katika makala yake iliyochapishwa Mei 20, 2014.

Mtafiti, Mohamed Issa katika ripoti iitwayo Universities and enhancement of English as a second language in Tanzania secondary schools,  anasema uwezo mdogo wa kutumia Kiingereza kama lugha ya pili ni kikwazo kwa vyuo kuzalisha wahitimu wanaoweza kushindana katika soko la ajira la kanda ya Afrika Mashariki.

“Hali hii ikiendelea, lengo la Tanzania kufunza nguvu kazi inayohitajika kwa matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika maendeleo litakuwa jambo gumu,” inasema sehemu ya ripoti na kutoa rai kwa vyuo vikuu nchini kusaidia ufundishaji wa Kiingereza kama lugha ya pili katika shule za sekondari ili kuzalisha wanafunzi watakaoimudu wakiwa vyuoni.

Naye Anastazia Majenga katika tasnifu ya shahada ya uzamili iitwayo: “The challenges of using English languages in Tanzania colleges” anataja mambo kadhaa yanayosababisha wanafunzi vyuoni kuwa na uwezo mdogo wa kutumia lugha ya Kiingereza.

Yanayotajwa ni udhaifu wa menejimenti za vyuo kusisitiza matumizi ya lugha, wahadhiri kutohamasisha lugha hiyo, uwezo mdogo wa wanafunzi tangu wakiwa ngazi za chini na ukosefu wa motisha kwa watumiaji wa Kiingereza.

“Utafiti unapendekeza hatua madhubuti zichukuliwe na Serikali na menejimenti za vyuo kushughulikia changamoto za matumizi ya Kiingereza. Hatua hizo zinaweza kujumuisha uwekaji wa sera na taratibu kama vile sera ya hakuna huduma kama hutumii Kiingereza sambamba na utoaji motisha kwa wanatumia wa lugha hiyo,” anashauri.

Wakati hali ikiwa hivi vyuo vikuu na bila shaka hali mbaya zaidi ikiwa katika ngazi za chini za elimu, Sera ya Elimu toleo jipya la 2023 inatambua matumizi ya lugha zote mbili, yaani Kiswahili na Kiingereza katika ngazi tofauti za elimu.

Sehemu ya sera hiyo inasema: “…upo umuhimu wa kusisitiza matumizi ya Kiswahili katika kufundishia masomo yanayojenga uelewa wa utamaduni na historia ya Mtanzania ili kuihifadhi na kuitangaza. Aidha, lugha ya Kiingereza ni nyenzo muhimu ya kuwezesha kupata maarifa. Hivyo, ni muhimu kutumia lugha zote mbili.’’

Ni kwa sababu hiyo sera ikatamka: “Serikali itahakikisha kuwa Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za kigeni zinafundishwa kwa ufasaha na ufanisi katika ngazi zote za elimu na mafunzo.’’

Pamoja na utambuzi huo na hakikisho hilo la lugha kufundishwa kwa ufasaha, hali ya Kiingereza bado inatia shaka kwa walimu na wanafunzi kukosa umilisi wa lugha hiyo nyeti na muhimu ambayo ni sawa na Kiswahili cha dunia.

Ili kukuza weledi wa kutosha wa lugha hiyo na pengine kama sehemu ya mkakati wa kuondokana na aibu ya ubanangaji wa lugha kwa wanafunzi shuleni na vyuoni, Dk Kristomus anashauri matumizi ya mbinu ya ufundishaji na ujifunzaji inayolenga kumpa mwanafunzi uwezo wa kuwasiliana kwa stadi zote nne za kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.

“Hali hii ya kuacha kusisitiza stadi zote nne za lugha katika ufundishaji wa Kiingereza, ndiyo inayochangia wanafunzi kukosa msingi bora wa lugha,’’ anasema na kuongeza:

“Hali hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na walimu wetu ambao tafiti nyingi zinaonyesha wao wenyewe hawaimudu vizuri lugha hii. Mwalimu asipoweza kuimudu lugha anashindwa kujiamini katika ufundishaji.’’

Kwa upande wake, mdau wa elimu, Bakari Kheri anahoji kama mataifa mengi yana raia wanaozungumza lugha zao za taifa sambamba na Kiingereza kwa umahiri mkubwa, Tanzania inafeli wapi.

“Nenda mataifa kama Ufini na mengineyo ya Ulaya, watu wanajua lugha zao lakini wanaweza kuwasiliana vizuri tu kwa Kiingereza. Na hata Wazungu tunaowaona hapa nchini, wanatoka mataifa mbalimbali lakini wanakijua Kiingereza cha mawasiliano. Kile ambacho wao wamekifanya katika mifumo yao ya elimu, hata nasi tunaweza labda uniambie kuna mkakati maalumu wa kuhakikisha watoto wa Kitanzania hawatakiwi kukijua Kiingereza ili wakose fursa za kidunia,” anabainisha Kheri.

Waziri  ataja mbinu mpya za ufundishaji

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda anasema Kiingereza ni lugha muhimu na ndiyo maana kwenye mabadiliko ya mtalaa mpya, Serikali imeamua lugha hiyo ianze kufundishwa tangu darasa la kwanza, tena kwa mbinu za kimawasiliano

“Kiingereza kitafundishwa kwa namna ya mawasiliano zaidi kuliko mambo ya kanuni. Kumbuka mwalimu anaingia darasani kufundisha halafu muda mwingi anajaribu kueleza kanuni… ‘past tense’, ‘present tense’ ambavyo ni muhimu …lakini mwanafunzi hapati mvuto kwa sababu haanzi mapema kuzungumza, mwalimu anazingatia kanuni badala ya mawasiliano…,” anasema Profesa Mkenda katika mahojiano aliyowahi kufanyiwa na kituo cha televisheni cha Azam.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.

Related Posts