Zanzibar kuwakutanisha wataalamu wa mafuta na gesi Afrika

Unguja. Wakati Zanzibar ikiendeleza jitihada za kuboresha sekta ya gesi na petroli, unatarajiwa kufanyika mkutano mkubwa utakaowakutanisha wataalamu wa sekta hiyo kutoka ndani na nje ya Afrika.

Mkutano huo utajadili mbinu mpya na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuendeleza rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.

Tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, imetangaza rasmi vitalu 10 vya mafuta na gesi asilia kwa ajili ya uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa rasilimali hizo.

Kati ya vitalu hivyo, vinane vipo katika maeneo ya baharini (offshore) huku viwili vikiwa nchi kavu (onshore), hatua inayoashiria dhamira ya Serikali kufungua fursa zaidi kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa katika sekta ya nishati.

Kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji, Serikali imekamilisha marekebisho ya modeli ya mkataba wa mgawanyo wa uzalishaji (Model Production Sharing Agreement – MPSA).

Marekebisho haya yanalenga kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata mazingira rafiki ya kufanya biashara huku yakilinda masilahi mapana ya Zanzibar na watu wake katika usimamizi endelevu wa rasilimali za mafuta na gesi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo leo Juni 24, 205,  Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi  Asilia Zanzibar, Dk Mwadini Juma Khatib, amesema kwa sasa kuna mwamko mkubwa kuhakikishaa sekta hiyo inakuwa kwa kasi kubwa.

“Sekta ya mafuta na gesi ni moja ya vipaumbele vitano vya uchumi wa buluu, vijana wamekuwa na mwamko wa kuona sekta ya mafuta na gesi inakuwa vizuri na kuomba wadau wengine kuunga mkono hitihada hizi ili sekta hii iendelee kukua zaidi,” amesema.

Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Jumuiya ya Vijana katika Sekta ya Mafuta na Gesi wanaotoka mataifa tofauti ya Afrika (Yapa), Jaffar Mohamed Hamza amesema  shughuli hiyo ni muelekeo au mtazamo mpya wa sekta ya mafuta na gesi.

Amesema lengo kubwa ni kutangaza zaidi sekta hiyo katika utumiaji wa teknolojia na mbinu mpya katika sekta ya gesi.

“Kutakuwa na wataalamu mbalimbali ambao wamebobea katika sekta hii kwa hiyo watabadilishana uzoefu, matumizi ya teknolojia na fursa zilizopo katika sekta hii, kwa hiyo mbali na wataalamu kutoa uzoefu wao kutakuwa na maonyesho mbalimbali yakayofanyika,” amesema.

Amesema jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono masuala mbalimbali ya Serikali ili kuona lengo linafikiwa ikiwemo la kuwapatia elimu za mafuta na gesi.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Juni 27 hadi 29 mwaka huu, ambapo lengo kuu ni kutoa elimu inayohusiana na mafuta na gesi sambamba na kutangaza utalii wa Zanzibar.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Rashid Simai Msaraka amesema huo ni ubunifu mzuri ambao utasaidia kuibua mambo mengi ya maendeleo ya nchi pamoja na kuonesha uwezo wa vijana wa nchi hasa katika masuala ya mafuta na gesi pamoja na utalii wa Zanzibar.

Mkutano huo abao ni wa kwanza kufanyika Zanzibar, utakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika na ulimwenguni unalenga kukuza sekta ya mafuta na gesi ikizingatiwa kwasasa mwelekeo wa Zanzibar ni kuwekza katika sekta hiyo.

“Niwapongeze kwa uthubutu vijana maana tunaamini kupitia mkutano huuu kuna mambo makubwa yapatikana nan a uzoefu utaongezeka katika sekta hii kwani tutakutana na wataalamu wakubwa duniani ambao wamepiga hatua kubwa,” amesema.

Related Posts