Wanaume wakimbia kijiji kuhofia kukamatwa mauaji ya ndugu wawili

Shinyanga. Vijana wawili wa familia moja wakazi wa Kitongozi cha Bulima Kata ya ltilima wilayani Kishapu mkoani Shinyanga   wamekutwa wameuawa nyumbani kwao na mtu anayedhaniwa kuwa ni ndugu yao kisha kuiba magunia 15 ya mpunga.

Hata hivyo, imeelezwa mtuhumiwa huyo naye aliuawa na wananchi baada ya kukiri kuhusika na wizi wa magunia hayo 15 katika nyumba hiyo walikouawa vijana hao.

Tukio la mauaji ya vijana hao limegundulika  Juni 22, 2025 baada ya kaka yao ambaye alikuwa amehifadhi maguni 15 ya mpunga kwenye nyumba hiyo kufika na kukuta harufu kali ndipo alipoingia ndani na kukuta wote wameuawa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Itilima, Joseph Kulwa amesema baada kijana wa familia hiyo kwenda kuangalia magunia yake ya mpunga aliyokuwa ameyahifadhi kwa bibi yake ambaye alikuwa anaishi na wajukuu zake ambao wameuawa.

Kulwa amesema vijana hao Nestori Henery ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Busiya na mdogo wake Mashigana Juma wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 hadi 15 .

Amesema vijana hao walikuwa wanaishi na bibi yao ambaye hakuwepo wakati tukio linatokea kutokana na kusumbuliwa na maradhi  hivyo alikuwa amekwenda kupata msaada wa matibabu kwa mtoto wake wa kike kijiji jirani.

Nyumba waliyokuwa wanaishi ndugu wawili waliouawa na ndugu yao mwingine kisha kuiba magunia 15 ya mpunga.



Mwenyekiti huyo amesema kutokana na tukio hilo, wananchi kutoka maeneo mbalimbali walikusanyika na kuanza kufuatilia ndipo walipomkamata ndugu mwingine wa familia hiyo Tuju Henery (30) ambaye anatuhumiwa kufanya mauaji hayo.

Amesema baada ya kumhoji alikiri kuiba magunia 15 ya mpunga na kuwaua wadogo zake wawili ili kuficha ushahidi, ambapo wananchi hao waliamua kujichukulia sheria mkononi na kumshambulia kisha kumuua.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Busiya aliyokuwa akisoma kijana Nestroy Henery (15), Badi Mfinanga amesema tukio hilo limewasikitisha kutokana na kijana huyo alikuwa anajituma katika masomo yake na amekatishwa ndoto zake.

Kaka wa marehemu hao amesema wadogo zake wameuawa ili kuficha ushahidi akidai huenda walimtambua mhusika.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alipotafutwa kuzungumzia tukio hili alisema yuko kwenye kikao cha kazi, ambapo Mwananchi inaendelea kumtafuta ili kupata maelezo zaidi na hatua zilizochukuliwa.

Hata hivyo, jeshi la polisi nchini limekuwa likiwasisitiza wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi wanapowakamata watuhumiwa.

Related Posts