Makalla ataja sababu ya kusitisha ziara na mikutano

Dodoma. Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amosi Makalla, amesema kwamba kusitisha ziara, mikutano na makongamano ni hatua ya kuandaa vizuri mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani ndani ya chama hicho.

Ufafanuzi wa Makalla unakuja siku moja baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, kutoa taarifa ya kusitisha ziara, semina, mikutano na makongamano yote yanayohusisha wajumbe wa vikao vinavyohusika na kupigia kura za maoni wagombea.

Makalla ameyasema hayo leo Juni 24, 2025 wakati akihutubia katika mkutano wea hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mtekelezo jijini Dodoma.

Amesema kuwa viongozi wamefanya kazi kubwa ya kueleza yaliyofanyika katika kata na majimbo, ikiwemo mikutano ya kuimarisha CCM, ziara za wabunge na madiwani.

Makalla amesema CCM ni chama kikubwa na kwamba wamebakiwa na siku chache tu kabla ya kuanza kwa utaratibu wa chama wa wagombea kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu.

Shughuli ya uchukuaji wa fomu za uchaguzi kwa wanaoomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani litaanza Juni 28 hadi Julai 2, mwaka 2025.

Uchukuaji huo wa fomu unafanyika ikiwa tayari chama hicho kimewapitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza, huku Rais Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Ni dhahiri muda umeisha, nimesimama hapa kama katibu mwenezi kuwaambia kuwa tutasimama kwa muda ili tutoe nafasi ya maandalizi ya kura za maoni kwa maana mara baada ya chama chetu mabalozi ni watu muhimu sana katika msingi wa chama chetu,” amesema.

Amesema  mabalozi wa nyumba kumi ndio wako kule na wanachama, hivyo wameona wawape nafasi ya kuandaa mazingira kuelekea katika kusimamia kura za maoni.

“Sisi tuna viongozi wa matawi na kamati za kata wilaya mkoa wapate nafasi na kujiandaa kuratibu kura za maoni kwa hiyo kwa nia njema, tunasitisha kutoa nafasi ya maandalizi ya kura za maendeleo, kwa kuwa tunawaita mara kwa mara watakosa nafasi ya maandalizi,”amesema.

Makalla amesema hata yeye amepata upendeleo wa kwenda katika mkutano huo wa hadhara kwa kuwa yeye ni katibu mwenezi na msemaji wa chama.

Amesema ameambiwa ni mara ya mwisho na kuwa akawatangazie kuwa wanasimama kwa ajili ya  maandalizi ya kura za maoni.

Makalla amewataka kwenda kupata utulivu na kutafakari wagombea watakaochukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu.

Aidha, amesema katika taarifa alizonazo Mkoa wa Dodoma umevunja rekodi katika uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Mpigakura na hivyo wana matumaini ya kupata kura za kishindo kutoka mkoa huo.

Amesema kuelekea katika uchaguzi vyama 18 vitashiriki kwenye uchaguzi na kuwa Chadema imeamua kupumzika kushiriki kwenye uchaguzi baada ya kuchoka.

“Kwa hiyo tumewakubalia wapumzike na dalili za kupumzika kwao zimewakwaza wanachama nchini na nyie shahidi nimepokea hapa wanachama 280 kujiunga na CCM,”amesema.

Makalla amesema kama ‘derby’ ipo pale pale akimaanisha kuwa Uchaguzi Mkuu uko kama ulivyopangwa na kuwataka wote waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi huo.

Aidha, Makalla amesema kwa idadi ya wanachama wa CCM inayofikia milioni 13 ndicho chama kinachoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanachama duniani.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde anayemaliza muda wake, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Sita na amewaaga wakazi wa Dodoma kuwa atakwenda kugombea jimbo la Mtumba katika uchaguzi mkuu.

Katika mkutano huo, Makalla alipokea wanachama 280 wa vyama vya ACT Wazalendo na Chadema waliojiunga na CCM kwenye mkutano huo.

Mmoja ya wanachama waliokihama chama cha Chadema ni aliyekuwa Diwani wa Kigwe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, (Chadema), Adon Mabalwe amesema wamejifunza mengi kwa kukaa kwao nje ya CCM miaka mitano na wamekuja kushirikiana kukijenga chama.

Related Posts