Morogoro yapunguza idadi wagonjwa wa rufaa Muhimbili

Morogoro. Idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili na nyingine za kanda imepungua kutoka wastani ya wagonjwa 80 hadi kufikia wasiozidi 40 kwa mwezi.

Hiyo imetajwa kutokana na maboresho ya miundombinu, vifaa tiba, vipimo vya kisasa na uwepo wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali hospitalini hapo.

Hayo yamesemwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Daniel Nkungu alipokuwa akitoa taarifa baada ya ukarabati wa miundombinu ya jengo la kliniki maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali, uliofanywa kwa msaada wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF uliogharimu Sh18 milioni.

Dk Nkungu amesema kwa sasa hospitali hiyo inatoa huduma ya vipimo vya kisasa kikiwemo cha CT Scan, Digital X-Ray, mtambo wa kufua hewa tiba ya oksjeni, kifaa cha kuchunguza sikio, koo na pua, mashine 10 za kuchuja damu (dialysis) na uboreshaji wa huduma za daraja la kwanza.

Jengo la kliniki maalumu ya madaktari bingwa hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro baada ya kufanyiwa ukarabati kwa ufadhili wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF. Picha Hamida Shariff



“Miaka ya nyuma huduma hizi hazikuwepo, hivyo hospitali tulilazimika kuwapa rufaa wagonjwa wetu ya kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali nyingine za rufaa za kanda, lakini kwa sasa wagonjwa tunaopokea kutoka kwenye hopsitali za wilaya ni zaidi ya 2,000 kwa mwezi na rufaa tunazotoa kwa hazizidi 40, mtaona namna hospitali yetu ilivyoboreshwa,” amesema Dk Nkungu.

Pamoja na maboresho hayo amesema kukarabatiwa kwa jengo la kliniki maalumu ya madaktari bingwa hospitalini hapo kutasaidia madaktari bingwa 16 waliopo kutoa huduma kwa wagonjwa wakiwa katika mazingira mazuri ya usalama tofauti na lilivyokuwa awali, jengo hilo lilikuwa chakavu.

Akieleza ukarabati uliofanywa, Dk Nkungu amesema ni pamoja na kukarabati vyoo, kurekebisha na kufunga upya mfumo wa umeme na maji safi na maji taka, kuweka sakafu, dari, kupaka rangi na kuweka madirisha ya vioo.

Akitoa taarifa yake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi WCF Dk John Mduma amesema ukarabati huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kipaumbele cha kuboresha sekta ya afya nchini, hivyo mfuko umechangia kiasi fedha Sh18 milioni kwa ajili ya ukarabati.

“Tumeona tufanye hivi kwa sababu hospitali ni moja ya taasisi tunazoshirikiana nazo kwa karibu katika majukumu yao ya kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali ama ugonjwa wakiwa kazini, hospitali ni moja ya sekta ambazo tunazitumia katika kujua ukubwa wa ugonjwa ama madhara aliyoyapata mfanyakazi kabla ya kumlipa fidia,” amesema Dk Mduma.

Jengo la kliniki maalumu ya madaktari bingwa hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kabla ya kufanyiwa ukarabati. Picha Hamida Shariff



Amesema mfuko huo unapotekeleza sera yake iliyopitishwa na Serikali ya Jamhuri ya muuungano wa Tanzania ya kurudisha sehemu ya makusanyo ya michango ya wafanyakazi kwa umma, hospitali ni moja ya eneo wanaloangalia.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Best Magoma amesema Serikali kwa awamu mbalimbali imetoa fedha nyingi kweye sekta ya afya na mkoa wa Morogoro ni moja ya mikoa iliyonufaika na fedha hizo hasa kwa kununua vifaa tiba na kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Hivyo ametoa wito kwa watoa huduma kuangalia namna ya kuboresha huduma za afya, kwakuwa moja ya shughuli za msingi za hospitali za rufaa ni kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.

Muuguzi kiongozi wa kliniki maalumu ya madaktari bingwa, Rose Mmari amesema kuwa kuboreshwa kwa miundombinu ya kliniki hiyo kutawafanya wagonjwa waweze kupata huduma katika mazingira mazuri na ya matumaini.

Aidha amesema hata madaktari sasa wanatoa huduma katika mazingira salama, kwani jengo hilo limefungwa mifumo ya maji safi ambayo wanaitumia madaktari kunawa mikono kila wanapomaliza kumhudumia mgonjwa.

Related Posts