Dar es Salaam. Umeshawahi kukosa hedhi miezi miwili au mitatu, ukawa unaishi kwa hofu ukidhani una mimba, Je? Ulichukua hatua gani, ulishafikiria ile damu ambayo haikutoka ilienda wapi?
Wataalamu wa afya wamesema mwanamke anapokosa hedhi, damu hubaki ndani, hujengeka na wakati mwingine ikisababisha maumivu na hupunguza nafasi ya kushika mimba.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 24, 2025 Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na mfumo wa uzazi, Abdul Mkeyenge amesema kwenye mfuko wa uzazi kuna sehemu ndogo juu ambako iwapo yai halikurutubishwa na mbegu ya kiume, huenda kukaa hapo.
Amesema eneo hilo lina mishipa mingi ya damu, hivyo muda unapofika ile mishipa hupasuka na damu hutoka ikiambatana na yai ambalo halikurutubishwa.
“Mwingine hapati hedhi miezi sita mpaka mwaka, kila mwezi damu inatoka inatakiwa kutoka kwenye mfuko wa uzazi. Damu inaweza kujikusanya pale, mwingine damu anapata lakini kidogo sana hivyo nyingine inaweza kujikusanya, haya yote yanapunguza uwezekano wa kushika mimba,” amesema Dk Mkeyenge.
Mtaalamu wa afya ya mama na mtoto kutoka kituo cha Waridi Fertility Solutions kinachojihusisha na afya ya uzazi, Dk Rose Masonda amesema mwanamke kukosa hedhi mara kwa mara huashiria tatizo lililopo kwenye mfumo wa uzazi.
“Ukikosa hedhi hiyo damu haiendi popote, inabaki ndani inajengeka na kuleta maumivu. Inapunguza nafasi ya kushika mimba lakini pia mwili wako unakupa dalili,” amesema.
Amefafanua kuwa inawezekana ni tatizo la homoni, PCOS au mabadiliko ya maisha ikiwa siyo mwanamke aliyefikia hatua ya kukoma hedhi.
Mwanamke eyote aliyefikisha umri wa balehe, anatakiwa apate hedhi, katika ukuaji wa mwanamke zamani kuanzia umri wa miaka 9 mpaka 13 anakuwa kwenye umri wa kuvunja ungo na wengine huchelewa mpaka miaka 15.
Kwa mujibu wa Dk Mkeyenge mwanamke anapokuwa amefikia katika hatua hizo za ukuaji, mwili wake unakuwa umejirekebisha kwenye vichocheo, anapokamilika kwenye umri wa ukuaji lazima mfumo wake wa homoni au vichocheo uwe umekamilika tayari kutengenezwa.
Amesema ndiyo maana mara ya kwanza kupata hedhi, hutajwa amevunja ungo au kitaalamu ‘menarche’ akifika hatua hii ile homoni au vichocheo vinakuwa vimetengenezeka vizuri, kuanzia pale kila mwezi anaingia kwenye siku zake.
“Nini kinatokea mpaka anatokwa na damu ya hedhi, mwanamke huyu aliyefika katika ukuaji kuna mayai yanatenegezwa kwenye ovari, kila siku ya hatari likizalishwa linakuja kukutana na mbegu ya mwanaume, ikitokea limezalishwa na kuletwa kwa ajili ya kurutubishwa kama mbegu hazijafika kurutumbisha lile yai, linapoteza uhai ndani ya siku tatu tunasema mayai yake ni XX.
“Likipoteza uhai linaenda kuhifadhiwa katika mfumo wa uzalishaji eneo la juu la mfuko wa uzazi linaitwa ‘endometrium’ katika lile eneo limezungukwa na mishipa ya damu kwahiyo homoni kama inafanya kazi vizuri na ule mfumo uko vizuri inapofikia mwisho wa mwezi kuna mishipa ya damu huwa inapasuka lenyewe.”
Kwa mujibu wa Dk Mkeyenge damu inapotoka huwa imechanganyika na yai ambalo halijarutubishwa. Mwanamke anayepata hedhi hana changamoto yoyote kwenye uzazi.
Mwanamke mwingine haingii sababu amefikia ukomo wa hedhi miaka 45 na kuendelea, mwingine ni dada lakini haingii hedhi kwa sababu mfumo wake wa hedhi hauko sawa.
“Kitaalamu tunaita ana homone imbalance, homoni zake zinakuwa chache hata uzalishwaji wa mayai unakuwa mdogo lakini hata kinachochangia ile mishipa ipasuke inakuwa haiwezi kutokana na homoni zake kuwa chini,” amesema.
Amesema hiyo ndiyo sababu ukiwa na ujauzito sababu zile homoni za kutengeneza mayai zinakoma.
Hata hivyo, Dk Mkeyenge ametaja visababishi vingine mwanamke kukosa hedhi ni matumizi ya dawa za uzazi wa mpango, vidonge vya kila siku, dawa za dharura kukinga ujauzito maarufu P2 mara kwa mara, mwishowe anapata tatizo hilo.
“Madhara yake ni kuwa mwingine anaweza kuwa amefikia umri wa kupata ujauzito, akawa hapati wengine wananenepa sana kupita kiasi, mwingine anakuwa hayuko sawa, hisia hapati akifanya tendo la ndoa,” amesema.