Beersheba. Rais Donald Trump ametangaza kusitisha mapigano dhidi ya Iran, huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akidai kuwa malengo yao dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran yametimia.
Hata hivyo Israel imesisitiza itajibu kwa namna yoyote iwapo kutatokea uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa, uamuzi huo wa Marekani na Israel kukubali kusitisha mapigano umetangazwa leo Jumanne Juni 24, 2025, siku moja tangu Iran itekeleze mashambulizi dhidi ya Israel na kambi ya kijeshi ya Jeshi la Marekani iliyoko Doha, Qatar ya Al Udeid.
Kupitia ukurasa wake wa Truth Social,Rais Trump aliandika: “Hongera kwa wote! Tumekubaliana kwa kikamilifu kati ya Israel na Iran kuwa tutasitisha vita kwa jumla (ndani ya takribani saa 6 zijazo, baada ya pande zote mbili kukamilisha oparesheni zao za mwisho! kwa muda wa saa 12 na baada ya hapo vita vitakuwa vimekwisha rasmi!,”
Baada ya saa kadhaa kupita, Trump amechapisha tena ujumbe kwenye ukurasa wake wa Truth Social leo asubuhi saa 8 (saa 4 asubuhi za Afrika Mashariki), akisema: “Kusitisaha vita sasa kumeanza. Tafadhari msivunje makubaliano haya.”
Huenda tangazo hilo likawa ni mwanzo wa mwisho wa mgogoro huo uliodumu kwa siku 12, huku macho na masikio ya ulimwengu yakigeukia huko.
Mapema asubuhi ya leo, Israel ilishambuliwa vikali na Iran ambapo taarifa kutoka nchini humo zinasema watu wasiyopungua watano wakiwemo wanne waliouawa kwenye shambulizi lililofanywa eneo la Beersheba huku raia wengine wakijeruhi.
Ofisa wa Idara ya uokoaji za Israel, Magen David Adom amesema hadi sasa ving’ora vimeendelea kulia kote nchini humo ishara ya kwamba Iran bado inaendeleza mashambulizi yake dhidi ya miundombinu ya kijeshi na makazi ya raia nchini Iran.
Katika matangazo yake ya leo asubuhi Jumanne, Televisheni ya taifa ya Iran (IRNA) iliripoti kuwa kusitishwa kwa mapigano kati yake na Israel kumeanza, hata wakati huu ambao Israel inaendelea kuwatahadharisha raia wake kuhusu wimbi jipya la makombora kutoka Iran.
9,000 wakimbia makazi Israel
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetoa takwimu kuwa zaidi ya raia 9,000 wa Israel wamelazimika kuyakimbia makazi yao tangu vita na Iran ianze siku 12 zilizopita.
Mkazi wa Beersheba nchini Israel, Yehezkiel Cheri amesema alikuwa kwenye nyumba ya ibada asubuhi Jumanne wakati ving’ora vya tahadhari viliposikika kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, alipokuwa akielekea yalipo makazi yake alishtukia kuona misururu ya makombora yaliporomoshwa kutokea uelekeo wa Iran na kusababisha mlipuko mkubwa.
“Niliuona moto mbele yangu, nikakimbilia ndani ya nyumba. Sidhani kama tunahitaji kuendeleza vita hivi. Ni aibu. Hawa wanaouawa ni roho za Mungu, tunapaswa kuwalinda wote, kutoka kila taifa. Kila mtu anapaswa kujali kuhusu kila mtu,” amesema.
Qatar, Iraq zaingizwa kwenye mgogoro
Tangu Juni 13, eneo hilo lenye misukosuko limeshuhudia mashambulizi ya kila mara ya ndege zisizo na rubani na makombora kati ya Iran na Israel, hali iliyosababisha vifo vya raia wa pande zote mbili na kuongeza hatari ya kuzuka kwa vita vikuu visivyodhibitika.
Qatar nayo imejikuta ikivutwa kwenye mzozo huo baada ya kambi ya kijeshi ya Marekani ya Al-Udeid, iliyoko nchini humo, kushambuliwa kwa makombora kutoka Iran.
Tehran ilirusha makombora 14 kuvuka Ghuba ya Uajemi kuelekea kwenye kambi ya ushirika ya Al-Udeid nje kidogo ya Doha, Qatar, ikiwa ni kujibu mashambulizi ya Marekani kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran mwishoni mwa wiki.
Iran ilisema idadi hiyo ya makombora ililingana na mabomu yaliyodondoshwa na Marekani kwenye maeneo yake ya nyuklia. Iran pia ilisema kuwa walilenga kambi hiyo kwa makusudi kwa sababu iko nje ya maeneo ya makazi ya watu.
Maofisa walithibitisha kuwa makombora yote yalidunguliwa hewani na hakuna hata moja lililofikia lengo wala kusababisha majeruhi.
Wakati makombora yakishuka Doha, video kutoka ndani ya jumba la biashara maarufu la Villaggio Mall zilionesha raia wakikimbia kwa hofu kubwa, wakihofia usalama wao.
Akina mama waliokuwa na watoto mikononi mwao walionekana wakikimbia kwa hofu kuu kutoka jumba hilo la kifahari linalohudumia matajiri wa jiji hilo.
Hata hivyo licha ya Iran ilitoa taarifa kuhusu mashambulizi hayo kabla hayajatokea, Trump kwa mshangao mkubwa alishukuru Iran kwa onyo hilo la mapema.
Alisema kupitia ukurasa wake wa Truth Social: “Wameachilia yote yaliyokuwa moyoni mwao, na sasa tunatumaini hakuna chuki nyingine itakayofuata. Nawashukuru Iran kwa onyo la mapema, ambalo limewezesha kuepusha vifo na majeruhi.”
Tehran ilisema kuwa imezindua “Operesheni ya Ahadi ya Ushindi” ili kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya Marekani yaliyopewa jina la “Operesheni Nyundo ya Usiku wa Manane” yaliyofanyika Jumamosi.
Maandalizi ya mashambulizi hayo yalibainika kupitia uchunguzi wa setilaiti, na usiku wa jana maafisa wa usalama wa Marekani walithibitisha kuwa Iran ilitoa taarifa kwa mamlaka za Qatar kuhusu nia yao.
Mbali na hayo, video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha mlipuko mkubwa katika kambi ya kijeshi ya Taji, kaskazini mwa Baghdad, Iraq, ambayo inasemekana ilishambuliwa na ndege isiyo na rubani. Hakuna kundi au taifa lililokiri kuhusika na shambulio hilo.
Rais Trump na timu yake waliangalia maendeleo kutoka chumba cha operesheni Ikulu ya Marekani, huku anga la Qatar likifungwa kwa zaidi ya saa moja kabla kufunguliwa tena.
Kambi hiyo ya Al-Udeid inahifadhi wanajeshi wa Marekani pamoja na makao ya kikanda ya Jeshi la Anga la Uingereza. Ndege zote za Marekani na za ushirika zilikuwa tayari zimehifadhiwa sehemu salama kabla ya mashambulizi.
Iran ilisema mashambulizi hayo yalifanywa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi, ikionya kuwa “kipindi cha kupiga na kukimbia kimefikia mwisho.”
Kuwait na Bahrain pia zilifunga anga zao wakitarajia mashambulizi, lakini hadi sasa hakuna shambulizi lililoripotiwa katika nchi hizo.
Urusi nayo iliiunga mkono Iran, ingawa haikutoa msaada wa kijeshi kwa Tehran