Undani kibano cha CCM kwa wagombea, uteuzi wa Rais Samia

Dar es Salaam. Baada ya tetesi zilizodumu kitambo, hatimaye rasmi viongozi wa Serikali waliohusishwa na nia za kuutaka ubunge katika majimbo mbalimbali, wameondolewa kwenye nafasi zao, huku wadau wa siasa wakisema, uamuzi huo umelenga kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea.

Hatua ya kuondolewa kwa viongozi hao, inakuja zikiwa zimesalia siku tano kabla ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuanza rasmi mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa makada wake wanaowania ubunge, udiwani na uwakilishi.

Viongozi hao ni wakuu wa mikoa, wilaya, taasisi na watendaji wakuu wa wizara, ambao awali gazeti hili, liliripoti kuhusu nia zao za kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Waliowekwa kando, kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi iliyotolewa jana, Juni 23, 2025 ni Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Peter Serukamba (Iringa), Juma Homera (Mbeya), Daniel Chongolo (Songwe) na Thobias Andengenye (Kigoma).

Ukiacha wakuu wa mikoa, viongozi wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe.

Inadaiwa Makonda atagombea Arusha Mjini, Chongolo (Makambako), Homera (Namtumbo), Serukamba (Kigoma Kaskazini) na Andengenye (Busokero).

Baada ya kuondolewa, Chongolo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika kumshukuru Rais Samia kwa kumwamini kwenye nafasi hiyo na wananchi wa Songwe kwa ushirikiano wao, huku akidokeza kuwa anarudi nyumbani Njombe.

“Asante Mheshimiwa Rais wangu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa kwangu. Asante sana wana Songwe kwa kunipokea na kunipa ushirikiano mkubwa. Hakika mwaka mmoja na robo mmenipa ushirikiano mkubwa sana. Songwe imeingia kwenye historia ya maisha yangu ya kudumu, hakika sitaisahau.

“Nimehitimisha utumishi wangu. Kijiti nakikabidhi kwa mdogo wangu mkubwa Mheshimia Jabir Makame, mhifadhi wa maisha. Narudi nyumbani Njombe,” ameandika.

Hata hivyo, kuondolewa kwao ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye Machi 11, 2025 aliwaambia wateule wake wanaotaka kugombea watoe taarifa mapema ili nafasi zao zirithiwe na walio chini yao.

“Nilimwambia Katibu Mkuu Kiongozi, peleka sekula serikali za mitaa, yeyote mwenye nia ya kugombea atwambie mapema ili tumpandishe wa chini yake ashike ile nafasi. Hatutaki pale wakati fomu zinatoka watu wote wanakimbia kwenda kuchukua fomu na mnatuacha serikali za mitaa hazina wasimamizi.

“Mnabakia kujaza watu ambao hawana uzoefu. Lakini tukijua mapema tutatayarisha watu wa kujaza hizo nafasi, kuwapa miongozo, kuwafanyia mafunzo ili wawe tayari kukabiliana na uchaguzi. Sasa usipojisema mapema ukija kuchukua fomu mbele umekosa yote,” alisema.

Hayo yote yanakuja, ikiwa tayari CCM ilishatangaza kuwa, Juni 28 hadi Julai 2, mwaka huu, ndiyo mwanzo na mwisho wa mchakato wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho kuchukua na kurejesha fomu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alitangaza marufuku kwa wagombea ndani ya chama hicho, kuitisha vikao, warsha, ziara na makongamano na wajumbe watakaopiga kura za maoni.

Marufuku hiyo, imekuja miezi kadhaa baada ya chama hicho, kuweka kibano kwa wagombea wake, kwa kuwaongezea wajumbe wataoshiriki kupiga kura za maoni.

Yote hayo kwa mujibu wa wataalamu wa siasa, yanalenga kupunguza vitendo vya rushwa kuelekea mchakato wa ndani wa chama hicho na kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea.

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Kiama Mwaimu amesema kuondolewa kwa wateule wenye nia ya kugombea, kunalenga kuweka mizania sawa kati yao na wagombea wengine.

Ametolea mfano kwa nafasi kama ya mkuu wa mkoa, anapoachwa aendelee na wadhifa wake hadi muda wa kuchukua fomu, atakuwa na ushawishi zaidi ukilinganisha na wagombea wasio na nafasi.

“Mkuu wa Mkoa ana ushawishi, lakini anaogopwa kwa nafasi yake, ukimuacha na nafasi yake kuna uwezekano akachaguliwa kwa sababu ya ukuu wa mkoa alionao. Lakini ukimwondoa unaruhusu watu wampime kwa uhalisia wake,” amesema.

Kwa ujumla kilichofanywa na mamlaka ya uteuzi na katazo lililotolewa na CCM, amesema shabaha yake ni kuweka mizania sawa miongoni mwa wagombea na kudhibiti rushwa.

“Ni mchakato wa kutaka kuzuia rushwa ndani ya Chama. Kwa sababu akiendelea kuwa na nafasi yake ya Mkuu wa Mkoa atakuwa na ushawishi kwenye jamii, akiondolewa atapunguziwa nguvu hiyo, ili kuwe na mizania sawa na wagombea wengine,” amesema.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda ametoa tafsiri mbili kuhusu uamuzi wa CCM na mamlaka ya uteuzi.

Kuhusu marufuku ya CCM, amesema pengine imeona kuna kundi lililojilimbikizia fedha kujipanga kununua uongozi na kwamba tayari limeshaonekana kuwa tishio.

Amesema CCM imeamua kuendelea kuweka mazingira magumu ya rushwa katika michakato yake, ili kutengeneza mazingira sawa kwa wagombea wote.

Ukiacha sababu hiyo, amesema uamuzi huo unalenga kudhibiti rushwa na hatimaye wapatikane wagombea kwa sababu wamekidhi kuzipata nafasi husika.

Nyamsenda amesema yote yanayoendelea ni dalili kuwa uchaguzi umewadia. Hata hivyo, utaratibu wa viongozi kuondolewa katika nafasi zao ili wakagombee ni kawaida.

“Kwa mwenendo unaoendelea hasa katika mabadiliko yaliyofanywa na CCM kuongeza wigo wa watu wanaotakiwa kupiga kura ni wazi kuwa chama hicho kimepanga kudhibiti rushwa,” amesema.

Amesema kwa muda mrefu kumeonekana viongozi mbalimbali wakitoa misaada, kuitisha mikutano na wajumbe na vikao mbalimbali wakitoa zawadi, mambo ambayo ni rushwa.

Hata hivyo, amesema katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kustukiza, inabidi kufanyike utafiti wa kina ili kubaini undani wake.

“Hili la kuzuia vikao nalo limekuja kustukiza lakini kama limekuja kudhibiti rushwa au kundi fulani lililojilimbikizia nguvu za kifedha na limeonekana kuwa tishio kwa kundi lililopo madarakani,” amesema Nyamsenda.

Related Posts