Serikali kuboresha skimu mpya za umwagiliaji Iringa

Iringa. Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imezindua mradi wa ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji mkoani Iringa, ukilenga kuongeza tija ya kilimo kwa wakulima wa vijiji vya Kata ya Ilolompya unaogharimu Sh33.8 bilioni.

Vijiji vya kata hiyo vilivyofikiwa na mradi ni  Luganga, Magozi, Ukwega na Ilolompya unaolenga kunufaisha wakulima 8,600 ndani ya mwaka mmoja. 

‎Akizungumzia mradi huo leo Juni 24, 2025 mhandisi wa umwagiliaji Iringa, Peter Akonaay ameeleza kuwa mradi huo unahusisha ujenzi mpya na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye jumla ya ekari 20,250 na kukamilika kwake kunatarajiwa ndani ya mwaka mmoja.

‎Vilevile skimu ya umwagiliaji ya Magozi itahusisha ekari 3,250, zitakazowekewa miundombinu ya kisasa kuhakikisha maji yanawafikia wakulima kwa ufanisi zaidi.

‎”Lakini, Skimu ya Luganga itaongeza uwezo wa umwagiliaji hadi kufikia ekari 1,700,” amesema Akonaay.

‎Amesema ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo ni mwendelezo wa kazi zilizoanza mwaka 2020, lakini sasa zimepanuliwa kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi. 

‎”Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha kaya 2,276 zenye jumla ya wakazi 8,869, kati yao wanawake ni 4,531 na wanaume 4,338 na wanufaika hawa wanatoka katika vijiji vitano vilivyoko kwenye Kata ya Ilolompya, ambavyo ni Luganga, Ukwega, Magozi, Ilolompya na Mkombilenga,” amesema.

‎Aidha, mazao makuu yanayotarajiwa kulimwa kupitia skimu hizo ni mpunga, mihogo, mahindi, maharagwe, nyanya na mbogamboga.

‎”Kupitia mradi huu, wakulima watakuwa na uwezo wa kulima misimu yote miwili, hivyo kuongeza uzalishaji na kipato,” amesema Akonaay.

‎Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha uendelevu wa miundombinu hiyo pamoja na kutoa mafunzo ya matumizi bora ya maji na kilimo cha umwagiliaji chenye tija.

‎Mradi huo umetajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 mkoani Iringa.

‎”Na mkandarasi aliyepata zabuni ya kutekeleza mradi huu ni Kampuni CREC (EA) Ltd,” amesema Akonaay katika taarifa yake.

‎Wakizungumza na Mwananchi Digital wananchi wa maeneo husika kutoka Tarafa ya Pawaga wameeleza kuwa wamepokea mradi huo kwa furaha, wakisema ni mkombozi hasa kutokana na changamoto za kutegemea mvua zisizo na uhakika.

‎Mkulima Siwazuri Mgoiganga amesema: ‎“Tulikuwa tunalima kwa kubahatisha. Tukipata mvua tunavuna, tusipopata tunapoteza kila kitu. Lakini sasa, mradi huu utatufanya tulime mara mbili kwa mwaka na kuongeza kipato.” 

‎Wakulima wa Magozi wameahidi kushirikiana katika uendelezaji wa mradi huo, wakiomba pia wapatiwe mafunzo ya matumizi bora ya maji na mbinu za kisasa za kilimo ili kufaidika zaidi.

‎ Mwenyekiti wa skimu ya umwagiliaji Magozi, Alphonce Mdindile amesema kuwa skimu ina jumla ya wanachama 500 walioko eneo la mradi na wanatarajia kunufaika moja kwa moja kupitia upatikanaji wa huduma bora za umwagiliaji. 

‎“Tunaishukuru Serikali kwa mradi huu. Wananchi wanatarajia kupata huduma ya maji kwa ajili ya kilimo na hii ni neema kwa wakulima wa Magozi, hasa kipindi hiki ambapo mvua hazitabiriki,” amesema Mdindile. 

‎Amesema faida ya mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa mazao, uhakika wa chakula, kipato na kupunguza changamoto ya umaskini katika kaya.

Related Posts