Saa tano ngumu ndani ya mwendokasi

Dar es Salaam. Kama inavyosemwa na Waswahili, ukitaka kujua utamu wa ngoma sharti uingie uicheze, ndivyo ilivyo hata unapotaka kujua karaha za usafiri wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam, sharti upande.

Huduma za usafiri wa mabasi hayo, zilizoanza mwaka 2016, zikibeba matumaini ya kukoma kwa msongamano wa magari katika jiji hilo, lakini sasa yamegeuka kuwa tafsiri halisi ya karaha ya usafiri.

Ukiacha matumaini ya kukoma kwa msongamano, huduma za mabasi yaendayo haraka zilitajwa kuwa muarobaini wa kuchelewa kwenda kazini na kurudi nyumbani kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) mwaka 2017, usafiri huo umepunguza muda wa kusafiri kutoka saa 2 mpaka 3 hadi dakika 30–45 kwa barabara ya Morogoro.

Utofauti wa raha ya huduma za usafiri huo kati ya enzi hizo mradi ulipoanza Mei, 2016 na uhalisia wa hali ya sasa, ni mithili ya mbingu na ardhi, kama inavyoelezwa na watumiaji wa usafiri huo.

Magreth Nemez, mkazi wa Kimara Mwisho, Dar es Salaam, anasema ukitaka kuchelewa kufika kazini panda basi la mwendokasi.

Kuchelewa kwake, anasema, hakutokani na mwendo pole, bali ni muda utakaoutumia kituoni kusubiri basi lifike, unazidi saa moja na wakati mwingine zaidi.


Kinachoelezwa na Magreth kinasisitizwa na Amina Munisi anayeishi Mbezi Mwisho, Dar es Salaam, aliyewahi kujeruhiwa kupitia usafiri huo.

Jeraha hilo kidoleni, anasema, lilitokana na kubanwa na mlango baada ya kulazimisha kuingia kwenye basi lililojaa abiria, lakini hakuwa na muda tena wa kusubiri kwa sababu alishapoteza zaidi ya saa.

“Wakati naingia nikae vizuri, dereva akafunga mlango, vidole vyangu vikabanwa. Nikawa nalazimisha kutoa. Kwa kelele za watu ndani ya basi, dereva hakusikia haraka. Hadi anafungua mlango tayari kilishapasuka, damu zinavuja,” anasema Amina.

Mussa Adam si mtumiaji wa usafiri huo, lakini mwanawe anayesoma Shule ya Msingi Diamond hutumia zaidi mabasi hayo kwenda shuleni na kurudi nyumbani.

Anasema ingawa kuchoka ni kawaida kwa mtu anayesafiri kila siku, lakini inavyokuwa kwa mwanawe imepitiliza. Anapomuuliza, anamjibu karaha za mwendokasi.

“Mtoto anachoka sana. Kuna siku anafika nyumbani anashindwa kula. Anasema ameumia, mara amekosa pumzi. Anatoka shuleni saa 10, anafika nyumbani saa tatu hadi nne usiku,” anasema Mussa.

Ukitaka kuonja magumu na karaha za usafiri huo, kwa mujibu wa Meena Dawson anayeishi Kimara, upande basi hilo muda wa asubuhi kutokea Kimara Mwisho au Mbezi, na wakati wa jioni kutoka Gerezani au Kivukoni.

Anasema kusubiri basi kituoni pekee ni karaha tosha, bado kugombea nafasi ya kuingia pale linapofika, kadhalika kinyang’anyiro kingine ni kupata pa kukaa au kusimama.

Simulizi za machungu hayo zimesababisha mwandishi wa Mwananchi afunge safari kwenda kupanda basi hilo saa 12:02 asubuhi katika kituo cha Kimara Mwisho kwenda Kivukoni, na uhalisia wa ilivyokuwa ni kama anavyosimulia:


Ilichukua dakika chache kutoka nyumbani hadi kituo cha Kimara Mwisho. Ilikuwa saa 12:02 asubuhi. Isingewezekana kuhesabu idadi ya abiria waliokuwepo kituoni hapo, safari ni moja kwenda mjini ama Morocco kwa wachache, au Gerezani na Kivukoni.

Picha linaanza, kituoni kulikuwa na msongamano wa abiria kiasi cha kukosa eneo la kusimama kwa utulivu. Inakulazimu kumuegemea mwingine kujiegesha, huku kundi kubwa la watu likipambania nafasi ya kukaa mbele eneo linakosimama basi.

Kwa eneo nililokuwa, ilibidi nisubiri mabasi kadhaa yapakie ili walio mbele yangu watoke ndipo nipate nafasi ya kukaa mstari wa mbele na hatimaye zamu yangu iwadiye.

Kusukumana, malalamiko ya kukanyagwa, matusi na ukosoaji wa mradi ni machache kati ya mengi yaliyokuwa yakitoka vinywani mwa abiria tunaposubiri usafiri.

Wakati si ukuta bwana! Hatimaye nusu saa ikapita bila basi la Kivukoni kuingia, muda huo tayari yalishapita mabasi mawili moja linalokwenda Gerezani na lingine Morocco. Wale wa kwenda Kivukoni tukaendelea na subira.

Kwa msongamano uliokuwepo kituoni hapo, kimo chako kingeamua uvute hewa safi au upokee inayotoka kwa wenzio.

Hatimaye basi la Kivukoni linaingia. Ile hali ya kusukumana iliyokuwepo awali kumbe cha mtoto, wakati basi linafika ndipo niliposhuhudia uhalisia wa msukumano.

Haikuchukua dakika mbili baada ya basi hilo kufungua mlango, tayari lilishajaa. Kilichosikika ni kelele za “unaniumiza, unanikanyaga, kiatu changu,” kutoka kwa abiria waliokuwa wakipambania kupanda usafiri huo.

Haikuwa bahati yangu kwenda kwa basi hilo la kwanza, lakini tayari nilishatokwa jasho mithiri ya aliyelowana kwa mvua. Naangalia saa ilikuwa saa 1:12 asubuhi.

Mapambano yaliendelea na turufu ilikuwa kupata nafasi ya kukaa mbele, eneo ambalo basi husimama na kufungua mlango. Baadhi ya abiria walisikika wakisema lolote litakalokuja watapanda angalau wapunguze safari, kwangu haikuwa hivyo.

Msukumano wa abiria ukasababisha mwanafunzi aangukie barabarani eneo linakosimama basi, akanyanyuliwa. Tukio hilo lilimuinua mmoja wa watu waliovalia vazi linalomtambulisha kuwa mlinzi.

Kuja kwake, ilikuwa kujaribu kuwapanga watu wakae katika mstari. Pamoja na nia yake njema, hakuna aliyemuelewa hatimaye yakamshinda na akatolewa eneo hilo kwa aibu na fedheha. Alisukumwa akakosa la kufanya.

Mara linaingia basi lingine la Kivukoni. Mapambano yakaendelea, lakini awamu hii ilikuwa bahati mbaya kwa mwanamama mmoja, aliyeanguka mlangoni na kugeuzwa daraja la kuvuka abiria.

Kwa sababu alishakanyagwa na akawa hoi, ilibidi apewe nafasi ya kuingia ndani na kutunukiwa sehemu ya kuketi, ingawa daktari ndiye angeweza kuthibitisha hali yake.

Sikuwa mnyonge kihivyo, nilipambana hadi nikajikuta mstari wa mbele. Ni kuzuri kwa sababu basi likija unaliona na unakuwa wa kwanza kupanda, lakini hatari kwa sababu ni eneo linalopiganiwa na abiria wote, hivyo muda wowote unaweza kujikuta umeangushiwa barabarani.

Naangalia saa yangu, ilishafika saa 1:37 asubuhi. Nikiwa kituoni yalipita mabasi manne bila abiria na hayakuchukua abiria, yakaendelea na safari. Kila basi lililopita bila abiria, lilipigiwa zogo isiyo mfano.

Kila kundi la abiria lililopanda basi, liliacha kitu. Basi la kwanza kiliachwa kiatu, la pili liliacha miwani, lakini ilishavunjika.

Dakika 10 baadaye basi la Kivukoni linaingia, kabla halijafika kila abiria aliyekuwa mbele alikaa mkao wa mapambano na lilipofika na mlango kufunguliwa, nilijikuta ndani si kwa juhudi zangu, nilisukumwa.

Sikuelewa ni muda gani umetumika abiria kuingia ndani ya basi na kujaza vitu vyote, huku wengine tukisimama na kukosa hata pa kushika. Isingekuwa rahisi kukwepa kugusana na mwingine au kujitenga na pumzi ya jirani yako.

Eneo nililokuwepo ni katikati na isingewezekana kushika popote na hata hivyo, nisingeanguka kwa sababu nilibanwa kiasi cha kukosa pumzi ya hakika.

Safari ikaendelea kidogo, mara linasikika tangazo la abiria wasogee kutokea mlangoni. Haikuwa rahisi kuinua hata mguu. Dereva akaendesha kwa mwendo wa haraka kiasi, kisha akafunga breki ghafla. Nikaambiwa “anatuchekecha.”

Mapambano ilikuwa kuangalia saa. Nikashindwa kuinua mkono kutoa simu mfukoni kwa namna nilivyobanwa. Namuuliza jirani aliyekuwa na simu mkononi ananambia tayari ni saa 1:58.

Safari kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni ilikuwa na vituo vichache na ilichukua dakika 40 kufika mwisho. Hadi nafika Kivukoni ilishakuwa saa 2:32 asubuhi.

Hata hivyo, nilifika Kivukoni nikiwa na harufu tofauti na manukato niliyotumia na ilinilazimu kwenda kusafisha viatu upya.

Sikuishia hapo, siku kadhaa baadaye nilikwenda kupanda basi Kivukoni kwenda Kimara Mwisho. Shida ilianzia eneo la kukata tiketi. Nilikuta kundi la abiria wanasubiri huduma. Naambiwa mtandao unasumbua.

Ilinichukua nusu saa hadi kupata tiketi. Saa 10:22 jioni naingia kituoni. Ndani ya kituo nakutana na msururu wa abiria waliojipanga kwa mistari. Niliona ulipoanzia lakini si ulipoishia.

Wakati nauliza sisi wa Kimara tunakaa wapi, naonyeshwa mstari usio na mwisho, huku na kule mara napata ulipoishia na hatimaye naungana na safu.

Hali ilikuwa hivyo, wakati kituoni hapo kukiwa na mabasi saba yaliyoegeshwa bila dereva. Naambiwa mabovu, wengine wanasema madereva wanaringa, wapo walionijibu yanapumzika.

Tofauti na Kimara, katika kituo cha Kivukoni hakuna kusukumana, lakini utasimama kwenye mstari hadi uite mama. Magari zaidi ya matatu yakapakia, lakini bado sikufikiwa.




Hatimaye saa 12:48 jioni napata gari tena na nafasi ya kukaa. Nilidhani halitajaza, kumbe iliachwa nafasi kwa ajili ya abiria wa mbeleni. Tulipofika kituo cha Posta ya Zamani, liliingia kundi la abiria kwa kusukumana ghafla basi lilijaa. Hadi nafika Kimara, ilishakuwa 1:29 usiku.

Idadi ya saa tano zimepatikana kuanzia saa 12:02 asubuhi hadi saa 2:32 asubuhi kutoka Kimara hadi Kivukoni, kisha Kivukoni hadi Kimara kuanzia saa 10:22 jioni hadi saa 1:29 usiku. Ni zaidi ya saa tano.

Kinachoshuhudiwa nyakati za asubuhi na jioni, ni tofauti na mchana. Abiria ni wachache na kuna wakati baadhi ya viti vinakosa wakaaji.

Mwandishi alifanya safari ile ile kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni, lakini ilikuwa saa 5:26 asubuhi. Katika kituo cha Kimara Mwisho kulikuwa na abiria 18 waliokuwa wakisubiri mabasi ya kwenda maeneo tofauti.


Ilichukua dakika 15 basi la Kivukoni kufika, hivyo saa 5:41 tulipanda bila bughudha wala kugombea.

Safari kutoka Kimara Mwisho hadi Kivukoni, ilichukua dakika 27, ingawa basi lilikuwa linasimama kila kituo kupakia abiria na katika baadhi ya maeneo hakukuwa na mtu aliyepanda.

Hadi tunafika Kivukoni, basi hilo linalopakia abiria 80 kwa mujibu wa Dart, lilikuwa na jumla ya abiria 34, baadhi ya viti vilibaki wazi.

Katika safari hiyo, hakukuwa na purukushani za kugombea kuingia ndani ya basi wala nafasi ya kukaa. Kila aliyeingia alikuta viti vya kutosha na alichagua pa kukaa.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa hata kwa safari ya kutoka Kivukoni kurudi Kimara Mwisho iliyoanza saa 6:18 hadi saa 6:50. Basi lilisimama kwenye kila kituo kwa takriban dakika moja.

Baadhi ya vituo havikuwa na abiria na vingine walikuwepo wachache. Basi halikujaa kama ilivyokuwa kwa safari ya jioni.

Msongamano huo wa abiria kwa mujibu wa Dart unasababishwa na uchache wa mabasi katika njia hiyo, tatizo linalotarajiwa kukoma hivi karibuni.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali inatanzua vikwazo vya kisheria vinavyoathiri uendeshaji wa mradi huo, ili awamu nyingine ziendeshwe kwa ufanisi.

Ili kutatua changamoto ya uhaba wa mabasi, alisema tayari zilishapatikana kampuni nne zitakazotoa huduma katika awamu mbalimbali za mradi huo, zikihusisha kuleta mabasi mengi.

Ukiacha kilichoelezwa na Waziri Mkuu, Juni 3, 2025, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia alisema mradi wa mabasi yaendayo haraka awamu ya pili Gerezani-Mbagala utaendeshwa na wazawa ambao wanatarajia kushusha mabasi 255.

Dk Kihamia alisema wameingia mkataba na Kampuni ya Mofat Company Limited: “Kuanzia Juni na ni mkataba wa miaka 12 ili kuendesha mradi wa njia ya Mbagala.”

Alisema kampuni hiyo ni ya wazawa wanaotarajia kuanza Agosti 2025: “Wataingiza mabasi 255 yanayotumia gesi,” amesema.

Dk Kihamia amesema awamu ya kwanza njia ya Kimara- Morocco- Kivukoni na Gerezani itaendeshwa na Kampuni ya Emirates National Group (ENG) kwa kipindi cha miaka 12 na anatarajia kushusha mabasi 177.

Mbali na mabasi hayo yanayofika Agosti, Dk Kihamia amesema Septemba kuna mabasi mengine 200, Novemba 200 na baadaye 100 kwa njia zote.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Dart, William Gatambi amesema tangu kuanza kwa mradi huo asubuhi na jioni kumekuwa na abiria wengi.

Ili kuendana na hali hiyo, amesema wamekuwa wakipeleka mabasi mengi nyakati za asubuhi na jioni katika vituo husika.

Amesema mpango wa muda mrefu, ni kuongeza mabasi kwa ajili ya kuhakikisha vyombo vya usafiri vinavyopelekwa vinakidhi mahitaji.

Related Posts