Dodoma. Serikali imeanzisha programu maalumu ya uendelezaji upya maeneo chakavu katika miji, ili kuondoa changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa huduma za msingi.
Kupitia programu hiyo, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.35 yameainishwa katika mikoa 24 kwa ajili ya kuendelezwa upya, ili yawe na tija kiuchumi na kijamii.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Godfrey Pinda ameliambia Bunge leo Jumanne Juni 24,2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Azan Mwinyi.
Katika swali lake, mbunge huyo aliuliza Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaondoa nyumba zisizo na ubora nchini.
Naibu Waziri amesema Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 zinahimiza uboreshaji wa makazi chakavu au yasiyopangwa.
Utaratibu huo unahusu maeneo ya miji kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma na miundombinu sambamba na kuongeza mchango wa maeneo hayo katika pato la Taifa.
“Kwa kuzingatia maelekezo hayo ya kisera, Serikali imeendelea kubadili taswira ya miji yetu kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Watumishi Housing Investment na mifuko ya hifadhi ya jamii,” amesema Pinda.
Naibu Waziri amewaomba wabunge kuwahimiza wananchi na wadau wengine katika maeneo yatakayoguswa na mpango huo kutoa ushirikiano, ili kurahisisha kazi ya kuondoa makazi chakavu na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wetu.