Kaa chonjo na nguo zenye nembo ya bangi

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo ametangaza kuwa Serikali itaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaovaa mavazi yenye picha ama alama za bangi.

Akizungumza jana mjini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa Ripoti ya Kitaifa ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2024 jana Juni 23, 2025, Lyimo amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada pana za kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na athari zake katika jamii.

“Kulingana na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, ni kosa kwa mtu yeyote kuvaa mavazi au kutangaza kwa namna yoyote matumizi ya dawa za kulevya haramu. Kifungu cha 24 cha sheria hiyo kinasema kuwa mtu atakayekiuka atachukuliwa hatua ikiwemo kifungo. Hivyo, yeyote atakayekutwa amevaa mavazi ya aina hiyo atawajibishwa,” amesema Lyimo.

Amesisitiza zaidi kwamba mavazi yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuathiri mitazamo na tabia za jamii, na hivyo kusisitiza umuhimu wa jamii kuungana katika mapambano dhidi ya matumizi ya bangi na dawa nyingine haramu.

Bangi iliongoza katika orodha ya dawa zilizokamatwa kwa wingi mwaka 2024, ikifuatiwa na Methamphetamine, Heroini na Fentanyl dawa ya kulevya ya kutengenezwa kwa njia ya kemikali huku DCEA ikikamata jumla ya tani 2,300 za dawa hizo, kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali.

Mbali na fulana (T-shirt), bidhaa nyingine maarufu zenye alama au picha za bangi ni pamoja na blauzi za mikono mifupi (vesti), mikufu, bangili, vitambaa vya kichwani, leso, duragi, vikuku vya mikononi, soksi, vikuku vya miguuni, pamoja na bidhaa nyingine

Related Posts